Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makalla akitoka chuoni hapo Mara Baada ya Kukifungia Chuo hicho.(Picha na David Nyembe wa Fahari News) |
Vilio kwanafunzi wa chuo hicho vilitawala. |
mkurugenzi wa chuo Ellerton Mwamasika akiwa chini ya Ulinzi wa Polisi Mara Baada ya kufungiwa kwa chuo cha Mbeya Polytechnic |
Akiingia kwenye Gari. |
Baraza
la Elimu ya Ufundi (NACTE) kupitia Mkuu
wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla imekifungia chuo cha kilimo cha Mbeya
Polytechnic cha jijini Mbeya ambacho kilisajiliwa na Baraza la Elimu ya Ufundi
(NACTE) kwa jina la Ilemi Polytechnic mwaka 2012.
Katika
taarifa iliyotolewa mbele ya uongozi wa chuo hicho, wanafunzi wa chuo hicho na
waandishi wa habari, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala amesema kuwa sababu za
kufungiwa kwa chuo hicho ni pamoja na kutotambuliwa kwa program za kilimo na
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutokana na kutokufuata mchakato wa wizara
hiyo ambao pamoja na mambo mengine walitakiwa kuijulisha wizara husika
kutambuliwa kwake na NACTE na kukamilisha matakwa ya Wizara ya Kilimo,Mifugo na
Uvuvi kwa taaluma hiyo.
Aidha
imebainika kuwa wanafunzi 270 kati ya 359 wa program ya kilimo walidahiliwa
kujiunga na chuo hicho pasipo kufuata taratibu na sifa stahiki za za kujiunga
na masomo hayo ambapo kati ya sifa hizo ni pamoja na ufaulu mzuri wa masomo ya
Kilimo, Fizikia, Baiolojia, Kemia, Hesabu na Jiografia.
Pamoja
na sababu hizo lakini pia imebainika kuwa chuo hicho cha Mbeya Polytechnic
hakikuwa na waalimu (wakufunzi) wa kutosha au kukidhi ufundishwaji wa moduli
zote kwa idadi ya wanafunzi walio dahiliwa, mazingira duni na hafifu ya kusomea
wanafunzi, kudahili wanafunzi kwa awamu nne kwa mwaka na hivyo kuwa kinyume na
msimu wa mvua kwa mikoa ya nyanda za juu kusini pamoja na akaunti za chuo
kumilikiwa na kuratibiwa na familia ya mkurugenzi wa chuo Ellerton Mwamasika na
hivyo kushindwa kuwalipa waalimu na hata kushindwa kuwapeleka wanafunzi katika
mafunzo ya vitendo.
Hata
hivyo mkurugenzi wa chuo hicho Ellerton Mwamasika amekiri kufanya makosa ya
kitaaluma katika uongozi wa chuo hicho na kisha kushikiliwa jeshi la polisi
mkoa wa Mbeya huku akiamriwa kurejesha gharama zote zilizotumiwa na wanafunzi
wa chuo hicho mara moja. Pia mkurugenzi wa chuo hicho Ellerton Mwamasika kwa
niaba ya wanahisa wa chuo hicho ametakiwa kuripoti kwa mkuu wa upelelezi wa
makosa ya jinai na kwa mkuu wa polisi wa mkoa ili apewe masharti ya ziada hadi
atakapomaliza kulipa madeni yote.
Baadhi
ya wanafunzi wameshukuru kusikilizwa na kuchukuliwa hatua ya kufungiwa kwa chuo
hicho kwani wamekuwa wakinyanyasika kwa kuongezewa ada kila mara huku wengine
wakidai kutopewa vyeti vyao baada ya kumaliza masomo katika chuo hicho na
wengine wakilia na madeni wanayodaiwa baada ya kukopa pesa kwaajili ya ada na
matumizi mengine ya chuoni.
Pamoja
na yote mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makala ametoa rai kwa wananchiwote kuwa
makini pale wanapotaka kujiunga na vyuo vya elimu ya kati na juu kuhakikisha
wamefanya utafiti wa kutosha kuhusu vyuo husika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni