Sakata ya
usajili wa nahodha wa timu ya soka ya Tanzania, Mbwana Samatta
inaonekana kukamilika baada ya mshambulizi huyo kukubali kujiunga na
klabu ya ubelgiji ya KRC Genk.
Samatta maarufu Samagoal, ameanza safari ya kuelekea Ubelgiji ambapo anatarajiwa kusaini mkataba na klabu hiyo.
Ajenti wa nyota
huyo, Jamal Kisongo ametetea hatua ya Samatta kujiunga na Genk licha ya
Nantes kutoa donge nono Zaidi ya Genk huku akisema kuwa uamuzi huo ni
kwa minajili ya ufanisi wa Samatta.
''Wachezaji
wengi waTanzania wanaazimio la kucheza soka Ulaya na naamini fursa hiyo
itafika kwani hali ya sasa itafungua milango kupitia Genk''.
Kisongo
ameongeza kuwa mkataba huu mpya na Genk utawanufaisha pia wachezaji wa
Tanzania kwani makubaliano hayo yataiwezesha klabu hiyo kusaka vipaji
zaidi nchini Tanzania.
Samatta ambaye
pia ni mchezaji bora wa wachezaji wa nyumbani barani Afrika anatarajiwa
kupigania nafasi yake ya kikosi cha kwanza cha Genk.
''Ni muhimu kwa
Samatta kuingia na kucheza katika kikosi cha kwanza cha Genk na
inatarajiwa hali hio itamwezesha kutimiza ndoto hiyo,'' alisema Kisongo.
Uhamisho wa
Samatta unadaiwa kuzua utata baina yake na mmiliki wa klabu ya TP
Mazembe, Moise Katumbi kwani Katumbi alichagua Nantes ambayo ilitoa
kitita bora zaidi.
-Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011.
-Aliisaidia TP Mazembe kutwaa taji la vilabu bingwa barani Afrika.
-Alituzwa mchezaji bora Afrika.