Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo la kukaangia samaki kwenye soko la
samaki Feri la jijini Dar es salaam Machi 22, 2016, Kushoto kwake ni
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mama Lishe wakati alipotembelea
soko la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia Mama Lishe wakati alipotembelea soko
la samaki la Feri jijini Dar es salaam Machi 22, 2016.
*************
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya soko la Kimataifa la Samaki la
Feri, kukutana na makampuni mbalimbali yanayouza gesi ili kupata kampuni
inayouza kwa bei nafuu zaidi lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama
wakaangaji wa samaki sokoni hapo.
Pia
Waziri Mkuu Majaliwa alimtaka Meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi
kuhakikisha wanakuwa na kifaa maalumu cha kupimia ujazo wa mitungi ya
gesi sokoni hapo ili kubaini kama ni sahihi.
Ametoa
agizo hilo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara
ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo
la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo ambapo aliridhishwa na
unavyofanya kazi.
Waziri
Mkuu ambaye ametumia dakika 44 kulitembea soko hilo, alitoa maagizo
hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara ambao
wamesema wamekuwa wakiuziwa gesi kwa bei kubwa ambayo imekuwa
ikiongezeka mara kwa mara.
Akizungumza
kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Bw. Ally Iddi amesema awali walikuwa
wanauziwa mtungi wa gesi wenye ujazo wa kilo 32 kwa sh. 70,000 na sasa
umeongezeka hadi sh. 98,000 kiasi ambacho ni kikubwa ukilinganisha na
uzalishaji wao. “Nimeulizia kwenye baadhi ya maduka na kukuta mtungi
wenye ujazo kama huo unauzwa sh. 75,000,” alisema.
Kijana
mwingine ambaye ni mkaangaji wa samaki, Bw. Mwanya Selemeni alisema
hivi sasa hali ya soko la feri ni nzuri tofauti na walivyokuwa wakitumia
kuni kwa sababu hakuna moshi. Alimuomba Waziri Mkuu ahakikishe
wanafikishiwa gesi ya kutoka Mtwara ili gharama ziweze kupungua.
Mfanyabiashara
mwingine wa soko hilo, Bi. Mariam Samweli ambaye alikuwa akiuza kuni na
sasa yeye na wenzake wanataka kufanya biashara nyingine lakini banda
walilokuwa wakilitumia halina umeme licha ya kuwa wameomba mara nyingi.
“Tunaomba kupatiwa umeme ili tuweke vipepeo tuweze kufanya biashara
nyingine,” alisema.
Waziri
Mkuu pia alitembelea eneo la mnada wa kuuza samaki sokoni hapo ambako
alielezwa matatizo ya umeme na uzibaji wa mitaro ya maji machafu hali
ambayo inatishia usalama wa afya zao.
“Kuna
jipu la umeme hapa, tunachangishwa hela na kumpa mtu ambaye hatumjui
lakini hatujawahi kuona risiti, wao wanaweka umeme juu kwa juu na umeme
wenyewe wala haukai. Mita tunayo hapa lakini hata namba hatujapewa,”
alisema Bw. Omari Masoud kwa niaba ya wenzake.
Kuhusu
tatizo la uzibaji mitaro na kutiririsha majitaka, kiongozi wa mama
lishe sokoni hapo, Bi. Fatma Ally aliomba watatuliwe tatizo hilo ambalo
limedumu kwa zaidi miezi miwili.
Akijibu
kero zao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Raymond
Mushi asimamie suala la kuweka umeme kwenye hilo banda pamoja ahakikishe
mama lishe wa soko hilo upande wa mnadani waanze kutumia majiko ya gesi
badala ya mkaa.
Kuhusu
mitaro, alimwagiza meneja wa soko hilo, Bw. Solomon Mushi aimarishe
uzibuaji wa mitaro katika soko hilo. “ Mwambie mkandarasi azibue mitaro
kila siku jioni na watumiaji wa soko waache kutumia mifuko ya plastiki
kwa sababu inapoingia kule inaziba na wala haiozi,” alisema.
Aliwataka
wafanyabiashara waimarishe usafi kwa sababu ni sehemu ya chakula.
“Lengo letu ni kufanya soko hili liwe kwenye viwango vya kimataiafa ili
mteja anapokuja kununua samaki wabichi ama wa kukaanga awe na chaguo,”
alisema.
Kwa
upande wake, Meneja wa soko hilo, Bw. Mushi alisema bodi ya soko hilo
ambayo imeundwa hivi karibuni itakutana kesho kwa mara ya kwanza na
miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni maelekezo yaliyotolewa na Waziri
Mkuu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni