Tunapoelekea
kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka ambayo inaanza kesho Ijumaa Kuu,
Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi, kuwa makini
katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali zao. Katika
kipindi cha sikukuu baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya
vitendo vya uhalifu. Hata hivyo, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika mikoa yote
kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza
na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi
umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za
bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na
mikusanyiko mikubwa ya watu.
Aidha, Jeshi la
Polisi halitasita kumuwajibisha mzazi ama mlezi yeyote atakayeshindwa
kutunza mtoto wake na kusababisha mtoto huyo kupotea au kupata madhara.
Pia tunawataka wananchi wote kuwa wepesi katika kutoa taarifa pindi
wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama
maeneo ya biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa
ni 111 au 112.
Vilevile, Jeshi
la polisi linawataka wananchi kuwa makini na watu wanaojipatia kipato
kwa njia za utapeli kwa kutumia simu na mitandao. Mtu yeyote asikubali
kutaja taarifa zake binafsi kwa mtu asiyemjua, mfano kutaja namba ya
siri ya akaunti anayotumia kuhifadhia pesa katika simu, ama kutuma pesa
kwa mtu ambaye huna uhakika naye.
Jeshi la Polisi
linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa
makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva
wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba
mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi
hovyo.
Tunawatakia watanzania wote Pasaka njema.
Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni