Wananchi wa kijiji cha Ubetu kata ya Ubetu
kahe wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wanalazimika kwenda nchi jirani ya Kenya
kufanya vibarua mashambani na biashara ndogondogo ili kuweza kupata fedha za
kujikimu kuhudumia familia ikiwemo kulipia watoto ada za shule.
Wakizungumza wakati wa zoezi la kusaidia kaya maskini
kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF awamu ya tatu wananchi hao ambao wengi
wao ni wananwake wamesema wanalazimika kufanya vibarua ili kupata fedha za
kuhudumia familia kupata chakula na kusomesha watoto.
Wamesema wanawake wengi wanalazimika kubeba jukumu la
kuhudumia familia kutokana na wanaume kutojishughulisha mara baada ya kunywa
pombe na hivyo kukuta familia inashindwa kupata hata mlo mmoja wa chakula.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw.Damas Tarimo amekiri
wananchi wa eneo hilo kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinawalazimu
kwenda kutafuta vibarua nchi jirani ya Kenya kutokana na kukabiliwa na uhaba wa
chakula ambao umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa upande wake afisa ushauri na ufuatiliaji mfuko wa
TASAF wilaya ya Rombo Bw.Jimmy Mongi amesema kutokana na changamoto hizo mfuko
huo umeweza kuibua kaya maskini 6834 ambazo zitapatiwa fedha kiasi cha zaidi ya
shilingi milioni 238 kwaajili ya kuanzisha miradi midogomidogo ya kiuchumi
ambayo itawawezesha kujikwamua na umaskini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni