.

.

21 Juni 2016

JE WAJUA KUWA NGUCHIRO NDIYE MNYAMA BINGWA WA KUUA NYOKA NA ANAE MUOGOPA COBRA?



Nguchiro-Jangwa


JE WAJUA?
Nguchiro bingwa wa kuua nyoka anayeogopa cobra

NGUCHIRO ni mnyama mdogo jamii ya panya, anayepatikana kwa wingi barani Afrika na kusini mwa mabara ya Ulaya na Asia.

Kuna kama jamii 33 hivi za nguchiro. Lakini kuna jamii nyingine nne za ziada ambazo hupatikana huko Madagascar.

 Hawa ni jamii ndogo ya Galidiinae. Awali, jamii hizi nne ziliwekwa katika kundi la wanyama wengine wanaopatikana huko Madagascar lakini baadaye ikaja kujulikana kuwa wana sifa tofauti, hivyo kuundiwa makundi yao yanayojitegemea.

Utafiti wa kijenetiki unaonyesha kuwa Galidiinae wana uhusiano wa karibu na wanyama wengine wa familia ya Eupleridae, ambao wanakaribiana sana na nguchiro.

Mwonekano

Kama tulivyodokeza hapo juu, nguchiro hupatikana kwa wingi katika maeneo ya Afrika na kusini mwa Ulaya na Asia. Lakini pia kwa kiasi kidogo hupatikana huko Puerto Rico na sehemu ya visiwa vya Caribbean na Hawaiian.

Lakini huko walipelekwa kama wanyama wa kufugwa na kupambana na wanyama waharibifu na hatari kama vile panya na nyoka.

 Kuna jamii kuu 33 za nguchiro ambao kwa wastani ukubwa wao ni kati ya futi moja na nne kwa urefu. Uzito wa nguchiro unatofautiana sana kulingana na jamii husika.

Wapo nguchiro wadogo ambao uzito wao ni kama gramu 280 tu wakati wapo wengine wakubwa ambao hufikia uzito wa zaidi ya kilo nne.

 Baadhi ya jamii ya nguchiro huishi maisha ya upweke huku kila mmoja akijitafutia chakula chake mwenyewe.

Lakini zipo jamii nyingine ambazo nguchiro huishi katika kundi kubwa, wakisafiri na kufanya mambo mengine pamoja kama vile kutafuta na kugawana chakula. 

Nguchiro anafanana sana na mnyama mwingine ajulikanaye kama
Mustelids. Wote wana sura ndefu na miili mirefu pia. Wana masikio madogo ya duara, miguu mifupi na mikia mirefu. Wengi wana manyoya machache sana mwilini, ni wachache tu ndio wana manyoya mengi.

Vidole vyake vina kucha lakini kucha hizi hutumika sana kwa ajili ya kazi ya kuchimba. Kama ilivyo kwa mbuzi, nguchiro wana macho madogo sana.

 Wengi wa jamii za nguchiro wana vifuko kwenye sehemu yao ya makalio vyenye kemikali inayotoa harufu ambayo huitumia kuweka mipaka na himaya ya maeneo yao. Pia, harufu hii hutumika kuashiria kuwa mnyama fulani yupo tayari kwa ajili ya kujamiiana.

 Kama ilivyo kwa nyoka, nguchiro naye ana aina fulani ya mfumo ambao unazuia mwili wake kudhurika na sumu. Wataalamu bado wanaendelea kutafi iwapo hii ndiyo sababu mnyama huyu hadhuriki na sumu ya nyoka.

Historia
Nguchiro mwembamba (Galerella sanguinea)
Tofauti na wanyama wanaofanana naye kama vile viverrids, nguchiro ni mnyama ambaye hufanya shughuli zake nyakati za mchana wakati wale wengine hujishughulisha zaidi usiku.

 Nguchiro wa Misri ndiye anayetambulika kama nguchiro anayependa kutembea peke yake. Hata hivyo, kuna wakati nguchiro hawa nao hutembea katika makundi.

 Nguchiro jamii ya Meerkat au kwa jina jingine Suricate (Suricata suricatta), ambao wana umbo dogo, wanaishi katika makundi ya hadi wanyama kati ya 20 na 30.

Katika kila kundi kunakuwa na dume mkubwa mmoja na jike wake. Huwa wanaambatana na watoto wao na vijukuu na vitukuu. Hawa hupatikana pia katika maeneo ya wazi huko kusini mwa Afrika katika nchi kama Angola, Namibia, Botswana na Afrika Kusini.

Jamii nyingine ya nguchiro ijulikanayo kama meerkat; ni wadogo kwa umbo ambao chakula chao kikuu ni wadudu na wanyama wadogo wadogo na nyoka. Udogo wa umbo na uzito mdogo ni mambo yanayomfanya awe hatarini sana kushambuliwa na wanyama wakubwa walao nyama na hata ndege wakubwa kama tai. Hata hivyo, naye huwakamata ndege wadogo wadogo na kuwala.

 Kama njia ya kujilinda katika kundi, nguchiro mmoja hufanywa mlinzi wakati wengine wakitafuta chakula.

Huyu hukaa sehemu iliyoinuka na kusimama kwa miguu miwili ya nyuma ili kumwezesha kuona mbali na pande zote.

 Anapoiona hatari, hutoa sauti kali ili kuwashitua wenzake kuwa kuna hatari inawanyemelea. Pamoja na sauti hiyo pia hutoa ishara hatari inatokea upande gani, kama ni angani au ardhini ili kuwawezesha wenzake kuchukua hatua zinazofaa kujilinda.

Chakula

Chakula kikuu cha nguchiro ni wadudu, kaa, minyoo, mijusi, nyoka, ndege na panya. Pia hula mayai.

 Nguchiro wa kijivu wa huko India na wengine wanafahamika kwa uwezo wao mkubwa wa kuwashambulia na kuwaua nyoka hata wale wenye sumu kali kama vile cobra.

Inaaminika kuwa wanaweza kufanya hivi kutokana na ukali wao na ngozi yao ngumu.

Lakini kikubwa zaidi ni kemikali iliyomo mwilini mwao, ambayo inazuia sumu ya nyoka kuingia kwenye damu na misuli. Ingawa nguchiro ana uwezo wa kuwinda nyoka, lakini mara nyingi hujiepusha sana kuwinda cobra.

Nguchiro miriba
Nguchiro pia anaweza kufugwa na kutumika kama mnyama wa kupambana na panya ndani ya nyumba kama vile anavyotumika paka.

 Hata hivyo, pamoja na kuzuia panya, nguchiro anayefugwa anaweza kuwa mwaribifu. Wakati nguchiro walipopelekwa huko West Indies kwa ajili ya kuua nyoka na panya, waliharibu pia mimea hasa ile midogo midogo ambayo nayo huitafuna kama sehemu ya mlo wao.

 Kutokana na sababu hii, hivi sasa ni kinyume cha sheria kupeleka aina yoyote ya nguchiro huko Marekani na Australia. Nguchiro walipelekwa katika Kisiwa cha Hawaii mnamo mwaka 1883 na tangu wakati huo wameonekana kuwa na madhara kwa wanyama wenyeji wa eneo hilo.

Uhusiano na binadamu

Nguchiro hupenda sana kuishi karibu na makazi ya watu. Hivyo mara nyingi huonekana wakikatiza barabara na nyakati za usiku wengi hugongwa na magari.

 Huko Pakistan, watu wanaocheza na nyoka huwafuga nguchiro na kuwafundisha kupigana na nyoka na huwatumia kama sehemu ya michezo yao.

 Zamani huko Okinawa nchini Japan, nguchiro waliletwa ili kupambana na nyoka aitwaye Habu, lakini kutokana na mbinyo wa watetezi wa haki za wanyama, suala hilo limeachwa siku hizi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni