Mabingwa wa Tanzania bara na wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia katika michuano ya CAF, timu ya Yanga SC chini ya mkufunzi, Hans Van der Pluijm siku ya leo Jumatano itashuka uwanjani kuwakabili mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi ya mabingwa Afrika, timu ya Al Ahly ya Misri huko jijini Alexandria.
Wakati usiku wa jana Watanzania walishuhudia timu yao (Azam FC) ikitupwa nje ya michuano ya Shirikisho na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya magoli 4-2, Yanga wataingia uwanjani mida ya saa 3 usiku wakiwa mguu mmoja nje ya michuano hiyo kwani watalazimika kwa namna yoyote kuhakikisha wanapata goli la ugenini ili kufuta goli la kikosi cha kocha Martin Jol walilopata jijini, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Maandilizi yote muhimu tayari yamekamilika na wachezaji wote wako fiti kwa mchezo. Tunaomba Watanzania wenzetu waendelee kutuombea, sisi kama timu tumejiandaa kupambana ili kuhakikisha tunapata matokeo yatakayotupeleka katika hatua ya makundi.” anasema mkuu wa kitengo cha habari wa klabu hiyo, Jerry Murro wakati nilipofanya naye mahojiano mafupi usiku wa Jumanne akiwa nchini Misri
Ikumbukwe kuwa mchezo wa kwanza baina ya timu hizo (Yanga v Al Ahly) ulimalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1 hivyo basi Yanga watalazimika kushambulia kwa nguvu ili kupata goli ambalo litawarejesha katika michuano.
Ikiwa na washambuliaji wake watatu, Saimon Msuva, Amis Tambwe na Donald Ngoma ‘MTN’ waliofunga magoli 40 katika michezo 24 ya ligi kuu Bara, Yanga inatambua kuwa kushindwa kufunga katika mchezo wa leo walau goli moja tu wataondolewa katika michuano hiyo na kuangukia katika ‘kapu’ la kuwania kufuzu kwa michuano ya shirikisho hatua ya makundi.
Tumeshazungumza mengi kuhusu tofauti kubwa iliyopo kati ya Yanga na Al Ahly na namna timu hiyo namba moja kwa ubora barani Afrika inavyowanyanyasa Yanga kila wanapokutana katika ardhi ya Misri.
Katika michezo minne waliyokutana nchini Misri katika miaka tofauti, Yanga imepoteza yote, lakini imani ni kubwa na pengine hii ni nafasi yao nyingine ya kufuzu kwa michuano ya makundi ambayo walifuzu kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1998-takribani miaka 18 iliyopita.
Yanga watapaswa kujilinda vizuri, kocha Hans atawapanga nahodha, Nadir Haroub, Kelvin Yondan na Vicent Bossou katika beki ya kati ili kuhakikisha golikipa Deogratius Munish ‘Dida’ akiwa salama.
Juma Abdul ambaye alibanwa sana katika game ya kwanza ataanza katika beki namba 2 na Mwinyi Hajji ambaye hakucheza michezo dhidi ya Mwadui FC na Mtibwa Sugar katika ligi kuu, yeye atarejea katika beki 3 ili kutengeneza ukuta wa watu watano.
Haruna Niyonzima ambaye hakucheza game ya kwanza kutokana na kutumikia kadi tatu za njano, atarejea katika game hii ya Leo kuongeza nguvu na ubunifu katika idara ya kiungo sambamba na ‘pacha’ wake Thaban Kamusoko.
Hans anakabiliwa na mtihani wa kufanya chaguo la kuanza mechi kati ya kiungo wa pembeni, Deus Kaseke na Msuva. Ili kuwacheza walinzi wake wote watatu wa kati (Nadir, Kelvin, na Bossou,) kocha Hans atalazimika kumuweka bechi mmoja kati ya Msuva na Kaseke.
Msuva ni mshambuliaji mzuri mwenye kasi na ametoka kufunga magoli mawili katika game mbili za mwisho za VPL lakini amekuwa mzito na asiye na msaada katika kukaba wakati Kaseke licha ya kwamba si mfungaji wa mara kwa mara ila hukaba vizuri na kusaidia utengenezaji wa magoli.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni