Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei kikomo ya
mafuta, ambapo bei ya dizeli imeshuka kutoka Sh. 1,747 hadi Sh 1,600,
likiwa ni punguzo la Sh. 147 kwa lita.
Kadhalika, bei
ya mafuta ya petroli imeshuka kwa Sh. 55, hivyo kufanya mafuta hayo
kuanzia leo kuuzwa kwa bei isiyozidi Sh. 1,842 kutoka Sh. 1,898 kwa lita
kama kilivyokuwa ikiuzwa mwezi uliopita.
Taarifa
iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix
Ngamlagosi, ilieleza kuwa, kupungua kwa bei ya mafuta kwenye soko la
ndani kwa kiasi kikubwa kumetokana na kushuka kwa bei ya nishati hiyo
katika soko la dunia na pia kushuka kwa gharama za usafarishaji na
bidhaa za mafuta hayo kuja nchini.
Ngamlagosi
alisema kushuka kwa namna hiyo kulitokea Machi, mwaka jana, lita moja ya
mafuta ya dizeli ilishuka hadi kufikia Sh. 145 na dizeli kuzwa kwa Sh.
1,563 kwa lita.
Mkurugenzi huyo
wa Ewura aliwaomba wananchi kupuuza uvumi unaoenezwa kuwa mamlka hiyo
haipendi kushusha bei za mafuta kwa kuwa kushuka kwake kutaadhiri
mapato.
Alisema tozo ya Ewura inatokana na kiasi cha lita za mafuta kinachouzwa na si kupanda kwa bei.
Aidha,
amewakumbusha wamiliki wa vituo vyote vya mafuta kubandika bei za bidhaa
za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana, yakionyesha bei ya
mafuta, punguzo, vivutio vya biashara na promosheni zinazotolewa na
kituo husika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni