Mji mmoja kaskazini mwa Italia unasherehekea kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza tangu mapema miaka ya 1980.
Meya wa mji wa
Ostana, ulioko eneo lenye vilima la Piedmont, anasema kuzaliwa kwa mtoto
huyo ni “kutimia kwa ndoto” ya jamii ndogo inayoishi katika mji huo.
Idadi ya watu
katika mji huo imeshuka sana katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, na
walikuwa wamesalia watu 84 pekee na ni nusu yao pekee huishi katika mji
huo bila kuhamahama, Gazeti la La Tampa linasema.
Mtoto Pablo, aliyezaliwa katika hospitali moja mjini Turin amefikisha idadi ya watu mjini humo hadi 85 sasa.
Meya Giacomo
Lombardo anasema mji wa Ostana ulikuwa na watu 1,000 mapema miaka ya
1900 lakini wakaanza kupungua baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
"Watu walipungua
zaidi kuanzia 1975, ambapo ni watoto 17 pekee waliozaliwa kati ya 1976
na 1987, ambapo mtoto wa mwisho – mvulana- alizaliwa,” anasema.
Tangu wakati huo, hakuna mtoto mwingine aliyezaliwa hadi sasa mji huo ulipompokea Pablo.
Mji huo unajaribu kukabiliana na hali ya kushuka kwa idadi ya watu kwa kuunda nafasi za kazi.
Wazazi wa Pablo,
Silvia na Jose, walikuwa wamepanga kuhamia ng’ambo miaka mitano
iliyopita lakini ripoti zinasema waliamua kukaa baada ya kupewa kazi.
Sherehe kubwa
imeandaliwa mjini Ostana, kusherehekea kuzaliwa kwa Pablo, na kwa mujibu
wa La Stampa, sanamu ya korongo imewekwa kwenye lango la kuingia mji
kwa heshima yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni