WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali aende
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili akague taarifa za mapato ambazo
zilikuwa zikilipwa na mawakala wa forodha na bandari kupitia benki ya
CRDB lakini hazionekani kwenye mifumo ya benki.
Ametoa agizo
hilo leo jioni (Jumatatu, Machi 17, 2016) wakati akizungumza na mamia ya
mawakala wa forodha na bandari waliohudhuria mkutano aliouitisha ili
kusikiliza kero zinazowapata katika utendaji kazi wao.
Akizungumza na
mawakala hao kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu
alisema kuna dalili za kutupiana lawama baina TPA na CRDB kuhusu malipo
yaliyikuwa yakifanyika benki halafu fedha hazionekana na wakala
anaidaiwa kuwa hajalipia mzigo wakati alishaulipia.
"Kimsingi bado
liko tatizo baina ya Mamlaka ya Bandari pamoja na Benki ya CRDB. Naona
kila mmoja hapa anamkana mwenzake. Nitamtuma CAG ili akafanye ukaguzi wa
kina ili tujue ni nani kati yao amehusika na upotevu wa fedha,” alisema
huku akishangiliwa na mawakala hao.
Alimwagiza pia
Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei aandae dispatch zote
walizotumia kupokelea malipo za kuanzia mwaka 2015 na ikibidi aandae za
kuanzia mwaka 2014 ili CAG anapozopitia aweze kupata picha halisi.
Vilevile, Waziri
Mkuu alimwagiza Eng. Matei kuhakikisha wananunua mashine ya photocopy
ili iwekwe kwenye chumba cha kupokelea stakabadhi za malipo ya benki
(bank pay in slip) ili mteja anapoleta nakala ya benki aweze kutolewa
photocopy na kubakia na nakala ya malipo aliyofanya.
Waziri Mkuu
alisema Serikali inatambua bandari ni eneo nyeti katika kuinua uchumi na
mapato ya nchi lakini pia ni eneo muhimu katika kutengeneza ajira.
“Ninapenda
niwahakikishie kuwa bado tutaendelea kukagua bandari hadi pawe safi. Hii
bandari ni yenu na mtafanya kazi kama kawaida,” alisema.
Mapema,
akizumgumza kwa niaba ya mawakala hao, Rais wa Chama cha Mawakala wa
Forodha nchini (TAFFA), Bw. Stephen Ngatunga alieleza matatizo
mbalimbali ambayo wao kama mawakala wa forodha wamekuwa wakikumbana nayo
kuanzia ulipaji, utoaji wa mizigo na kuitaka Serikali iongeze nguvu
katika kuikabilia sekta hiyo.
Alizikosoa
baadhi ya sheria ambazo zinaruhusu wamiliki wa bandari kavu kumiliki pia
makampuni ya uwakala wa forodha, sheria kadhaa zinazochangia kukwamisha
utoaji wa mizigo bandarini, ukaguzi hafifu wa kwenye scanner na uwepo
wa vituo vinane vya mizani kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma ambavyo
vimegeuka kuwa kero kwa wasafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
Wakati huohuo,
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani
amesema Serikali imeamua kuyafungulia makampuni zaidi ya 150 ambayo
yalikuwa yamefungiwa kufanya kazi za uwakala wa forodha kutokana na
madai ya kuhusishwa na ukwepaji wa kodi.
“Hapa tumegundua
kuwa wote siyo wasafi iwe ni mawakala, benki ama bandari. Mkurugenzi wa
Bandari, kuanzia leo watu hawa waruhusiwe waanze kufanya biashara
lakini nyaraka za nyuma zisiguswe hadi CAG atakapokamilisha uchunguzi
wake,” alisema kuibua kelele za shangwe kwenye ukumbi huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni