Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa lugha ya
matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es
Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana akili na
mpuuzi.
Askofu Gwajima
alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu
Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya Machi 16 na 25,
mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe jijini
Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi Askofu
Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja, amekula
nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’ alinukuu
maneno hayo.
Alidai kuwa
Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi ya Askofu Pengo na
kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Upande huo wa
Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa alifikishwa Kituo cha
Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.
Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.
Hata hivyo,
Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri majina yake,
wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.
Wakati huo huo,
mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya awali ya kesi
inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa nne
kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.
Mbali na Gwajima wengine ni anayedaiwa kuwa mlinzi wake George Mzava,Yekonia Bihagaze na Georgey Milulu.
Katika kesi ya
msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika
Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, jijini Dar es Salaam,washtakiwa
kwa pamoja walikutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta yenye namba ya
siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na
silaha na milipuko.
Alidai kuwa
washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) na cha
34 (1)(2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya 223
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
Upande wa
Jamhuri, uliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio Mzava akiwa na wenzake
hao walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na
risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa walikana mashitaka yao
kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni