.

.

14 Julai 2015

SUGU AOMBA MIAKA MITANO ZAIDI


Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, amesema baadhi ya majukumu aliyopewa na wananchi hajayakamilisha, hivyo anasubiri uamuzi wa chama kuhusu hatima yake ya kuteuliwa tena kuwania ubunge.
Sugu alitoa kauli hiyo juzi wakati wa mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Ruanda, Nzovwe kuwashukuru wananchi wa jimbo hilo baada ya kuwawakilisha bungeni kwa miaka mitano.
Pamoja na kuelezea mambo aliyofanya, Mbilinyi alitumia nafasi hiyo kuwaonya wapinzani wake wanaotaka kumpinga kwenye jimbo hilo.
“Nawashukuru watu wangu wa Mbeya kwa kunipa heshima hii kubwa. Kujitokeza kwenu kunipokea kwa wingi inadhihirisha wazi sikuwaangusha,” alisema na kuongeza: “Kuna mambo bado sijayamaliza, nahitaji kipindi kingine ili niweze kumalizia.”
Akifafanua Mbilinyi aliwataka wananchi kuwachagua madiwani wa upinzani ili wapate maendeleo.
Kwa upande wao, viongozi wa Chadema wilaya, Mkoa wa Mbeya na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, waliwataka makada wenye nia ya kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali, waelekeza dhamira kwenye majimbo yanayomilikiwa na CCM. Mratibu wa Chadema kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema kuna majimbo 34, lakini ni majimbo manne yaliyokuwa yakishikiliwa na upinzani.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija alisema kitendo watu cha kujitokeza kwa wingi kumpokea mbunge wao ni ishara kwamba hakutakuwa na shida kumpata mgombea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni