Jumatatu, Januari 25, 2016
Jumatatu, Januari 25, 2016
WAZIRI wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mh. Profesa Makame Mbarawa amemteua
aliyekuwa Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), Mhandisi George Sambali kukaimu nafasi ya Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kufuatia kifo cha
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Suleiman S.
Suleiman.
Mhandisi
Suleiman alifariki dunia tarehe 18 Januari, 2016 wakati akipelekwa
katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam baada ya kuishiwa nguvu
ghafla akiwa katika mazoezi ya kuogelea katika eneo la Feri, jijini Dar
es Salaam.
Akitangaza
uteuzi huo kwa niaba ya Waziri Mbarawa mbele ya Menejimenti ya TAA
Jumatano tarehe 20 Januari, 2016 katika Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka
hiyo kwa niaba ya Mh. Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuliho, alisema uteuzi
wa Mhandisi Sambali umeanza rasmi tarehe 20 Januari, 2016.
Mhandisi George
Sambali alizaliwa mwaka 1965, mkoani Tabora na ana shahada ya Uzamili ya
Sayansi Uhandisi Uchukuzi na Barabara (MSc. Transportation (Transport
& Road) Engineering, aliyoipata mwaka 1999- 2001 nchini Uholanzi.
Mhandisi Sambali
alihitimu shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Uhandisi Ujenzi (BSc.Civil
Engineering) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1995 .
Mhandisi Sambali
pia amepata mafunzo na kozi mbalimbali za masuala ya anga kutoka katika
vyuo vya hapa nchini na nje ya nchi, ikiwemo Stashahada ya Uongozi wa
Viwanja vya Ndege (Certificate in Airport Executive Leadership) mwaka
2014 huko Montreal, Canada.
Pia mwaka 2015
alitunukiwa Stashahada ya Wataalamu wa Kimataifa wa Viwanja vya ndege
(Post-Graduate Diploma in International Airports Professionals (AIP)
chini ya AMPAP nchini Canada.Mhandisi Sambali aliajiriwa na TAA mwaka
2001 kama Meneja Mipango, Usanifu na Uthamini (Manager Design, Planning
and Evaluation) na mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma
za Uhandisi na Ufundi.
Mwaka 2013,
Mhandisi Sambali aliteuliwa kuwa Mshauri Maalum wa Mkurugenzi Mkuu kabla
ya mwishoni mwa mwaka jana kuteuliwa tena kuwa Kaimu Mkurugenzi wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Mhandisi Sambali
ni mwanachama kwenye vyama mbalimbali vya kitaaluma kikiwemo cha
Wataalamu wa Kimataifa wa Viwanja vya Ndege chini ya Baraza la Viwanja
vya Ndege Duniani (ACI) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga
(ICAO).
Pia Mhandisi
Sambali ni Mjumbe wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET); Mjumbe katika
Jukwaa la Kimataifa la Uendeshaji wa Uchukuzi Vijijini (IFRTD); na Bodi
ya Usajili wa Wahandisi (ERB).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni