Rais Jakaya Kikwete amelihutubia bunge la kumi na la mwisho
kwa uongozi wake ambapo ameainisha mafanikio ambayo yamepatikana tangu aingie
madarakani ikiwemo kupunguza matukio ya uhalifu na ujambazi na kuongeza kuwa
changamoto kubwa inayoikabili taifa hivi sasa ni tatizo la ajali za barabarani.
Viongozi mbalimbali wa serikali, marais na mawaziri wakuu
wastaafu pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini wamefika
bungeni mjini hapa na kushiriki kusikiliza hotuba ya rais ambapo mara baada ya
rais Kikwete kuwasili viwanja vya bunge wimbo wa taifa uliimbwa na baadae
akakagua gwaride liloandaliwa maalum kwa shughuli hiyo.
Katika hotuba yake rais Kikwete mbali na kuwashukuru wabunge
kwa ushirikiano waliompa na kazi kubwa walizofanya za kupitisha miswada
mbalimbali ya sheria amesema nchi iko salama na kuwahakikishia watanzania kuwa
atahakikisha anaiacha salama na kwamba serikali yake itaendelea kutatua
changamoto zilizopo hivi sasa kwa kipindi kilichobaki ikiwemo msongamano wa
wafungwa magerezani.
Awali kabla ya rais Kikwete kuhutubia bunge waziri mkuu Mh
Mizengo Pinda alihitimisha rasmi mkutano wa ishirini wa bunge huku akitangaza
wilaya mpya sita ikiwemo wilaya ya Ubungo na wilaya ya Kigamboni kwa jiji la
Dar es Salaam na akatumia nafasi hiyo kuwaaga na kuwashukuru wabunge kwa
ushirikiano waliompa katika kipindi chote tangu alipoteuliwa kushika wadhifa
huo.
Kwa upande wake spika wa bunge Mh Anne Makinda amewataka
watanzania kuimarisha tabia nzuri na amani iliyopo nchini na waache chokochoko
za hapa na pale hasa tatizo la kuumizana lililoanza kujitokeza ambapo baadhi ya
watu wameumizwa wakati wa zoezi la kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la
wapiga kura.
Tofauti na maudhurio ya vikao vya bunge vilivyokuwa
vinaendelea hapa bungeni idadi ya wabunge imeongezeka mara dufu wakati wa hotuba
ya rais licha ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni kutokuwepo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni