.

.

24 Mei 2016

JKCI YAFANYA UPASUAJI MKUBWA WA MOYO WA KUPANDIKIZA MISHIPA YA DAMU


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi akitia saini mkataba wa ushirikiano wa kutoa huduma na mafunzo kati ya JKCI na Hospitali ya Moyo ya BLK ya India. Kulia ni mwakilishi wa Hospitali ya Moyo ya BLK ya India akitia saini kuhusu mkataba huo.



Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete –JKCI- kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK kutoka nchini India kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (Buypass Surgury ) bila kuusimamisha moyo kwa kutumia mashine maalum inayoitwa Heart Lung Machine.


Upasuaji huo ni mkubwa wa kwanza na wa aina yake kufanyika hapa nchini na kwa kanda Afrika ya Mashariki na Kati .


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam , Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dk. Peter Kisenge amesema wataalam wa taasisi hizo mbili kwa mara ya tatu wameweza kutoa tiba kubwa ya moyo bila mgonjwa kupasuliwa kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa kuzibua Valvu zilizoziba( BMV Procedure ).


Wataalam hao wa Moyo ambao watakuwa hapa nchini kwa siku mbili watatoa mafunzo kwa watoa huduma wa Taasisi ya moyo ambapo wagonjwa watakaopewa huduma hii watafikia takribani 18 .


“ Taasisi itaokoa zaidi ya Shilingi Milioni 180 kwa siku mbili kama wagonjwa hawa wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu haya haya , na kubwa zaidi si fedha tu bali tumeokoa maisha ya watanzania wenzetu” amesema Dk. Kisenge.


Katika hatua nyingine, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imetia saini mkataba wa ushirikiano wa kutoa huduma na mafunzo na Taasisi ya BKL ya nchini India , lengo ni kuwapa mafunzo watumishi wake na kuendelea kutoa huduma ya upasuaji wa moyo kwa kushirikiana na taasisi ya BLK .


Kwa mwaka huu peke yake JKCI imefanya procedure 471 ikiwemo upasuaji wa Moyo kwa kufungua kifua 99, vipandikizi 78 , vizibua njia 265 na nyinginezo 29 .


Mbali na ushirikiano huu na Taasisi ya BLK , JKCI imeweza kufanikisha huduma hizi kubwa kwa kushirikiana na taasisi nyingine marafiki zikiwemo Al-Muntada ( Saudi Arabia ) Open Heart International ( Australia) , Save a Child’s Heart ( Israel) na Madaktari Afrika.


Kambi kama hizi zitaendelea tena Julai, Septemba na Novemba .
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya taasisi hiyo kufanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kupandikiza mishipa ya damu. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi na Mwenyekiti wa Hospitali ya Moyo ya BLK ya nchini India, Dk Subhash Chandra. Watu 18 watafanyiwa upasuaji wa njia hiyo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka India.
Mwenyekiti wa Hospitali ya Moyo ya BLK nchini India, Dk Subhash Chandra akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu upasuaji mkubwa wa moyo unaofanyika JKCI. Kulia ni Mwenyekiti wa Hospitali ya Moyo ya BLK ya India, Dk Ajay Kaul.
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji JKCI, Dk Bashir Nyangasa akiwaeleza waandishi wa habari jinsi walivyofanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa kutumia njia ya upandikizaji mishipa baada ya mishipa hiyo kutolewa sehemu ya miguuni ya mgonjwa. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi na Mwenyekiti wa Hospitali ya Moyo ya BLK ya India, Dk Subhash Chandra.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni