KUFUATIA
malalamiko ya klabu kadhaa za Ligi Kuu Bara juu ya Azam FC kuruhusiwa
kwenda nchini Zambia wakati ligi hiyo ikiendelea, Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) limeibuka na kuomba radhi juu ya kitendo hicho.
TFF
iliipa ruhusa Azam kwenda Zambia kushiriki michuano maalumu
iliyoandaliwa na timu ya Zesco ya nchini humo ambapo kikosi hicho
kiliondoka Jumatatu ya wiki hii na kusababisha michezo yao miwili
kupigwa kalenda, hali ambayo imezua taharuki miongoni mwa timu za ligi
kuu ambazo nazo zimekuja juu na kutaka zipewe ruhusa ya kusafiri.
Rais wa TFF,
Jamal Malinzi, jana alizungumza na wanahabari na kusema kuwa wanaziomba
radhi timu za ligi kuu kwa kitendo kilichotokea cha kuipa ruhusa Azam
kwa kuwa hakikuwa katika utaratibu mzuri.
“Kiukweli
tunaomba radhi kwa kitendo ambacho tumekifanya kwa kuipa Azam ruhusa ya
kwenda Zambia hali ambayo imezua taharuki kwa timu nyingine na
kusababisha wao pia kuomba ruksa ya kwenda nchi mbalimbali, lakini
tutajitahidi kuwabana pale watakaporudi kwa kuwachezesha mara mbili kwa
wiki ili kuwafanya wawe sawa kimichezo na wenzao.
“Lakini niseme
tu kuwa tumekosea kwa Azam lakini hatutaki kuona timu nyingine
zinachukulia mwanya huo nao kuleta barua zao kwa kutaka kwenda nje ya
nchi kama ilivyofanyika kwa timu hiyo.
“Hatutakuwa
tayari kufanya jambo ambalo tumelikosea na tunasema hatutaipa ruhusa
timu yoyote ile hata hawa Yanga ambao nimesikia wanaomba kwenda Afrika
Kusini safari hiyo haitakuwepo, watambue hilo,” alisema Malinzi.