Zahma inayokumba wahamiaji wanaovuka Mediteranea wakisaka usalama na maisha bora Ulaya imechukua sura mpya baada ya gazeti moja nchini Uingereza kuwafananisha na kombamwiko.
Kufuatia makala iliyochapishwa na gazeti hilo Sun la tarehe 17 mwezi huu, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra'ad Al Hussein amesema jambo hilo linaeneza chuki dhidi ya wageni na ubaguzi na halikubaliki kwa mujibu wa sheria za kimataifa na mikataba ambayo Uingereza imeridhia.
Taasisi moja ya kiraia nchini humo imetaka uchunguzi ufanyike na msisitizo wa Kamishna Zeid unafafanuliwa na msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva, Rupert Colville.
"Kamishna Mkuu anasihi Mamlaka za Uingereza kuchukulia malalamiko hayo kwa umakini na kuchunguza kwa karibu uchochezi wa chuki unaofanywa na magazeti na sekta nyingine kwenye jamii."
Kamishna Zeid amesema historia inadhihirisha tena na tena hatari za kuendelea kunyanyasa wahamiaji akieleza hilo ni jambo la aibu na ni mbinu zinazotumiwa na nchi mbali mbali kwa kuwa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni husaidia kupata kura na kuuza magazeti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni