.

.

21 Aprili 2016

MKUU WA MKOA WA MBEYA AMOSI MAKALLA AONJA MOTO WA UKAWA...MADIWANI 34 WAKIONGOZWA NA MEYA WAO WASUSIA KIKAO CHAKE CHA KUJITAMBULISHA.



Meya wa Jiji la Mbeya Mh Mch David Mwashilindi akiwa na madiwani wakitoka nje.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)



Madiwani Wakitoka ndani ya ukumbi (Picha na David Nyembe wa Fahari News)


Baadhi ya madiwani wa Chadema wakiondoka.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)

Meya wa Jiji la Mbeya Mh Mch David Mwashilindi akiondoka mara Baada ya kususia Kiakao cha Mkuu wa Mkoa.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto la Mbeya baada ya meya wa jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34 kususia kikao chake cha kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji hilo.
Meya alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda mfupi kabla ya Makalla kuanza kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi, wazee maarufu, viongozi wa dini na machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Nyirembe Sabi alimkaribisha Meya Mwashilindi kuzungumza chochote kwa niaba ya madiwani wake.
Hata hivyo, Meya Mwashilindi alipochukua kipaza sauti alisema: “Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakumbuka kwa mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba tufanye kazi, siasa zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii umekwenda Soko la Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala madiwani wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”
Baada ya kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti kwa mkuu wa wilaya, kisha akachukua nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia Chadema na kutoka ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi ni siasa ambazo tulizikataa, lakini wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi kupuuzwa kwa kiasi hiki.”
Mkuu wa Wilaya, Mnasa alisema anaamini taratibu na ratiba yote ilipangwa vizuri hivyo hawaoni sababu ya madai ya madiwani hao kwamba hawakushirikishwa kwenye ziara hiyo, wao kama wawakilishi wa Rais hawaangalii siasa, bali wanaangalia uchapakazi na siyo masuala ya siasa.
Akizungumzia kitendo cha meya na madiwani wake kususia kikao hicho, Makalla alisema ‘Nashangazwa na uamuzi wa madiwani hawa kwa kitendo hiki, kwani siku ile nilipotembelea Shule ya Sekondari Iyunga, nilisema kwamba Aprili 20 ambayo ndiyo leo (jana) nitakuwa na ziara ya jiji na kabla ya kikao nitataka kutembelea Soko la Mwanjelwa,” alisema Makalla.
Alisema suala la meya na madiwani wake kutoshirikishwa kwenye ziara ya kwenda Soko la Mwanjelwa halimhusu, kwani mwenye wajibu wa kupeana taarifa ni kwenye ngazi ya halmashauri ya jiji, lakini siyo yeye (Makalla).
“Jamani mimi sijaja kufanya siasa nimekuja kufanya kazi ya wananchi na nilishatahadharisha jambo hili, sasa kwa kitendo hiki ndiyo siasa na wananilazimisha kufanya siasa, lakini wao ndiyo watahukumiwa na wananchi. Na ninasema kama Mola ataendelea kunilinda kubaki katika mkoa mwaka 2020 nitakwenda kuwaambia hiki kinachofanyika sasa na wawakilishi wao,” alisema Makalla.
Awali Makalla akiwa katika Soko la Mwanjelwa alinusa harufu ya ufisadi kwenye soko hilo na kuagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoa huo, kufanya uchunguzi ndani ya wiki nne wa uhalali wa fedha kiasi cha Sh22.9 bilioni iliyotumika katika ujenzi huo ukiwa ni mkopo kutoka Benki ya CRDB.
Makalla alitoa agizo hilo jana mchana baada ya kutembelea soko hilo na kuzungumza na wafanyabiashara wa jijini hapa, ambao walimueleza wanashindwa kumudu gharama ya upangaji ya vyumba vya biashara ambayo inaanzia kiasi cha Sh500,000 kwa chumba kimoja kwa mwezi, ndiyo maana hawataki kuingia ndani ya soko hilo.
Mwenyekiti wa soko hilo, Peter Chacha alimueleza Makalla kwamba wasipokuwa makini soko hilo litabaki gofu, kwani wafanyabiashara hawataki kuingia kwa kuogopa gharama kubwa ya vyumba hivyo, alimuomba afanye awezalo kukaa chini na uongozi wa benki ambao unadai fedha zao kwa jiji na kuona namna ya kupunguziwa gharama hiyo.
“Ni kweli wenzetu jiji, wametingwa na deni la mkopo kutoka Benki ya CRDB, ndiyo maana wamekuja kutubana sisi wafanyabiashara kwa kutupangia chumba kuanzia Sh500, 000 hadi Sh 800,000, kitu ambacho hatuwezi kumudu hata kidogo,”alisema Chacha
Baada ya kusikiliza kilio cha wafanyabiashara hao, Makalla alisema kiasi cha Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi wa soko hilo haiendani na thamani yake, hivyo vyombo vya dola vikiongozwa na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, wanafanya uchunguzi wa kina na kuwanasaka wale wote waliohusika kwenye mchakato mzima wa ujenzi wa soko hilo.
“Nataka kupata taarifa ya mchanganuo mzima wa namna ya fedha ilivyokopwa, ilivyotumika na mkataba wake ulivyokuwa ndani ya wiki nne, taarifa hii niipokee na wale watakaobainisha kufuja fedha watapelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
"Kwenye hili, kuna watu waliotufikisha hapa, Sh22.9 bilioni iliyotumika kwenye ujenzi huu haiendani na ujenzi wa soko hili, kuanzia muda uliotumika na gharama ya kodi ya upangishaji wa vyumba siyo rafiki ni kubwa mno, hivyo jiji na CRDB mkae muone namna ya kupunguza gharama hiyo, kwani hali ilivyo sasa lile soko litabaki gofu."
 CREDIT FAHARI NEWS

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni