HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA
FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), AKIWASILISHA
BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA,
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA
SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/17
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, Mwanafalsafa Baron Montesquieu aliwahi kuandika ifuatavyo kuhusu
mgawanyo wa madaraka “Pale ambapo madaraka ya Bunge na ya Serikali kuu
yanakuwa yamehodhiwa na mtu mmoja, au katika chombo hicho hicho cha
hukumu, hakutakuwa na uhuru, kwa sababu hofu itazuka, utawala huo huo au
bunge litatunga sheria kandamizi na kuzitekeleza kwa mfumo kandamizi.
Pia hakutakuwa na uhuru endapo madaraka ya Mahakama, Bunge na Serikali
hayatatenganishwa.
Pale
ambapo madaraka ya Serikali kuu yanapokuwa yamefungamanishwa na Bunge,
uhai wa Bunge na Uhuru wake unakuwa katika hatari kubwa ya kudhibitiwa
kiholela: kwa kuwa Jaji hawezi kuwa mtunga sheria. Pale ambapo Serikali
kuu imefungamanishwa na mahakama, basi Jaji anaweza kuwa na tabia ya
mabavu na ukandamizaji. Inakuwa mbaya zaidi, pale ambapo mtu huyo huyo
au chombo hicho hicho, iwe ni wateule wa Serikali au watu wengine
wanapotumia hayo madaraka ya kutunga sheria, kutekeleza maazimio ya umma
na kutoa hukumu za jinai au tofauti za watu”
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa mada iliyowasilishwa na Profesa P.J. Kabudi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam juu ya “Mafundisho ya Mgawanyo wa Madaraka
na jinsi yanavyotumiwa Tanzania” (Doctrine of Separation of Powers and
its Application in Tanzania: Success, Challenges and Prospects) ni
kwamba; hakuna mgawanyo dhahiri wa madaraka baina ya mihilimili mikuu ya
dola na kwamba bado Tanzania ina ‘hang-over’ ya ulevi wa siasa za chama
kimoja . Sehemu ya Mada hiyo inasomeka hivi: nanukuu; “Katiba ya
Tanzania ya mwaka 1977 bado inatumika mpaka leo pamoja na kuwa
marekebisho yalikuwa mfano wa Ustawishaji wa mfumo wa chama kimoja
nchini Tanzania. Katiba pia iliendelea kustawisha dhana ya Ukuu wa Chama
kushika hatamu. Ibara ya 3 na 10 zilibainisha kuwa CCM ndio chama pekee
cha Siasa Tanzania na kuwa shughuli zote za Serikali ilibidi zifuate
sera na miongozo ya chama. Hii ilimaanisha kuwa Bunge na Mahakama
vilitakiwa kufuata maelekezo ya chama katika kutenda majukumu yao. Zaidi
ya yote, kama ilivyokuwa kwa Katiba ya Mpito, ibara ya 63(4) ya Katiba
ililifanya Bunge kuwa kamati maalumu ya Mkutano Mkuu wa Chama wa Taifa.
Ilikuwa ni jambo la kawaida pale ambapo bajeti ya wizara imekwama basi
wabunge waliahirisha mkutano na Bunge lilikaa kama kamati ya Chama ili
kujadili hilo suala. Mara tu uamuzi unapofikiwa basi Bunge linarejea na
bajeti inapitishwa bila kuwa na upinzani mkubwa”
Katiba
ya mwaka 1977 imerekebishwa mara kadhaa. Marekebisho makubwa zaidi
yalikuwa ni yale ya tano, ambayo yaliingiza Haki za Binadamu katika
Katiba, na marekebisho ya nane yaliyofanyika mwaka 1992 yaliyorejesha
tena Mfumo wa Vyama Vingi Tanzania.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia maudhui ya nukuu ya mwanafasafa wa kale wa
Sayansi ya Siasa Montesquieu, mada ya Profesa Paramagamba John Kabudi,
na tabia isiyokubalika ya Serikali kuendelea kushawishi Mahakama na
kulidhibiti Bunge kwa hila mbalimbali ni kwamba, Tanzania sasa iko
katika hatari kubwa ya kuingia katika mfumo wa Dola la Kidikteta na
tayari dalili zote za utawala wa namna hiyo zimeanza kuonekana.
Mheshimiwa
Spika, vitendo vya hivi karibuni vya Serikali hii kukanyaga uhuru wa
vyombo vya habari kwa kufuta kabisa usajili wa baadhi ya vyombo vya
habari, kupiga marufuku urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya
mijadala ya Bunge kupitia televisheni ya Taifa, kuingiza polisi ndani ya
ukumbi wa Bunge na kuwapiga na kuwadhalilishwa wabunge; kuzuia mikutano
ya vyama vya siasa ni sehemu tu ya tabia za utawala wa kidikteta.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakemea kwa nguvu zote
ukandamizaji wa demokrasia na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na
Serikali ya Tanzania dhidi ya watu wake. Aidha, tunataka Jumuiya ya
Kimataifa ijue na dunia ijue kwamba sasa Tanzania hakuna utawala wa
kidemokrasia tena – kinachofanyika ni utekelezaji wa amri za Rais –
yaani Presidential decrees.
Mheshimiwa
Spika, kabla sijatoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya
Serikali ya 2016/17, napenda kuweka rekodi sawa kuhusu upotoshaji
unaofanywa na Wabunge wa CCM kwamba Wabunge wa Upinzani wanaisaini
mahudhurio bungeni na kuchukua posho bila kufanya kazi. Napenda mkumbuke
kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikisisitiza kufutwa kwa
posho za vikao kwa maana ya “Sitting allowance”, lakini serikali
imekuwa ikipata kigugumizi, hivyo basi Kambi Rasmi inasema kama kweli
Serikali ya Rais John Pombe Magufuli inania thabiti ya kubana matumizi
ya Serikali basi inoneshe uthabiti huo kwa kuifuta posho ya vikao na
fedha hizo zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo hususani kuwapatia
Watanzania maji safi na salama. Hata hivyo, tunashauri, wale wanaokaa
bungeni bila kuchangia hata kwa maandishi na kuchukua posho, wafuatiliwe
na wakatwe mishahara yao, kwa kuwa hawajafanya kazi na hansard itumike
kuwabaini.
Mheshimiwa
Spika, katika jitihada kuongeza mapato, Serikali katika bajeti hii
imekusudia kukata kodi ya asilimia 5 kwenye kiinua mgongo cha wabunge.
Kambi Rasmi ya Upinzani haina tatizo na pendekezo hilo, ila inaitaka
Serikali kwenda mbali zaidi kwa kuifanyia marekebisho sheria ya mafao ya
viongozi wa kisiasa ambayo kwa sasa imewapa misamaha ya kodi ya viinua
mgongo viongozi wakuu wa kisiasa kama Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu,
Mawaziri, Spika, Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ili
sasa na wao walipe kodi hiyo. Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaikumbusha Serikali kwamba kiinua mgongo cha wabunge hutolewa
mwisho wa uhai wa bunge husika, hivyo haioni mantiki ya kutoa pendekezo
hili sasa kwa kuwa halina impact kwa bajeti ya 2016/17.
2. HALI YA UCHUMI
Mheshimiwa
Spika, tunaposema hali ya uchumi tunaangalia uchumi kwa ukubwa wake
(Macro economy) katika nchi, mataifa yanayotuzunguka na kwa dunia nzima,
na ni kwa vipi sera zetu za uchumi zinavyoathirika na uchumi wa dunia,
na ni kwa jinsi gani watunga sera wanatakiwa kuwa na mikakati
itakayoweza kukabiliana na sera za wale tunaotengamana nao kibiashara.
Mheshimiwa
Spika, Na katika hili ni lazima tuangalie ni jinsi gani uchumi mdogo
(micro-economy) ambao ndio nguzo kuu ya nchi kwa maana unaowafanya
wananchi waweze kuishi, au sera za uchumi zinazoendesha biashara ndogo
ndogo kati ya kampuni na kampuni, na zinaangalia jinsi biashara
zinavyoweza kufanikiwa kwa kiwango cha juu na aidha, namna gani maamuzi
ya biashara yanatakiwa kufanywa ili biashara ziweze kufanikiwa, kwa
maana nyingine ni kushughulika na “supply and demand”, jinsi ya
kufikisha uchumi kwenye mifuko ya watu mmoja mmoja.
Mheshimiwa
Spika, kukua au kutokukua kwa uchumi kutaonekana na jinsi pato la taifa
litakavyokua ambalo ni matokeo ya shughuli za uzalishaji na utoaji wa
huduma katika mzunguko mzima wa uchumi. Katika makadirio yaliyokuwa
yametolewa na serikali katika mpango wa maendeleo awamu ya kwanza kwenye
ukuaji wa uchumi ilitarajiwa kuwa ukuaji wa pato la taifa lifikie
asilimia 8. Hii iliwekwa kutokana na ukweli kuwa kwa mwaka 2011 GDP
ilikuwa 7.9%, 2013 GDP ikawa 7.3% na miaka miwili mfululizo GDP ikawa
7.0% na matarajio kwa mwaka 2016 ni 7.2%.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi hicho ukuaji wa baadhi ya sekta za uzalishaji
pamoja na shughuli za utoaji wa huduma ulikuwa kama ifuatavyo;
Mawasiliano (14.9%), Huduma za fedha na Bima (10.4%), Ujenzi (10.3%),
Kilimo - kwa maana ya mazao, ufugaji,misitu na uvuvi (3.1%) kwa
kulinganisha na 3.4% mwaka 2014. Sekta hii licha ukuaji wake kuwa mdogo
kwa kulinganisha na mwaka wa nyuma lakini mchango wake katika Pato la
Taifa uliongezeka na kuwa 31.4% kulinganisha na 28.9% kwa mwaka 2014.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa takwimu za Serikali, inaonesha kuwa kiwango cha
riba za amana za muda maalum kiliongezeka kutoka wastani wa asilimia
9.02 Januari, 2015 hadi asilimia 9.08 Januari, 2016, kiwango cha riba za
amana kwa mwaka kiliongezeka hadi 11.01% kutoka 10.66% 2015. Riba za
mikopo kiliongezeka kutoka 15.75% Jan. 2015 hadi asilimia 16.28
Jan.2016, wastani wa riba za amana za mwaka na riba za mikopo za mwaka
iliongezeka kutoka wastani wa 3.14% Jan.2015 na kufikia 3.33% Jan.2016
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema riba hizi zingeweza kuongezeka kama
Serikali isingekuwa inafanya biashara kubwa na mabenki na hivyo
kupelekea mabenki kushindwa kuhamasisha wananchi kufanyabiashara nayo.
2.1 USIMAMIZI WA TAASISI NDOGO-NDOGO ZA FEDHA
Mheshimiwa
Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inapenda kusisitiza tena kwa Serikali
kuleta muswada wa sheria ambao utaanzisha mamlaka ambayo itatoa kisheria
muundo wa kudhibiti na kusimamia taasisi ndogondogo za fedha nchini
ambazo kwa sasa zimekuwa zikisimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na
taasisi nyingine za kifedha kama mabenki. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaona haja ya kuwa na mamlaka huru iliyo chini ya Benki Kuu ya Tanzania
ya kusimamia taasisi ndogondogo kama ambavyo Benki Kuu ya Tanzania
imeruhusu uanzishwaji wa mamlaka za kusimamia mifuko ya hifadhi za
jamii, bima na kadhalika.
Mheshimiwa
Spika, kuundwa kwa chombo chenye mamlaka ya kusimamia taasisi
ndogondogo za fedha ni lazima kwa kuwa kwa sasa hakuna mrandamo wa
viashiria kwa mabenki na taasisi ndogondogo za fedha. Kutokana na
utofauti wa muundo wa mabenki na taasisi ndogondogo za fedha, inakua ni
vigumu kudhibiti riba na utoaji wa vigezo vya kifedha katika kuhudumia
wananchi na kutoa mikopo yenye unafuu.
Mheshimiwa
Spika, hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani ni kuwepo na chombo chenye
mamlaka tofauti na Benki kuu ya Tanzania itakayosimamia na kuratibu
taasisi ndogo ndogo za fedha na kuziwezesha katika kutoa mikopo kwa
wananchi hasa walio katika sekta isiyo rasmi. Hivi sasa kumekuwapo na
taasisi ndogondogo za kifedha ambazo zinawapa fursa wananchi kujiunga
katika vikundi vidogo vidogo na kuwapa elimu ya ujasiriamali kisha
kuwasaidia katika suala la mikopo ambayo utakaoweza kuwapa fursa
watanzania waliopo katika sekta isiyo rasmi kama wamachinga, mama lishe,
mafundi uashi na wajenzi, mafundi magari na seremala ambao chombo hicho
kingeweza kusimamia ukusanyaji wa fedha kutoka katika makundi haya na
kuweza kuwekeza kwa ajili ya kusaidia kutoa mitaji pale inapohitajika.
Mheshimiwa
Spika, hili ni suala zuri ambalo linalenga kuboresha maisha ya wananchi
wa vijijini na maeneo mbalimbali ya mijini. Pia, zipo Saccoss (vyama
vya kuweka na kukopa) na benki jamii (vicoba) ambazo zimekuwa na
wanachama wengi wanaoendelea kujiunga ili kujikwamua kiuchumi. Lakini
kumekuwa na mapungufu kwa kuwa taasisi ndodondogo za fedha zimeendelea
kutumia masharti sawa na zile za mabenki ambazo zimekuwa ni mzigo kwa
mlengwa ambaye ndiye analipa riba kubwa kutokana na masharti mazito
yenye kulingana na vigezo vya kutoa mikopo kwa mabenki chini ya Benki
kuu ya Tanzania. Kwa mfano, taasisi za fedha chini ya Benki Kuu bado
zimeendelea kumtaka mtu awe na dhamana ya mali isiyohamishika na zile
wanazojidhamini kwa vikundi. Je, itawezekanaje kwa Mwananchi mwenye hali
duni kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika?
Mheshimiwa
Spika, kuwepo kwa chombo chenye mamlaka pia itasaidia kuwa na Credit
Reference Bureau itakayokuwa na taarifa za wakopaji kutoka taasisi
ndogondogo za fedha tofauti na itakayosimamia wadaiwa wa mabenki na
taarifa hizi zitasaidia udhibiti wa wateja wa taasisi hizi kuchukua
zaidi ya mkopo mmoja kwenye taasisi tofauti tofauti ambapo hali hii
husababishwa na uchelewashaji wa mikopo unaotolewa na taasisi hizi
pamoja na uhafifu wa mikopo katika kumsaidia mlengwa.
3. MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO 2016/17
3.1. Ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017
Mheshimiwa
Spika, moja ya sifa kubwa ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
uliomaliza muda wake (2011/12 – 2015/16) ni kuweka msingi wa kibajeti
ulioitaka Serikali kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani kwa ajili
ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Mpango ulisema hivi: nanukuu,
“kwa kuelewa kuwa wakati wote kutakuwa na miradi ya uwekezaji nje ya
mpango, serikali, kuanzia sasa, itakuwa inatenga asilimia 35 ya
makadirio ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya
maendeleo kila mwaka” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na uhalisia kwamba Mpango huo haukutungiwa sheria ya
utekelezaji; Serikali ilijificha katika kichaka cha udhaifu huo; na
matokeo yake kwa miaka yote mitano ya utekelezaji wa Mpango huo,
Serikali haikuwahi hata mara moja kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya
ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuna wakati
mwingine haikutenga hata senti moja. Kwa mfano katika mwaka wa fedha
2012/13 Serikali haikutenga fedha yoyote kutoka katika mapato yake ya
ndani kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na Serikali kugoma kutoa asilimia 35 ya mapato yake ya
ndani kutekeleza miradi ya maendeleo, miradi mingi ya maendeleo
haikukamilika hadi mwisho wa muda wa utekelezaji wa Mpango.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na aibu ambayo Serikali iliipata kwa miaka yote mitano
ya utekelezaji wa Mpango huo kwa kushindwa kutekeleza utaratibu
iliyojiwekea yenyewe wa kutenga asilimia 35 ya Mapato yake ya ndani
kugharamia mpango wa Maendeleo; safari hii Serikali imefuta utaratibu
huo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17 –
2020/21).
Mheshimiwa
Spika, tafsiri rahisi ya uamuzi wa Serikali hii ya CCM inayojinasibu
kwa kauli ya “hapa kazi tu” kufuta msingi wa kibajeti wa kugharamia
mpango wa maendeleo kwa kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani ni
hofu ya kushindwa kutekeleza commitment hiyo kama ambavyo ilishindwa
kufanya hivyo katika Mpango uliomaliza muda wake lakini pia ni kukwepa
kuwajibika au kuwajibishwa na Bunge kwa hofu hiyo hiyo ya kushindwa
kutekeleza. Kwa hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inadhani ni bora
Serikali hii ikakubali uhalisia kwamba imetawaliwa na hofu tu na sio
kazi tu kwa kuwa inakimbia kivuli chake yenyewe.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kwamba: “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa
madaraka yake, Bunge laweza; kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa
muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya
Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;
hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuleta
Muswada wa Sheria ya Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo
unaopendekezwa kabla ya kupitishwa na Bunge. Aidha; Kambi Rasmi ya
Upinzani inapendekeza kwamba Muswada huo uitake Serikali kutenga
asilimia 40 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, suala la kutuga sheria ya kutekeleza Mpango huu sio ushauri wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni – ni takwa la kikatiba. Ikiwa Serikali
hii itapuuzia jambo hili basi ijulikane na iingie kwenye rekodi kwamba
Serikali imevunja Katiba ya Nchi.
Mheshimiwa
Spika imebidi sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ichukue jukumu la
kusimamia misingi ya Katiba ili Serikali hii isiendelee na tabia yake ya
kuwa na ndimi mbili katika jambo moja. Nasema hivi kwa sababu; Serikali
hii imekuwa na historia ya kulidanganya bunge, na kwa kuwa wanajivunia
wingi wa wabunge CCM basi mambo yamekuwa yakipitishwa kiholela bila
kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria za Nchi na hata Kanuni za Bunge.
Kwa mfano; Serikali imesema katika Mpango wake wa Maendelo wa 2016/17
kwamba imetenga shilingi trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti
yote kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; lakini ukisoma kitabu
cha Matumizi ya Fedha za Maendeleo (Public Expenditure Estimates
Development Votes) VOLUME IV, fedha zilizotengwa ni shilingi trilioni
10.511.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inapokuwa na tarakimu tofauti katika suala nyeti kama
hili la Bajeti ya Serikali, tunapata mashaka makubwa sana na weledi wa
watendaji wa Serikali akiwemo kiongozi wao mkuu. Katika hali kama hiyo,
ni lazima kuwa na sheria itakayotoa mwongozo kwa Serikali juu ya
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ambao unatumia fedha za umma.
3.2. Mpango wa Taifa wa Maendeleo na Agenda 2030 ya Dunia ya Maendeleo Endelevu
Mheshimiwa
Spika, tarehe 25 Septemba, 2015 Dunia iliingia mkataba wa kutekeleza
malengo 17 ya agenda 2030 ya kuibadilisha Dunia na kuwa mahali salama
zaidi pa kuishi kwa kuweka malengo ya kuwa na maendeleo endelevu.
Malengo hayo ni kama ifutavyo:
Lengo Na. 1. Kuondoa umasikini wa aina zote
Lengo Na. 2. Kuwa na kilimo endelevu, Kuondoa njaa na kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora kwa watanzania wote.
Lengo Na. 3. Kuhakikisha kuwa jamii ya rika zote inakuwa na afya bora.
Lengo Na. 4. Kuhakikisha fursa ya elimu bora na iliyo shirikishi kwa watanzania wote.
Lengo Na. 5. Kutoa usawa kwa jinsia zote na kuwawezesha akina mama na wasichana wote.
Lengo Na. 6. Kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa watanzania wote.
Lengo Na.7. Kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati endelevu na ya kisasa kwa wote.
Lengo Na. 8. Kukuza ajira endelevu na zenye staha na ukuaji wa uchumi shirikishi.
Lengo Na. 9. Kujenga miundombinu bora na shirikishi ili viwanda viwe endelevu kwa kupokea mabadiliko yoyote.
Lengo Na. 10. Kupunguza tofauti za ndani na baina ya mataifa kwa walionacho na wasio nacho.
Lengo Na. 11. Kufanya miji yetu na makazi shirikishi, endelevu na salama.
Lengo Na. 12. Kuhakikisha uzalishaji endelevu utakaoendana na matumizi.
Lengo Na. 13. Kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Lengo Na.14. Kutunza na matumizi endelevu kwa maendeleo ya rasilimali za baharini.
Lengo
Na.15. Kulinda na kuwa na matumizi endelevu ya ‘terrestrial ecosystem’,
kutunza misitu na kupambana na ukame na kurudisha uhalisia wa ardhi.
Lengo Na.16. Kuwa na taasisi imara ili kuwa na haki na amani, Lengo Na.
17. Kuimarisha ushiriki wa pamoja katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Mheshimiwa
Spika, Kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya dunia, na kwa kuwa Tanzania
haiwezi kusimama peke yake na kufanikiwa katika kufikia malengo yake ya
maendeleo kama haishirikiani na mataifa mengine, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imetekeleza kwa kiwango
gani agenda ya Dunia ya 2030 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu?
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa malengo yote 17 ya maendeleo endelevu ya dunia ni
muhimu kwa nchi yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa
mchanganuo wa kina wa jinsi kila lengo lilivyotekelezwa na kiwango cha
utekelezaji (asilimia) kwa kila lengo. Aidha, tunaitaka Serikali kutoa
majibu ya ziada na ya kipekee ya namna ilivyotekeleza lengo la 16 la
Kuwa na Taasisi imara ili kuwa na Haki na Amani.
Mheshimiwa
Spika, Tumeweka msisitizo katika lengo hili kwa kuwa haki inaleta amani
na amani ni tunda la Maendeleo. Kwa hali ilivyo sasa hapa nchini, kuna
dalili zote kwamba taasisi zetu haziko imara jambo ambalo linafifisha
jitihda za kuwa na haki na amani katika nchi yetu. Kama taasisi zetu
hasa za kutoa haki zingekuwa imara ni dhahiri Zanzibar kusingekuwa na
hitajio la uchaguzi wa marudio. Jambo hilo linatia mashaka kama Tanzania
tutaweza kukidhi malengo endelevu ya maendeleo kama Agenda 2030 ya
Dunia inavyohitaji.
4. UCHUMI WA VIWANDA
Mheshimiwa
Spika, kwa nchi yoyote Duniani ambayo uchumi wake unaendelea kukua ni
dhahiri kuwa sekta ya viwanda inakua kwa kasi inayoridhisha na sekta
hiyo ina uhusiano wa moja kwa moja na sekta zinazotoa malighafi kwa
sekta ya viwanda.
Mheshimiwa
Spika, Kuwa na uchumi wa kipato cha kati kupitia ujenzi wa uchumi wa
viwanda ni lazima kama nchi iwe na malengo ambayo yako wazi kuhusu aina
ya sekta zitakazowekezwa ili iwe chachu ya kututoa hapa tulipokwama kwa
kipindi chote. Ili malengo yawe wazi ni lazima kuangalia mazingira yetu
ya ndani na mazingira ya nje ambayo kwa njia moja au nyingine yana
uhusiano wa moja kwa moja na uzalishaji wa viwandani.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaposema malengo yaende sambamba na
mkakati mzuri wa utekelezaji, ni kwamba utakapo chagua viwanda viwe
katika sekta kama: bidhaa za kilimo, mifugo, uvuvi, madini, kemikali,
misitu na/au huduma; nk. Ni lazima ujenzi wa viwanda kufuatana na sekta
tajwa hapo juu uhitaji upembuzi yakinifu wa hali ya juu hadi kufikia
maamuzi ya wapi viwanda hivyo vijengwe kwa kulingana na kiwango cha
rasilimali zilizopo na kiwanda kitakachojengwa ni kwa muda gani kitaweza
kurudisha mtaji na ajira kiasi gani zitazalishwa. Na pia kuangalia nchi
za jirani zina kiwanda kama hicho na uwezo wake wa kuzalisha bidhaa na
ubora wa bidhaa zake ukoje (uhimili wa ushindani wa bidhaa). Je, aina ya
teknolojia itakayotumika kuzalisha bidhaa itaweza kutumiwa na wananchi
wetu (rasilimali watu ya hapa hapa ndani ya nchi) au kitakuwa tegemezi
kwa wataalamu wa nje?.
Mheshimiwa
Spika, Mojawapo ya malengo ni kuhakikisha yanakidhi mahitaji ya ndani
kwa bidhaa zinazozalishwa, kuwa soko la malighafi ya bidhaa za kilimo,
mifugo, uvuvi, misitu na madini kwa kuwa nguzo kuu ya mnyororo wa
thamani, kwa kuubadili mfumo wa uchumi ambao ulikuwa tegemezi kwa sekta
za kilimo, madini na huduma na kuwa uchumi tegemezi kwa sekta ya
viwanda. Pia kuwezesha bidhaa zinazozalishwa kuwa shindani katika soko
la Afrika ya Mashariki na soko la nchi za Kusini mwa Afrika1.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasema ili kuwa kweli nchi
yenye uchumi wa viwanda na hivyo kupelekea kuwa nchi ya uchumi wa kipato
cha kati, tuna hitaji mkakati mzuri na utekelezaji wake wa kutufikisha
huko na sio matamanio na mahubiri tu, kama yanavyotolewa na viongozi
wetu.Viwanda siyo tu vinakuza uchumi kwa kuongezea bidhaa thamani bali
pia vinatengeneza ajira nyingi kwa haraka na kwa sekta nyingine.
Mheshimiwa
Spika, Kwa kuwa mwaka huu wa bajeti 2016/17 ni mwaka wa kwanza kwa
awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa 2025, japokuwa ni mwendelezo wa
awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo, hivyo basi ni muhimu kuangalia
uwekezaji ambao tayari umefanyika katika sekta nzima ya uzalishaji.
Mheshimiwa
Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya China wameanzisha kituo
cha Biashara kwa ajili ya bidhaa toka China (Kurasini Logistic Center)
ambapo hadi sasa Tanzania imekwishatoa shilingi 65,279,464,100/-ambazo
ni sawa na Asilimia 72% ya fedha zilizotakiwa kutolewa na Serikali kwa
ajili ya fidia kwa wakazi wa kurasini.
Mheshimiwa
Spika, dhana nzima ya uwekezaji wa pamoja katika kuanzisha Kituo hiki,
kwamba bidhaa mbalimbali toka China zitakuwa zinaletwa hapo na
wafanyabiashara wa nchi za Afrika ya mashariki na zile za Kusini mwa
Afrika badala ya kwenda China kufuata bidhaa, basi watakuwa wanapata
bidhaa zote Dar es Salaam. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kwamba
uwekezaji uliokwishafanywa na unaoendelea kufanywa katika kuanzisha
kituo hicho ni dhahiri kwamba unapingana na dhana nzima ya awamu ya pili
ya Mpango wa maendeleo wa 2025 kuwa ni kuifanya nchi kuwa na uchumi wa
viwanda.
4.1. SEKTA YA NYUMBA NA UKUAJI WA UCHUMI
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kuwa mwaka 2011, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni Mhe. Freeman Mbowe (Mb) akiwasilisha Bungeni maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alipendekeza
kuwa pamoja na mambo mengine kuna ulazima kama taifa kuwa na mamlaka
udhibiti wa sekta ya nyumba (Real Estate Regulatory Authority)
itakayokuwa na jukumu la kusimamia sekta ya nyumba nchini hasa majengo
makubwa ili kuwa chanzo cha mapato ya serikali.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na pendekezo hilo kutolewa wakati huo serikali wakati wa
bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imependekeza
mwaka ujao wa fedha 2016/2017 imeahidi kuleta Bungeni muswada wa sheria
ambayo itasimamia sekta ya nyumba nchini. Ni msimamo wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni kuwa pendekezo hili limechelewa sana. Kama serikali
ingelitekeleza jambo hili mapema, serikali ingelipata chanzo cha mapato.
Mheshimiwa
Spika, majirani zetu wa Kenya ndani ya jumuiya ya Afrika ya Mashariki,
sekta ya nyumba imechangia pato la taifa kwa 10.6% sekta hiyo ikiwa ya
nne katika kuchangia katika uchumi wa nchi hiyo. Aidha athari za
kuanguka kwa bei ya mafuta duniani haijaathiri uchumi wa Dubai kwa
sababu ya kuwa na mafanikio makubwa katika sekta ya nyumba.
Mheshimiwa
Spika, tamwimu zinaonesha kuwa Tanzania kuna uhitaji wa nyumba 200,000
kila mwaka na uhaba wa nyumba milioni 3. Hii ni kutokana na ongezeko la
kasi la idadi ya watu nchini pamoja na uhitaji wa nyumba zenye hadhi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa serikali haijawa na mkakati
madhubuti wa kuhakikisha tunatumia fursa ya sekta ya makazi kukuza
uchumi wa nchi yetu kama ambavyo mataifa mengine yamepiga hatua kubwa
kwa kutumia fursa hiyo.
4.2 KODI YA MAJENGO (PROPERTY TAX)
Mheshimiwa
Spika, kwa miaka mingi kodi ya majengo ilikuwa ikikusanywa na
halmashauri, lakini kwa sasa serikali imeamua kodi hiyo ikusanywe na
Mamlaka ya Mapato Tanzania na kupelekwa Hazina. Agizo hili litaathiri
kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri zetu nchini kwa kuwa kodi ya
majengo ilikuwa chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri hasa za Miji,
Manispaa na Majiji.
Mheshimiwa
Spika, ieleweke kuwa kama fedha zitakusanywa na Hazina na kama
utaratibu wa kutoa fedha hizo kwenda Halmashauri utaendelea kama ilivyo
sasa ambapo fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu zinachelewa kupelekwa
kwenye Halmashauri basi tusitegemee kuwa fedha za kodi ya majengo
zitanuifaisha tena Halmashauri zetu.
Dhana
hii ni kutokana na ukweli halisi ambao upo kwenye kodi ya ardhi ambayo
ilikuwa inakusanywa na Halmashauri na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi
ilionyesha wazi kuwa ikishafika wizarani ilikuwa vigumu sana kurejeshwa
kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa
Spika, Hii ni kutokana na sababu kuwa serikali mara nyingi imekuwa
ikipeleka fedha Halmashuri katika robo ya mwisho ya mwaka wa fedha. Ni
rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa serikali itafikiria upya uamuzi huu
ambao utapunguza sana mapato ya Halmashauri zetu na kuzifanya kushindwa
kutoa huduma kwa wananchi wake.
4.3 SEKTA YA UTALII
Mheshimiwa
Spika, sekta ya utalii ni sekta ambayo inachangia fedha za kigeni
katika sekta nzima ya uchumi (foreign exchange earner), kwa kuwa na
watalii milioni moja wanaochangia asilimia 17.7 ya pato la Taifa (GDP).
Kwa mujibu wa takwimu za nchi nzuri duniani2 ni kwamba; Tanzania ni
namba 8 kati ya mataifa 20 yenye vivutio vizuri na vingi Duniani kwa
ajili ya watalii. Lakini kuwa na vivutio vingi sio sababu ya kuwa na
watalii wengi, ila sababu kubwa ni jinsi gani unajitangaza na unawavutia
vipi watalii?
Takwimu
zinaonesha kuwa Ufaransa ndiyo nchi inayoongoza kuwa na watalii milioni
83.77 kwa mwaka wakati katika zile nchi 20 haimo. Afrika ya Kusini
inapokea watalii 9,616,9643 kwa mwaka, lakini katika orodha inachukua
namba 1, Kenya ambayo ilikuwa imefikisha watalii milioni 1.7 kabla ya
tishio la ugaidi, sasa inatarajia watalii milioni 1.6, Uganda inapokea
watalii 1,266,000 kwa mwaka, Zimbabwe inapokea watalii 1,905,000 na
Msumbiji 1,661,0004
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kama tutaweza kuongeza idadi ya
watalii hata kufikia milioni 5 kwa mwaka ni dhahiri uchumi wa Tanzania
unaweza kuendeshwa na sekta ya utalii.
Mheshimiwa
Spika, Ili Tanzania iweze kupata watalii milioni 5 kwa mwaka, Kambi
Rasmi ya Upinzani inashauri kwamba Serikali iimarishe kwanza usafiri wa
anga. Hali ilivyo sasa, watalii wanapata tabu sana kufika Tanzania
kutokana na gharama kubwa inayosababishwa na kutokuwepo usafiri wa
uhakika wa ndege. Tunashauri kwamba Serikali iweke mkakati mahususi wa
kuwashawishi marafiki zetu wa China ili shirika lao la ndege lianzishe
safari za kuja Tanzania, na vile vile mashirika ya ndege toka Marekani
kuwa na safari za Tanzania kila wiki. Pili, tozo katika viwanja vyetu
vya ndege zipunguzwe ili kuvutia watalii. Tatu huduma zinazotolewa kwa
watalii huko mbugani ziboreshwe na kuwa na kiwango cha kimataifa ili
kuwavutia watalii zaidi.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na misimamo ya Serikali isiyokuwa ya kibiashara ni
kwamba utalii kuwa na faida sana inategemea na idadi ya watalii
wanaoingia, hivyo kama Serikali itakubali kuwa kipindi kisichokuwa cha
msimu wa utalii ni vyema bei zikashuka ili idadi ya watalii na siku za
kukaa nchini iongezeke. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuja kwa watalii
kuna wanufaisha watu wengi sana mbali ya Serikali kupata mgawo wake, ni
muda mwafaka sasa Serikali kuwa-“flexible” ili kuwa kibiashara zaidi.
Mheshimiwa
Spika, Tunaitaka Serikali kutumia mfano wa jirani zetu Kenya, ambapo
Rais Uhuru Kenyatta amefuta tozo za kutua kwa ndege zote za kukodi
zitakazokuwa zinaleta watalii nchini Kenya5.
5. VITUO VYA KUUZA UTALII WA TANZANIA NJE
Mheshimiwa
Spika, Bodi ya Utalii imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa muda mfupi
wakati wa maonyesho mbalimbali ya utalii yanayofanyika nje ya nchi. Ili
kuwe na ujio endelevu wa watalii nchini, Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza kwamba Serikali iweke vituo vya utangazaji wa utalii wetu
katika balozi zetu katika nchi za Marekani, Ujerumani, Ufaransa,
Uingereza, Italia,Uchina, Japani, Canada na nchi za Scandinavia na kuwe
na watumishi maalumu watakaoajiriwa katika vituo hivyo kwa kazi maalum
ya kuhakikisha kuwa wanatangaza vivutio vyetu na kuongeza idadi ya
watalii wanaokuja hapa nchini. Mkakati huo ukifanikiwa ni dhahiri kwa
mwaka mmoja tunaweza kupokea watalii zaidi ya milioni tano.
Mheshimiwa
Spika, fursa hii si kila mtu anaweza kuiona, hivyo ni muda muafaka
kuwashawishi wachina wawekeze katika hoteli za kitalii, badala ya
wawekezaji hao kushindana na watanzania katika maduka ya vifaa vya
ujenzi pekee. Kwa njia hii tutaweza kuvuta soko la watalii wengi toka
China.
6.0 SERIKALI YA HAPA KAZI TU, IMELETA BAJETI HEWA BUNGENI
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni
wajibu wa Bunge kupanga na kuidhinisha mapato na matumizi ya serikali
kila mwaka wa fedha .Hii ni kwa mujibu wa ibara ya 137(1)’Rais atatoa
maagizo kwa watu wanaohusika kwamba watengeneze na kuwasilisha kwenye
Bunge katika kila mwaka wa fedha wa Serikali, makadirio ya ‘Mapato na
Matumizi’ ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha
mwaka wa fedha unaofuata’
Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2016/17 serikali imewasilisha bajeti hewa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, ninasema kuwa serikali hii imeleta bajeti hewa hapa Bungeni na nitathibitisha maoni yangu haya kama ifuatavyo;
1.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato ya serikali katika mwaka huu wa fedha
volume 1 ‘Financial Statements and Revenue estimates’ for the year 1st
July ,2016 to 30th June 2017 kilicholetwa hapa Bungeni kinaonyesha kuwa
mapato yote ya serikali yaani mapato ya kodi , yasiyokuwa ya kodi
,mikopo na misaada ya kibajeti itakuwa jumla ya shilingi Trilioni
22.063.
Mheshimiwa Spika, upatikananji wa mapato hayo ni kama ifuatavyo;
i. Mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali ni shilingi Trilioni 17.797
ii. Mapato yasiyokuwa ya kodi ni shilingi Bilioni 665.664
iii. Mikopo na misaada ya kibajeti ni shilingi Trilioni 3.600
Mheshimiwa
Spika, ni muhimu Waheshimiwa Wabunge wakatambua kwamba Serikali hii
haijaonyesha chanzo kingine kipya cha mapato ambacho hakijathibitishwa
na au kupitishwa na Bunge hili kwa mujibu wa katiba na ijulikane pia
kuwa Bunge halipitishi kitabu cha hotuba ya waziri bali hupitisha
mafungu yaliyopo kwenye vitabu vya bajeti ya serikali.
2.
Kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya kawaida ,volume II Estimates of
Public Expenditure Consolidated Fund Services for the year 1st July
,2016 to 30th June, 2017 na kitabu cha Maendeleo, Volume IV Public
Expenditure Estimates Development Votes (part A) kama vilivyowasilishwa
Bungeni , tayari bunge limeshaidhinisha matumizi ya jumla ya shilingi
Trilioni 23.847
Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:
i. Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) shilingi 13,336,042,030,510
ii. Fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo (Volume IV) shilingi 10,511,945,288,575
3.
Ukichukua kitabu cha Mapato ya Serikali (Revenue Book Volume I) utaona
kuwa jumla ya mapato yote ya serikali ni shilingi Trilioni 22.063 , ila
serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi Trilioni 23.847 ambacho ni
kiasi tofauti na Mapato ambayo serikali imepanga kukusanya na tofauti
yake ni kuwa kuna nakisi ya shilingi Trilioni 1.783 jambo ambalo
linaifanya bajeti hii kukosa uhalali kwani nakisi hii ni kubwa sana.
4.
Kwa mujibu wa maelezo ya waziri wa fedha ‘Mapendekezo ya kiwango na
ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kwenye mkutano wa wabunge
wote katika ukumbi wa JNICC’ mnamo tarehe 06 Aprili, 2016 pamoja na
maelezo ya hotuba yake aliyoyatoa hapa Bungeni uk. 91 ameendelea
kulidanganya Bunge na Dunia kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali ina
bajeti ya kiasi cha shilingi Trilioni 29.539
5.
Hotuba ya waziri wa fedha katika ukurasa wa 92 ‘Mfumo wa Bajeti wa
Mwaka 2016/17’ inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi trilioni 7.475 ni
mikopo ya ndani yenye masharti ya kibiashara. Fedha hizi kwenye kitabu
cha mapato hazipo na pia hazionekani zitakopwa kutoka Benki gani kama
ambavyo mikopo ya nje yote imeonyeshwa kwenye kitabu cha mapato na hata
kwenye kitabu cha miradi ya maendeleo hazionekani kwenye kutekeleza
mradi wowote ule na hivyo ni sahihi kusema kuwa ni fedha hewa , maana
hazina hata kasma yake na Bunge hili tunapitisha kasma .
6.
Hotuba ya waziri wa fedha uk.58 anasema kuwa moja ya chanzo chake cha
mapato ni pamoja na kurekebisha sheria ya Kodi ya Mapato SURA 332
(i)’kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo
kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.’
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu ya kina kuhusu mambo yafuatayo;
i.
Bunge linapitisha takwimu zipi hasa? Ni kitabu cha hotuba ya waziri au
ni vitabu vya mapato na matumizi pamoja na kile cha Miradi ya maendeleo?
ii.
Fedha ambazo waziri kwenye hotuba yake anasema kuwa ni mikopo ya ndani
ya masharti ya kibiashara, zinakopwa ili kugharimia miradi ipi?
Kwani
tayari kitabu cha miradi ya maendeleo VOLUME IV kimeshataja miradi yote
na kiasi cha fedha ambazo kila mradi utatumia.Hii miradi inayosemwa
kuwa fedha itakopwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni miradi ipi hiyo?
Mbona haijapitishwa na bunge au ni miradi hewa?
iii.
Waziri wa fedha anaposema kuwa fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi
Trilioni 17.719 na hapo hapo anasema kuwa tunakwenda kulipa deni la
taifa kiasi cha shilingi trillion 8, mbona hizi fedha hazipo kwenye
kitabu ambacho kinapitishwa na Bunge? Kitabu cha matumizi ya kawaida
VOLUME IV?
iv.
Kwa kuwa CAG anakagua kasma zilizopo kwenye vitabu yaani VOLUME IV na
VOLUME II, katika bajeti hii atakagua kasma ipi?maana fedha za kulipia
deni la taifa hazipo kwenye kitabu cha VOLUME II na hata mikopo yenye
masharti ya kibiashara inayosemwa itakopwa haipo kwenye Revenue Book
v.
Huu mkanganyiko wa vitabu vya serikali moja imesababishwa na nini au
kuna mikopo na miradi hewa? Ni kwanini kitabu cha mapato (revenue book)
kinaonyesha mapato madogo kuliko kiwango cha matumizi?
vi.
Kuingiza malipo ya kiinua mgongo cha wabunge ambacho kinatakiwa kulipwa
mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria na kuwa chanzo cha mapato katika mwaka
huu wa fedha 2016/17 hiki si chanzo hewa? Nasema hivi kwa kuwa, kila
mwaka tutakuwa tukipitisha bajeti na hiki kilipaswa kuwa chanzo ifikapo
mwaka 2020 ambapo ndio kiinua mgongo hiki kinalipwa na ndio kingekuwa
chanzo cha mapato au serikali imepanga kulipa kiinua mgongo hicho kila
mwaka wa fedha?
Mwisho
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, tunaitaka serikali iwasilishe Vitabu
vyenye kumbukumbu na takwimu sahihi kabla ya kulitaka Bunge hili
kujadili bajeti hii na kuamua kuipitisha au kuikataa, la sivyo Bunge
litakuwa halitimizi wajibu wake kikamilifu kwa mujibu wa katiba ya Nchi
yetu.
7. WIZARA YA FEDHA NA JUKUMU LA UTEKELEZAJI MPANGO WA KWANZA WA TAIFA WA MIAKA MITANO 2011/12-2015/16
Mheshimiwa
Spika, Mpango huu ni wa kwanza kati ya mipango mitatu ya miaka mitano
mitano inayotumika kama chombo katika dhamira ya kuongeza kasi ya
utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka ishirini na mitano
(Tanzania Development vision(TDV)-2025). Malengo yakiwa ni Tanzania iwe
ya kipato cha kati ifikapo 2025 ambayo pamoja na mambo mengine litakuwa
taifa lenye:
i) Kiwango cha juu cha mapinduzi ya viwanda
ii) Ushindani na hali nzuri/bora ya maisha kwa wananchi wake
iii) Utawala wa sheria
iv) Jamii ya wasomi waliobobea
Vipaumbele vya msingi (Core Priorities) katika mpango huo ni :
i) Miundombinu / Infrastructure
ii) Viwanda / industry
iii) Maendeleo ya rasilimali watu /human capital development
iv) Nishati
Mheshimiwa
Spika, tuangalie mafanikio ya wizara ya fedha katika utekelezaji wa
jukumu lake la kusimamia utekelezaji wa mpango wa miaka mitano 2011/12-
2015/16.
1) Reli- mpango ulipanga kukarabati KM 2,707 ya reli ya kati, imefanikiwa kukarabati km 150 tu za Reli
2) Barabara – Kujenga na kukarabati km 5,204 za barabara. Zimejengwa km 2,775
3) Nishati- Ongeza uzalishaji wa umeme kufikia 2,780 MW. Sasa hivi tunazalisha MW 1,461
4)
Kilimo - Ukuaji wa mwaka kwa 6%, ukuaji kwa sasa 3.2% (ukuaji huu ni wa
kipindi chote toka tupate uhuru….).Kiwango cha umwagiliaji toka 345,690
– 1,000,000. Matarajio yalikuwa ni kuongeza eneo jipya la umwagiliaji
lenye ukubwa wa hekari 645,690. Mafanikio ni nyongeza ya hekari 115,656
tu!
5) Maendeleo ya viwanda na uzalishaji – kukua kwa 11%. Mafanikio ni ukuaji wa 6.6%
6)
Elimu - Nyongeza kada ya wasomi wa kiwango cha juu toka 2.7% mpaka 4.3%
ifikapo 2015. Idadi imepungua mpaka 2.5%. Halikadhalika kuongeza kada
ya wasomi wa kiwango cha kati toka 13.6% mpaka 17.8% ifikapo
2015.Imeongezeka kwa 1% tu kufikia 2015.
Mheshimiwa
Spika, Hakuna ubishi kwamba tukiwa tunaelekea katika mpango wa pili wa
miaka mitano, wizara ya fedha imeshindwa kutekeleza wajibu huu
kikamilifu, hali hii inatia mashaka ufanisi wa utekelezaji wa mpango wa
pili, wakati mpango wa kwanza umeisha kwa kusuasua!
Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ilieleze Bunge hili tukufu, Ni kwa
namna gani serikali imejipanga kuweza kufidia ombwe hili!ili miaka tisa
ijayo Tanzania liwe Taifa lenye mapinduzi ya viwanda ya hali ya juu,
hali bora ya maisha kwa wananchi wake, utawala bora na Taifa lenye
wasomi waliobobea (Rejea taarifa ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma
na Maendeleo ya jamii)ambayo ilitamka bayana kwamba hali ya elimu nchini
ni hatari kwa usalama wa Taifa. Ninukuu maneno ya kamati ‘Taifa letu
limejenga mfumo wa elimu ambayo haikidhi DIRA na Mahitaji ya Nchi’.6
7.1 UPATIKANAJI FEDHA KUTOKA HAZINA
a)
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi: Hadi kufikia Machi 2016 ,wizara
ilikuwa imepokea shilingi 660,333,375,957/- kati ya shilingi
816,080,198,000 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na maendeleo . Kati ya fedha zote zilizopokelewa kwa ajili ya
matumizi ya Wizara, mishahara ilikuwa 52%, matumizi mengineyo ilikuwa
47% na kwa upande wa bajeti ya maendeleo ni 1% tu.7
b)
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa: kwa miradi ya maendeleo
iliidhinishiwa shilingi bilioni 232.1. Mpaka Februari, 2016 Wizara
ilipokea shilingi bilioni 40 tu, sawa na asilimia 17.2 ya bajeti
iliyoidhinishwa na Bunge.
c)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto: Bajeti ya
maendeleo iliyotengwa 2015/16 ni bilioni 440.6, mpaka mwezi machi ikiwa
ni robo ya tatu ya mwaka hakuna fungu hata moja ambalo wizara hiyo
ilikuwa imepata zilizoidhinishwa na Bunge kwa angalau 50%. Halikadhalika
Fungu 52 – Idara kuu Afya hadi kufikia tarehe 31 March 2016 kiasi cha
fedha kilichopokelewa ni 31% tu ya Bajeti , halikadhalika fungu 53 kwa
Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii jinsia na watoto.
d)
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi: Katika kipindi cha mwaka 2015/16
wizara ilitengewa jumla ya shilingi 213,079,803,000/- kati ya fedha hizo
32,713,073,000 ilikuwa ni fedha za maendeleo. Hadi kufikia Machi 2016 ,
fedha za maendeleo zilizokuwa zimepatikana ni bilioni 5.1 ambazo ni
sawa na 15.9% tu ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.
Mheshimiwa
Spika, ikubukwe kwamba; Mpango wa kwanza wa miaka mitano (FYDP 1)
uliweka malengo ya kibajeti katika sekta ya kilimo (miaka mitatu ya
mwanzo) ya shillingi za kitanzania Bilioni 2,710.65 (Trillion 2.7).
(ambayo ingewezesha kilimo kukua toka 3.2% ya sasa mpaka 6%). Fedha
iliyokuja kutolewa kwa kipindi chote hicho ni shilingi 250.12 billioni
sawa na 9.23% ya mahitaji.
e)
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi: Wizara iliidhinishiwa
shilingi 511,525,227,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida . Hadi kufikia
robo ya tatu ya mwaka, yaani Machi 2016 Wizara ilikuwa imepokea kiasi
cha shilingi 316,402,868 ,828.00 sawa na 68%. Kuhusu bajeti ya
maendeleo, wizara imepokea jumla ya shilingi 360,922,754,359.61 sawa na
61.9% ya fedha iliyoidhinishwa 582,670,597,884.49. Bodi ya mkopo ambayo
ni sehemu muhimu sana ya wizara hii kupitia fungu 46 iliidhinishiwa
shilingi 418,300,000,000 kwa ajili ya Mradi Namba PT 4340 uliojulikana
kama Higher Education Students Loans ambao ni mradi wa kutoa Mikopo.
Hadi kufikia tarehe 15 Machi ,2016 Bodi ilikuwa imepokea jumla ya
shilingi bilioni 245 sawa na asilimia 55.9% tu ya bajeti iliyoidhinishwa
na Bunge . Fedha hizo zingetolewa zote kwa 100% wanafunzi wengi zaidi
wangepata mikopo.
f)
Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano: Wizara hii ni miongoni mwa
wizara (chache sana) zilizopata fedha zilizopangwa katika bajeti na
zaidi, hususan katika sekta ya ujenzi (barabara). Katika mwaka wa fedha
2015/16. Sekta hii ilitengewa shilingi 883,832,338,500/- kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maendeleo . Kati ya hizo, fedha za ndani kutoka
mfuko mkuu wa hazina wa serikali ni shilingi 191,619,568,500 na
shilingi 85,572,770,000 zilikuwa fedha za nje. Kwa upande wa fedha za
mfuko wa barabara zilitengwa shilingi 606,640,000,000. Hadi Aprili, 2016
fedha zilizotolewa ni shilingi 1.080,804,942,594. Kati ya fedha hizo
shilingi 607,350,007,730 ni fedha za ndani kutoka mfuko mkuu wa
hazina/serikali (Ongezeko la shilingi 415,730,439,230) ,shilingi
149,502,934,864 ni fedha za nje na shilingi 323,952,000,000 ni fedha za
mfuko wa barabara. Sehemu kubwa ya fedha za ndani zilizotolewa imetumika
kulipa madeni ya Makandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya
barabara.8
Mheshimiwa
Spika, Licha ya mabilioni yanayotumika kujenga barabara na kulipa
madeni yenye riba kubwa sana kutokana na serikali kuchelewa kulipa
madeni ya barabara, wakati kamati ikikagua miradi mbali mbali ya
barabara nchini imebaini kuwepo kwa changamoto ya kuharibika kwa
barabara mapema mara baada ya barabara kujengwa!9 Licha ya visingizio
vilivyotolewa vya uharibifu huo, sababu hizo hazina mashiko /msingi wa
kuhalalisha upotevu huo wa mabilioni ya fedha. Barabara zote hizi lazima
zifanyiwe ukaguzi wa kitaalam ili kujiridhisha na thamani ya fedha na
kazi iliyofanywa. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu sana
(tokea kipindi ambacho Rais alikuwa waziri wa miundombinu) Wizara hii
imekuwa ikihusishwa na uchakachuaji katika ujenzi wa barabara.
g)
Wizara ya Nishati na Madini: Wizara hii nayo ilipata fedha kuliko kiasi
kilichotengwa kwenye bajeti.Katika mwaka wa fedha 2015/16. Wizara
iliidhinishiwa na Bunge Jumla ya Shilingi bilioni 642.12. Kati ya fedha
hizo shilingi bilioni 502.30 sawa na 78% ya bajeti yote ilikuwa kwa
miradi ya maendeleo na shlingi 139.82 sawa na 22% zikiwa ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida .Hata hivyo bajeti iliongezeka kutoka bilioni
642.12 mpaka bilioni 762.12 (Nyongeza ya bilioni 120.12)
Mheshimiwa
Spika, Licha ya nyongeza hiyo, miradi ya REA inayogharimiwa na fedha za
Mfuko wa Nishati Vijijini ambao vyanzo vyake vya mapato ni pamoja na
tozo ya shilingi 100 katika kila lita ya mafuta ya petrol na Dizeli; na
shilingi 150 katika kila lita ya mafuta ya taa bado inasua sua. Hii
inatokana na fedha ambazo wananchi wanatozwa katika mafuta tajwa hapo
juu kwa makusudi ya kupeleka huduma ya UMEME vijijini kutumika kwa
matumizi mengine yasiyokusudiwa! Licha ya fedha hizo kuwa zimewekewa
wigo kisheria (Ring Fenced). Takwimu zinaonyesha kwamba tangu tozo hizi
zilipoanza kukusanywa Julai 2013 mpaka Machi 2016, fedha zilizopatikana
toka kwenye tozo ya petrol na Dizeli ni shilingi bilioni 493.8, Mafuta
ya taa shilingi bilioni 448.5 na shilingi bilioni 45.4 kutoka kwenye
‘Custom Processing Fee’.
Licha
ya makusanyo ya shilingi bilioni 987.7 (tozo ya petrol na dizeli) kiasi
kilichopelekwa kwenye umeme vijijini mpaka mwezi April 2016 ni shilingi
bilioni 366.95 tu sawa na 37.15% ya makusanyo yote. Katika mazingira
kama haya, kamwe serikali ya CCM haiwezi kujitapa imetekeleza wajibu
wake kikamilifu. Kwa lugha nyepesi imewaibia mamilioni ya wananchi
wanaoishi vijijini ambao mfuko huu uliundwa mahususi kwa ajili ya
kusogeza huduma za umeme kwao. Ikumbukwe hii fedha sio ya hisani bali ni
fedha ya nyongeza iliyoongezwa kwa kila lita inayonunuliwa na wananchi
kwenye mafuta ya taa, petrol au dizeli.
h)
Wizara ya Maliasili na Utalii: Katika mwaka wa fedha 2015/16 wizara ya
maliasili na utalii iliidhinishiwa jumla ya shilingi 66,313,757,000 kwa
ajili ya matumizi ya kawaida . Kati ya fedha hizo shilingi
45,235,955,000 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi mishahara na shilingi
21,077,802,000 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Mpaka Machi 2016, wizara
ilipokea 43,487,894,012.34 sawa na 65.5% ya bajeti iliyoidhinishwa
ambapo 32,714,043,166.18 ikiwa ni mishahara na 10,773,850,856 ni kwa
matumizi mengineyo. Fedha iliyoidhinishwa kwa miradi ya maendeleo ni
7,709,150,000/= . Fedha zilizotolewa ni bilioni 1 na yenyewe ni fedha ya
NJE sawa na asilimia 12.9 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kutokana na hali
hiyo katika miradi 10 ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa hakuna hata
mradi mmoja uliotekelezwa kwa ufanisi.10
i)
Wizara ya Viwanda na Biashara: Katika mwaka 2015/16 Wizara ilitengewa
jumla ya shilingi 87,470,349,000 ambapo 52,082,968,000 zilikuwa ni
matumizi ya kawaida (mishahara na matumizi mengineyo) na shilingi
35,387,381,000/- za matumizi ya maendeleo (shilingi 26,588,200,000 ni
fedha za ndani na shilingi 8,799,181,000 ni fedha za nje). Mpaka mwezi
Machi 2016 Wizara ilipokea 29,752,487,320/- sawa na 34% ya fedha
iliyotengwa. Kati ya fedha hiyo fedha za maendeleo zilizotolewa ni
1,602,111,662 tu ambayo ni fedha za nje! Kwa lugha nyingine fedha za
ndani za maendeleo zilizotoka ni 0%, na fedha ya nje iliyotoka ni 18%
tu! 11
j) Wizara ya Fedha na Mipango
Mheshimiwa
Spika, Wizara hii, licha umuhimu wake mkubwa katika uchumi wa Tanzania
katika mwaka wa fedha 2015/16, pamoja na mafungu yake nane (8)
iliidhinishwa kutumia jumla ya shilingi 7,326,769,737,771. Kati ya fedha
hizo shilingi 72,659,909,000 kwa ajili ya Mishahara (PE) Shilingi
7,218,508,850,128 kwa ajili ya Matumizi mengineyo (kati ya hizo shilingi
6,381,430,000,000 ni kwa ajili ya deni la Taifa). Kwa upande wa fedha
za maendeleo fedha zilizoidhinishwa ni shilingi 1,022,924,905,000 ambapo
fedha za ndani zilikuwa shilingi 651,541,992,000/- na fedha za nje
371,382,913,000. Mpaka mwezi machi 2016 wizara ilipokea fedha za
maendeleo shilingi 25,908,256,142, sawa na 3% tu ya fedha zote
zilizoidhinishwa!
8. MWENENDO WA MAPATO YA NDANI NA MKANGANYIKO WA TAARIFA ZA SERIKALI YA HAPA KAZI TU
Mheshimiwa
Spika, Katika mwaka huu wa fedha, na hususan miezi ya karibuni mwenendo
wa mapato umekuwa sio wa kuridhisha sana! Kodi ya ushuru wa forodha
haikufikia lengo na kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda hali inazidi kuwa
mbaya! Idadi ya meli zilizohudumiwa Januari - Aprili 2015 (TPA-
Kontena) zilikuwa 41 ukilinganisha na meli 16 tu zilizohudumiwa Januari-
Aprili 2016. Pungufu ya meli 25, badiliko la -61%. Halikadhalika kwa
Meli ya Mzigo Mchanganyiko ‘General Cargo’ meli zilizohudumiwa Jan-
April 2015 zilikuwa 53 ukilinganisha na meli zilizohudumiwa Jan – April
2016 ambazo ni 33 tu. Pungufu ya meli 20 sawa na badiliko la -37%
Mheshimiwa
Spika, Maelezo ya waziri wa fedha na Mipango kwenye kamati ya kudumu ya
Bunge ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2015/16 kwa
kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016 na mwelekeo hadi juni 201612
anaeleza sababu za upungufu kuwa ni ;
i) kupungua kwa uingizaji wa mizigo kutoka nje kutokana na hofu ya wafanya biashara katika kipindi cha uchaguzi
ii) Udanganyifu uliokuwa unafanywa na wafanyabiashara kwa kukwepa kodi ya ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazopitia bandarini
iii) kushuka kwa bei ya bidhaa katika soko la dunia
iv)
Na kwa upande wa kodi ya ongezeko la thamani upungufu umetokana na
marejesho ya VAT (VAT inputs) kuwa kubwa kutokana na uwekezaji katika
viwanda vya sementi pamoja na kupungua kwa mahitaji.
v) Halikadhalika tatizo la kutoa/kuomba risiti za kielekroniki katika huduma mbalimbali.
Mheshimiwa
Spika, Wakati wizara ya fedha ikitoa visingizio tajwa hapo juu, Mamlaka
ya usimamizi wa Bandari Tanzania katika maelezo yake ya Takwimu za
uingizaji mizigo katika Bandari ya Dar es salaam kwa kipindi cha
2013-2015 na kipindi cha Jan- April 2016 inaeleza sababu zilizopelekea
kupungua kwa shehena ya mizigo kuwa ni:
i) Kudorora kwa uchumi wa china (Hii imeleta madhara katika bandari nyingi duniani)
ii)
Hofu ya wateja kutokana na kuanzishwa kwa sheria ya VAT katika huduma
zinazotolewa na mawakala kwenye mizigo ya nchi jirani (VAT on Transit
GOODS) ambayo ni kinyume na sheria za kimataifa
iii)
Tatizo la Single customs Territory. Mizigo inayopatikana kwa mfumo wa
single customs territory unatozwa kodi kwa asilimia 100%, baadhi ya
wafanyabiashara wanaona kupitisha mizigo Tanzania ni gharama kubwa.
iv)
Kushuka kwa bei ya shaba duniani kumesababisha migodi mingi nchini
Zambia na DRC kufungwa na hata ile inayofanya kazi uzalishaji umepungua.
v)
Tozo la barabara (Road tolls) USD 16 kwa KM 100 hapa Tanzania
ulikilinganisha na USD 8 kwa kila KM 100 zinazotozwa kwa nchi nyingine
kwa magari yenye ekseli zaidi ya mbili.
vi)
Muda mfupi (Short grace period) kwa mzigo wa mafuta wa nchi jirani.
Tanzania ni siku 30 mzigo unatakiwa uwe umesafirishwa kabla ya kuwa
localised tofauti na nchi nyingine ambazo zinawapa siku 60 hadi 70.
vii)
Kuongezeka kwa Tozo kutokana na “Government Chemical Agencies” kutoza
USD 1.00 kwa Tani badala ya USD 100 kwa “ Bill of Lading” kwa bidhaa
ambazo wanazikagua kama vile mbolea hivyo kuongezeka kutoka wastani wa
USD 500 hadi USD 20,000 au Zaidi kutokana na ukubwa wa mzigo.
viii)
Mfumo wa TANCIS wa TRA kutoruhusu kugawanywa kwa “Bill of Landing” ili
kuruhusu kutoa mizigo ambayo haina tatizo panapokuwa na tatizo la mzigo
mmoja badala ya mzigo wote kuzuiwa na kusababisha gharama za tozo za
hifadhi kwa mteja ambazo sio lazima.
Mheshimiwa
spika, Ni aibu kubwa, kwa vyombo viwili vya serikali kuzungumza lugha
tofauti katika suala moja! Hiki ni kiashiria kwamba ama serikali hii
haifanyi kazi kama timu…ama waziri wa fedha amedhamiria kulipotosha
Bunge kwa kutoa sababu nyepesi huku zile za msingi akiziweka kibindoni
(sijui kwa manufaa ya nani).
Kambi
rasmi ya upinzani inaitaka Serikali ya CCM na Magufuli kutambua kwamba
Tanzania sio kisiwa na kwamba Bandari ya Dar es salaam inakabiliwa na
ushindani kutoka kwenye bandari za Mombasa (Kenya), Beira,Nacala na
Maputo (Msumbiji) , Durban (Afrika ya Kusini ), Walvis Bay (Namibia) na
Lobito (Angola) kama kuna vikwazo vyoyote vinavyoikwamisha bandari yetu
na nchi kushindana katika soko la ushindani vikwazo husika lazima
vishughulikiwe mara moja. Na wizara ya fedha iliyopewa jukumu kubwa la
kusimamia uchumi wa Tanzania haiwezi kukwepa jukumu hili.
9. UNUNUZI WA NDEGE ZA ATCL KUNA HARUFU YA UFISADI!
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa kitabu cha fedha za Maendeleo Volume IV Part A
fungu 62 kasma 4294 zimetengwa jumla ya shilingi Bilioni 500 fedha za
ndani kwa ajili ya kununua ndege za abiria kwa ajili ya shirika la Ndege
la ATCL.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa hotuba ya waziri wa ujenzi ,uchukuzi na
mawasiliano kifungu cha 185 alisema kuwa, nanukuu ‘kazi inayoendelea ni
kukamilisha taratibu za ununuzi wa ndege mbili mwaka 2016.Wizara kwa
kushirikiana na ATCL na wadau wengine imekwishaainisha ndege zinazofaa
kununuliwa baada ya kukutana na wawakilishi wa viwanda vya ndege vya
Boeing ya Marekani, Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier
ya Canada. Ndege mbili za awali zinazotarajiwa kununuliwa zitakuwa na
uwezo wa kubeba abiria 78 kila moja.Ndege ya tatu na ya nne
zitakazonunuliwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 zitakuwa na uwezo wa
kubeba abiria 155’
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango ni kwamba;
serikali imeamua kununua ndege kutoka kiwanda cha Bombadier ya Canada na
hii ni kutokana na ushauri ambao wizara ilipokea kutoka kwa wataalam
wake .Aidha tuna taarifa kuwa ndege mbili za mwanzo ambazo zitanunuliwa
sio mpya bali ni ndege ambazo tayari zilishatumika (kuukuu) kama taarifa
hizi ni za kweli , Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali
kutoa kwa Bunge hili sababu za kina zilizopelekea serikali kwenda
kununua ndege chakavu kinyume cha sheria ya manunuzi ya mwaka 2011.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa utafiti wetu kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
tuliamua kutafuta taarifa za kina na za uhakika juu ya Bei za ndege mpya
kwenye Viwanda ambavyo serikali ilisema kuwa iliwasiliana nao na
kufanya nao mazungumzo yaani Viwanda vya ndege vya Boeing ya Marekani,
Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada na na
kukuta bei za ndege mpya kuwa kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, kwa bei hizo hapo juu Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
tunataka kujua ni kwanini Serikali imeamua kununua ndege zenye uwezo wa
kubeba abiria 78 wakati fedha zilizopitishwa na Bunge hili ni Bilioni
500 ambazo zingetosha kununua ndege mpya kubwa na za kubeba abiria wengi
zaidi na hivyo kuwa na ufanisi na hata uwezo mkubwa wa kwenda safari za
mbali.Au ndio yaleyale ya kutumia Mawakala ambao wanajiwekea asilimia
kama ilivyokuwa huko nyuma katika ununuzi wa ndege ya Rais ?
Aidha
kwa mujibu wa waziri wa Fedha alipokuwa anawasilisha mpango wa
maendeleo hapa Bungeni alisema kuwa serikali imeamua kununua ndege mbili
aina ya Q 400 mbili na CS 300 Moja.
Kutokana
na uamuzi huo ni kuwa ndege aina ya Q400 mwaka jana ilikuwa dola
milioni 31.3 na ndege aina ya CS 300 ilikuwa dola milioni 82.0
Hivyo
basi kimahesabu ni kuwa ndege 2 aina ya Q400 na ndege 1 aina ya CS 300
ni jumla yake itakuwa shilingi Bilioni 318.120 (usd1= 2,200) na hivyo
kufanya kiasi cha shilingi Bilioni 181.880 kikisalia .
Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua ni kwanini tulitenga kiwango
hicho cha fedha (500bilioni) wakati bei halisi za ndege zinajulikana?
Hizi fedha zinazosalia baada ya manunuzi ya ndege hizo zitatumika
kufanya shughuli gani ? Je kuna Wakala katika ununuzi huu wa ndege
ambaye atapata Kamisheni, na kama yupo ni kiasi gani ?
9.1 Hakuna fedha za kuendesha ATCL
Mheshimiwa
Spika, pamoja na serikali kutenga fedha kwa ajili ya kununua ndege
mbili, jambo la kushangaza ni kuwa hakuna fedha za uendeshaji ambazo
zimetengwa na serikali kwa ajili ya shirika letu la ndege ATCL .Hata
kwenye mashirika ya serikali ambayo yatapata ruzuku kwa mujibu wa kitabu
cha Volume II ‘Public Expenditure’ kifungu 62 kasma 2006 kifungu 270846
ATCL zimetengwa shilingi bilioni 3.221 kwa ajili ya mishahara. Fedha
kwa ajili ya uendeshaji ‘other charges’ hakuna hata senti moja
iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha.
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua baada ya serikali kununua
ndege hizo mbili shirika litapata wapi fedha kwa ajili ya undeshaji na
hasa ikizingatiwa kuwa shirika mpaka sasa ni mufilisi ? Serikali
haikuona umuhimu wa kulipatia shirika hili ruzuku kwa ajili ya
uendeshaji wa shirika, mtaji wa kuanzia utatoka wapi?
9.2 UJENZI WA UWANJA WA NDEGE WA MWL.JK NYERERE PHASE II
Mheshimiwa
Spika, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere
awamu ya pili uko katika hatihati ya kusimama kutokana na Serikali
kutokutii makubaliano ya mikataba ambayo waliingia na Kampuni ya Ujenzi
ya BAM International ya Uholanzi. Hii ni baada ya wizara ya fedha kuamua
kukiuka masharti ya mkataba baina ya TAA na BAM International kuwa
fedha za kutekeleza mradi zitatolewa na HSBC kwa awamu zote mbili yaani
phase 1&2 na badala yake wizara ya fedha imeamua kwenda kutafuta
Mkopo Mpya nje ya makubaliano ya mkataba baina ya BAM na TAA wa Octoba
2015.
Mheshimiwa
Spika, jambo hili la wizara ya fedha kuingilia na kuanza kutafuta mkopo
sehemu nyingine nje ya makubaliano ya awali linahatarisha ukamilikaji
wa ujenzi wa uwanja huu na hata mkandarasi ametishia kusimamisha ujenzi
kama fedha za ziada hazitaongezwa kwa ajili ya mradi huu.
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua ni sababu gani zimeipelekea
wizara ya fedha kwenda kutafuta mkopo mwingine kutoka taasisi nyingine
nje ya makubaliano ya awali ya kimkataba? Nani ananufaika na utaratibu
huu wa kutafuta mkopo mpya badala ya kukamilisha taratibu zilizokuwepo?
Je, Kitendo cha kuanza kutafuta mkopo upya kitachelewesha ukamilikaji wa
mradi huu kwa kiwango gani? Nani atalipia hasara itokanayo na kuchelewa
kutekelezwa kwa mradi huu?
9.3 UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHATO
Mheshimiwa
Spika, ukisoma Mpango wa Maendeleo wa Taifa katika eneo la usafiri wa
Anga moja ya kipaumbele cha mpango katika uk.76 sehemu (x) ni ujenzi wa
kiwanja kipya cha ndege cha Chato. Mradi huu unahusisha ujenzi wa
kiwanja kipya cha ndege Chato kwa ajili ya huduma za usafiri wa anga kwa
mwaka huu wa fedha 2016/2017 mpango wa maendeleo umetenga kiasi cha
shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kuanza kufanyika kwa upembuzi yakinifu
kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja.
Mheshimiwa
Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua kama paliwahi
kufanyika kwa utafiti wa kina na majibu ya utafiti huo kuonyesha kuwa
ujenzi wa kiwanja cha ndege Chato ndio kipaumbele cha taifa kwa sasa na
kuwa mradi huu umelenga malengo mapana ya taifa ya kukuza uchumi wa
taifa letu. Kwanini fedha hizi zisingeongezwa kwenye kuimarisha viwanja
vilivyopo kwa sasa na hasa ikitiliwa maanani kuwa serikali ndio kwanza
inawaza kununua ndege tatu kwa shirika letu la Ndege.
10 .PRESIDENTIAL DELIVERY BUREAU-BRN
Mheshimiwa
Spika, kitengo hiki ambacho kilianzishwa kwa mbwembwe nyingi na
serikali ya awamu ya nne na hata Bunge hili kushawishiwa kuwa ndio njia
pekee ya kuongeza ufanisi serikalini chini ya kauli mbiu ya Matokeo
Makubwa Sasa! kimeshindwa kabisa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Itakumbukwa kuwa wakati kitengo hiki kinaanzishwa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni tulipinga uanzishwaji wa kitengo hiki kwani kilikuwa ni
kwa ajili ya ulaji tu.
Mheshimiwa
Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha wameamua kimya kimya
kukivunja kitengo hiki kwa kutotenga hata senti moja kwa ajili ya
mishahara na marupurupu mengine kwa ajili ya wafanyakazi wa Kitengo hiki
(VOTE 6) na badala yake zimetengwa kiasi cha shilingi 397,278,000 kwa
ajili ya kulipia kodi ya pango , (kasma 220700-rental expenses ).
Aidha,
ukiangalia bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha 2015/2016 kifungu hiki
kilitengewa kiasi cha shilingi 602,800,000 kwa ajili ya kodi hiyo hiyo.
Mheshimiwa
Spika, ukisoma katika kitabu cha Maendeleo - Volume IV utaona kuwa
fungu 06 President’s Delivery Bureau zimetengwa kiasi cha shilingi
bilioni 27,218,829,000 ambazo zote ni fedha kutoka nje (DFID & UNDP)
na maelezo yake ni kuwa ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya matokeo
makubwa sasa ambayo kimsingi haijaainishwa kwa ufasaha kwenye randama na
vitabu vya bajeti.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata maelezo ya kina juu ya mambo yafuatayo;
i.
Waliokuwa watumishi wa kitengo hiki wamehamishwa, wamefukuzwa au
wamesimamishwa kazi? Mbona hakuna fedha za mishahara na marupurupu
mengine kwa kitengo hiki?
ii. Ni sababu zipi zimepelekea kitengo hiki kutokupatiwa fedha za uendeshaji mwaka huu wa fedha?
iii.
Ni nani ataenda kusimamia fedha za Maendeleo takribani bilioni 27
ambazo zimetengwa kama kitengo hakina wafanyakazi? Au ndio kusema kwamba
DFID &UNDP itakuwa ikisimamia fedha zake moja kwa moja?
iv. Tangu kuanzishwa kwa kitengo hiki kimetumia kiasi gani cha fedha na ufanisi wake umekuwa upi?
v.
Fedha za malipo ya pango/kodi ni kwanini mwaka huu imepungua kwa zaidi
ya aslimia 48 kulinganisha na ya mwaka jana? Nani watakaa kwenye jengo
hilo wakati hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya mishahara yao?
11 . MILLENIUM CHALLENGE CORPORATION (MCC)
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa randama ya Wizara ya Fedha na Mipango kifungu 1007
katika mwaka wa fedha 2016/17 idara wameomba kuidhinishiwa jumla ya
shilingi milioni 500 kama bajeti yake ya matumizi ya kawaida. Kati ya
fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 60 (kasma 210300) zinaombwa kwa
ajili ya kuwalipa posho ya majukumu kwa watumishi 12 wa MCA-T Compact II
watakaofanya kazi ya uchambuzi wa miradi inayohitaji ufadhili wa MCC.
Aidha kiasi cha shilingi milioni 280 (kasma 220700) ni kwa ajili ya
kulipia pango la ofisi.
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kuwa Bodi ya wakurugenzi ya MCC mnamo tarehe
28,Machi 2016 ilisimamisha kutoa fedha kwa Tanzania katika mradi wa
MCA-T Compact II zaidi ya shilingi trilioni moja (USD. 472,824,825)
ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya miradi ya umeme nchini kutokana na
serikali hii ya CCM kupitisha sheria mbaya na kandamizi ya Makosa ya
Mtandao (Cyber Crime Act), Sheria ya Taifa ya Takwimu na kuminywa kwa
Demokrasia Nchini hasa kufutwa kwa matokeo halali ya Uchaguzi wa
Zanzibar ya Octoba 25,2016.
Mheshimiwa
Spika, baada ya Marekani kusimamisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi
huu, bodi ya wakurugenzi ya MCC ilimuandikia rasmi barua Rais wa
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mhe.John Magufuli tarehe 31 Machi,2016
na kumjulisha rasmi juu ya uamuzi wake .Pamoja na Rais kujulishwa kwa
barua Kambi rasmi ya Upinzani ina taarifa kuwa mpaka tarehe 11/05/2016
barua hiyo ya Bodi ya MCC ilikuwa haijapatiwa majibu na Ikulu .
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupatiwa majibu ya kina juu ya mambo yafuatayo;
i. Ni kwanini serikali inaomba fedha kwa ajili ya kulipa watumishi ambao watachambua miradi ya MCC ambayo haipo?
ii.
Ni lini serikali itaijibu barua ya bodi ya MCC? Kwanini imechukua muda
mrefu kiasi hicho kutoa majibu kwa barua yao? Hasa ikizingatiwa kuwa
katikati ya mwezi Juni Bodi ya MCC itakaa pamoja na mambo mengine itatoa
uamuzi wa mwisho juu ya jambo hili.
iii.
Hivi kulipia kiasi cha shilingi milioni 280 cha kodi ya ofisi kwa mwaka
ambayo ina watumishi 12 ni kiwango sahihi? Kinaendana na dhana ya
kubana matumizi?
12 . WATUMISHI HEWA SERIKALINI
Mheshimiwa
Spika, mnamo tarehe 01 Mei, 2016 wakati wa sherehe za maadhimisho ya
Mei mosi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.John Magufuli
alilitangazia taifa kuwa jumla ya watumishi hewa walikuwa wamefikia
10,295 na alisema kuwa kati ya watumishi hao hewa 8,373 wanatoka
TAMISEMI na watumishi 1,922 wanatoka Serikali Kuu. Aidha, aliendelea
kusema kuwa watumishi hao hewa walikuwa wakiligharimu taifa shilingi
Bilioni 11.6 kwa mwezi sawa na shilingi Bilioni 139 kwa mwaka na kwa
miaka 5 ni shilingi Bilioni 695.
Mheshimiwa
Spika, fedha hizi ni nyingi sana kwa nchi maskini kama hii ya kwetu
kupotea kwa sababu tu ya uzembe na kukosekana kwa usimamizi ulio makini
na dhabiti katika kusimamia rasilimali za taifa letu.Jambo hili
halikubaliki hata kidogo katika ulimwengu wa sasa na teknolojia
ilikofikia ya watumishi kupokea mishahara kupitia Benki.
Kambi
rasmi ya upinzani Bungeni, kupitia hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi
wa umma; ilitoa suluhisho la kuweza kushughulikia ufisadi huu wa
watumishi hewa ambao unalelewa na mfumo.
Aidha,
leo tunataka kujua hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya Maafisa
maduhuli, wakuu wa idara na vitengo pamoja na wahasibu ambao ndio
wanaondaa na kupitisha orodha ya watumishi ambao wanastahili kulipwa
kila mwezi ‘pay roll’. Hawa ndio wanaoandaa orodha, mbona mpaka leo bado
wapo kazini?
13 . WIZARA YA FEDHA, BENKI YA STANBIC NA SAKATA LA MKOPO WA DOLA MILIONI 600-UTAKATISHAJI FEDHA HARAMU
Mheshimiwa
Spika, Mwaka 2012/13 serikali ya Tanzania iliomba mkopo wa dola
millioni 600 kwa malengo ya kugharamia mpango wa Taifa wa miaka mitano.
Mkopo huu uluzihusisha benki zenye mahusiano ya kibiashara stanbic
(Tanzania) na Standard Bank PLC (kwa sasa inafahamika kama ICBC Standard
Bank PLC) (Standard Bank) ya Uingereza. Standard Bank ilihusishwa
kutokana na ukweli kwamba aina ya mkopo ambao serikali ilikuwa inautaka
Benki ya Stanbic Tanzania ilikuwa haitoi hiyo huduma ya aina hiyo.
Mheshimiwa
Spika, Inasemekana kwamba mchakato huo ulihusisha udanganyifu wa ada ya
mkopo, taarifa zinaonyesha kwamba ada halali iliyotakiwa kulipwa ni 1.4
% ya mkopo wote, hata hivyo ada iliyokuja kulipwa ni 2.4% ya mkopo
wote. Kutokana na udanganyifu huo, kuna kesi inayoendelea mahakamani
ikiwahusisha aliyekuwa kamishna Mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania,
ndugu Harry Kitilya (na mwenyekiti wa bodi ya EGMA, inayohusishwa katika
sakata hili), aliyekuwa Mkuu wa idara ya ushirikiano na uwekezaji wa
Benki ya Stanbic Tanzania, Shose Sinare pamoja na aliyekuwa mwanasheria
Benki ya Stanbic Tanzania, Bwana Sioi Solomon SUMARI.
Mheshimiwa
Spika, Sio dhamira ya Kambi Rasmi ya Upinzani kujadili wahusika tajwa
hapo juu kwa kuwa tunatambua, kanuni zetu za Bunge zinatuzuia kujadili
suala ambalo liko Mahakamani, lakini kwa kuwa leo ni siku ya kujadili
Bajeti ya Serikali ni wajibu wetu kama kambi kuhoji nini kilichopelekea
udanganyifu huo na kwa kiwango gani Serikali hii ilitekeleza wajibu wake
kikamilifu ili kuepusha makosa kama hayo kujirudia hasa ukizingatia
kwamba katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2016/17, serikali inatarajia
kukopa mikopo ya kibiashara ya aina hii ili kufidia ombwe la bajeti
yenye thamani ya shilingi trillion 7.4. Na wahusika wakuu katika
mchakato mzima ndio hao wahusika!
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inazo nyaraka mbali mbali, moja wapo
ikiwa ni barua toka TAKUKURU (TAASISI YA KUPAMBANA NA KUZUIA RUSHWA)
kwenda kwa mwanasheria mkuu wa serikali, Mhe. George M. Masaju yenye
kumbukumbu namba CACE255/362/01/104 ya tarehe 20/01/2016. Barua husika
imeambatanishwa na barua kwenda kwa Kitengo cha kimataifa cha makosa ya
jinai (International Criminal Unit) kikiomba msaada wa uchunguzi wa
wahusika katika sakata husika, huku ikirejea vifungu vya sheria
vilivyovunjwa!
Mheshimiwa Spika, Barua husika ina ainisha mambo yafuatayo:
1. Imewataja majina ya watu wanaochunguzwa kwa kukiuka:
a) vifungu 22,23,31,32 na 34(1)sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa (The Prevention and Combating of Corruption Act 2007.
b) Vifungu 333, 335 na 337 vya sheria ya kanuni za adhabu (The Penal Code (Cap 16 R.E 2002).
c) Vifungu 12,13 vya sheria ya kuzuia utakatishani wa fedha haramu ( Anti- Money Laundering 2006 (R.E 2012)
Watuhumiwa
wakiwa Stanbic Bank,Harry Msamire Kitilya (Aliyekuwa Kamishna Mkuu
TRA), Peter Anandi Nyabuti, Bashir Awale, Shose Sinare, Sioi Solomon
Sumari, Dr Servacius Likwelile (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha), Alfred
Paul Misana, Bedason Shalanda, Ramadhan Kijjah na Ngosha Said Magonya
2. Mpaka mwezi Februari 2012 makubaliano ya ada ya mkopo kwa benki zote mbili ( Standard na Stanbic ) ilikuwa 1.4% ya Mkopo wote
3. Mchakato ulisuasua sana /ulikwama mpaka mwezi septemba 2012 pale ambapo Stanbic ‘iliongeza’ ada mpaka 2.4% .
4.
Nyongeza hiyo ya 1% angelipwa ‘local partner’ na kwamba mgao huo
ulikuwa na malengo ya kumshawishi ndugu Harry Kitilya na pengine
‘maafisa wengine wa serikali ya Tanzania’ili wawape upendeleo wa
kuchukua mkopo toka benki tajwa hapo juu.
5.
Mara tu baada ya nyongeza ya 1%, mchakato ulikwenda kwa kasi ya ajabu.
Mwezi Novemba 2012 barua ya ‘mandate and fee’ ilisainiwa kati ya
standard bank, Stanbic Bank na Wizara ya fedha .
6.
Makubaliano husika hayakuelezea chochote kuhusiana na ‘local patner’ au
‘mtu wa tatu’ zaidi ya kuainisha ada ya ujumla ya 2.4% iliyoogezwa
kiaina toka 1.4%
7.
Pamoja na yote, utaratibu uliopangwa na pande zote tatu
(Stanbic/Standard na wizara ya fedha)uliruhusu fedha ya UMMA (MKOPO wa
kibiashara) kuingizwa kwenye akaunti binafsi ya ‘local partner’ badala
ya fedha husika kuingizwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Serikali ya
Tanzania.
8.
Pamoja na kwamba kulikuwa na viashiria vyote vya hatari ya rushwa na
udanganyifu,hakuna afisa yeyote ya serikali (wizara ya fedha) ,wala timu
ya benki ya standard bank aliyeonekana kujali,wala kuhoji chochote na
wala hawakutaka kuchunguza au kuhoji uhalali wa huyo ‘third party’ au
‘local partner’ ambaye sio sehemu ya mkataba /makubaliano kuingiziwa 1%
ya fedha ya Mkopo
9.
Baada ya fedha husika kuingizwa kwenye akaunti ya ‘Local Partner’ mwezi
Machi 2013. Kiasi kikubwa cha fedha kilianza kuondolewa haraka haraka
na ndugu Fratern Mboya. Ikumbukwe akaunti hii ilifunguliwa mahsusi mwezi
mmoja kabla (February 2013)
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iliambie Bunge hili tukufu;
i) Ni vigezo gani vilivyotumika kuwachuja watuhumiwa kutoka 11 mpaka 3?
ii)
Ni kwa vigezo gani wizara ya fedha iliruhusu fedha za Umma kuingia
katika akaunti binafsi huku ikifahamu (kama ilivyoainishwa kwenye barua)
anayeingiziwa fedha hajatajwa/hayuko kwenye mkataba baina ya serikali
na benki tajwa hapo juu?
iii)
Ni kwa kiwango gani wizara ya fedha inadhani, ilitekeleza wajibu wake
ipasavyo katika mchakato mzima? Kama ndio kwa nini? Kama sio ni hatua
gani zilizochukuliwa dhidi ya maafisa wa serikali (Wizara ya Fedha)
waliopewa dhamana kusimamia mchakato mzima?
iv)
Barua ya TAKUKURU inamtaja bwana Franten Mboya kuhusika na utoaji wa
mabulungutu ya fedha kwa kipindi cha siku 10 mfululizo, na kiasi
kilichobaki kuhamishiwa kwenye akaunti nyingine ya ‘local partner’.
Japokuwa Kambi Rasmi haijui hayo ‘mabulungutu’ yalienda kwa nani?. Kwa
nini ndugu huyu sio miongoni mwa washtakiwa? Kwa nini wameshtakiwa
watatu tu?
v)
Ni kwa nini mpaka sasa Dr. Servacus Likwelile , Katibu Mkuu Wizara ya
Fedha na ndugu Paul Misana kamishna wa wizara ya fedha hawajafunguliwa
mashtaka na wanaendelea kuitumikia serikali hii inayojinasibu kwa
kutumbua majipu? Mbona hii sheria sio msumeno tena? Inang’ata upande
mmoja tu?
13.2 Uwezo Mdogo wa Benki Kuu Kufanya Ujasusi wa Miamala ya Fedha na Kuchukua Hatua Stahiki
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatilia mashaka uwezo na
dhamira ya kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) cha Benki Kuu
kufanya ujasusi wa Miamala ya fedha katika kuzuia utakatishaji wa fedha
haramu hapa nchini.
Mheshimiwa
Spika, kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) kina mamlaka ya
kiutawala pekee na huishia kufanya uchambuzi wa taarifa za miamala ya
fedha na kuziwasilisha ama Jeshi la Polisi au PCCB, wakati huo huo PCCB
inalazimika kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili atoe ruhusa ya
kufungua mashitaka.
Mheshimiwa
Spika, matokeo yake ni kuwa FIU haina uwezo wa kufanya uchunguzi, wala
kuendesha mashitaka dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu jambo ambalo
ni mwanya unaotumiwa na watu waovu na mafisadi kama ilivyokuwa katika
wizi wa Mabilioni ya Rada, wizi wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow
na wizi wa fedha katika Mkopo wa Serikali dola milioni 600 kutoka
Stanbic Bank.
Mheshimiwa
Spika, mahakama ya mafisadi inayokusudiwa kuanzishwa na Serikali
haitaweza kufanya kazi kwa ufanisi kama mifumo iliyopo yenye mianya ya
kifisadi haitazibwa. Mfumo wa FIU ya Tanzania ni “administrative model”
wakati mfumo imara zaidi ni ule wa “Judicial Model” ambao unakiongezea
nguvu kitengo hicho cha kuzuia miamala ya biashara haramu za kutakatisha
fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa “Egmont13 Group of Financial Intelligence Units” Judicial Model of FIU inamaanisha kuwa
“The
Judicial Model is established within the judicial branch of government
wherein “disclosures” of suspicious financial activity are received by
the investigative agencies of a country from its financial sector such
that the judiciary powers can be brought into play e.g. seizing funds,
freezing accounts, conducting interrogations, detaining people,
conducting searches, etc.”
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuimarisha
kitengo cha FIU kwa kukiundia Mfumo wa Judicial Model ili kuepuka aibu
ambayo Taifa letu limekuwa likiipata kutokana na Serious Fraud Office ya
Uingereza kuwana na uwezo wa kurudisha fedha za zilizoibiwa kwa njia ya
kifisadi wakati kazi kama hiyo ingeweza kufanywa na vyombo vya hapa
nchini endapo vingeimarishwa kama ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inavyoshauri.
14 MADENI AMBAYO SERIKALI INADAIWA NA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII
Mheshimiwa
Spika, nchi yetu ina mifuko sita ya hifadhi ya jamii ambayo inachangia
kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa lakini pia maendeleo ya
kiuchumi ya wanachama wake. Mifuko hii ni Parastatals Pensions Fund
(PPF), Public Service Pension Fund (PSPF), Local Authorities Pension
Fund (LAPF) National Social Security Pension Fund (NSSF), National
Health Insurance Fund (NHIF) na Government Employees Pension Fund
(GEPF).
Mheshimiwa
Spika, pamoja na mchango mkubwa wa mifuko hii ya jamii katika uchumi wa
taifa na maendeleo ya kiuchumi ya wananchama wake; mifuko hii
imeathiriwa vibaya na mikopo isiyo na tija (non- performing loans)
inayotoa kwa Serikali na taasisi zake. Mifuko hii iko katika hatari ya
kufilisika kutokana na mikopo hiyo kukosa dhamana (guarantee) au
mikataba rasmi na Serikali jambo linalopelekea uwezekano wa fedha hizo
zilizokopeshwa kwa Serikali na taasisi zake kupotea au kurejeshwa kwa
kasi ndogo sana na hivyo kukosa tija.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 madeni ya Serikali kutoka katika
hifadhi za jamii yamekuwa yakiongezeka huku kukiwa na kasi ndogo sana ya
urejeshaji wa mikopo hiyo na wakati mwingine hakuna kabisa urejeshaji
unaofanyika.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, mpaka kufikia tarehe 30 Juni,
2014, deni la Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii lilikuwa limefikia
takriban shilingi trilioni 1. 69 ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha
takriban shilingi bilioni 975 kilikuwa kimeiva tayari kulipwa katika
mifuko hiyo ya hifadhi lakini Serikali haikulipa.
Jedwali Na.1. Mchanganuo wa madeni ya Serikali katika kila mfuko wa hifadhi ya jamii, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2014
Mheshimiwa
Spika, kufuatia malimbikizo ya madeni ya Serikali katika mifuko ya
hifadhi za jamii, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
iliitisha kikao cha baina ya Serikali na mifuko ya hifadhi za jamii
tarehe 24 Oktoba, 2014 ili kupata maelezo ya Serikali kuhusu ulipaji wa
madeni hayo. Katika kikao hicho, ilibainika kwamba kulikuwa na tofauti
ya kiwango cha deni la mkopo katika taarifa ya Serikali na ile ya mifuko
ya hifadhi za jamii. Kutokana na hali hiyo, kiliundwa kikosi kazi cha
kilichojumuisha wadau kutoka Serikalini, taasisi za Serikali na mifuko
ya hifadhi za jamii ili kufanya uchunguzi kujua kiwango halisi cha deni
ambalo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi za jamii.
Mheshimiwa
Spika, CAG anaeleza kwamba ripoti ya kikosi kazi hicho kilichoundwa ili
kubaini deni halisi Serikali inayodaiwa na mifuko ya jamii ilionyesha
kwamba hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2014 jumla ya deni halisi ambalo
Serikali ilikuwa inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii ni takriban
shilingi trilioni 1.875, ambapo kati ya fedha hizo shilingi bilioni
937.865 kilikuwa kimeiva tayari kulipwa lakini Serikali ilikuwa
haijalipa fedha hizo kwa mifuko ya hifadhi ya jamii. Hata hivyo, hadi
kufikia tarehe 7 Machi, 2015 Serikali ilikuwa haijalipa kiasi hicho
kilichoiva kwa mifuko ya hifadhi za jamii.
Jedwali
Na. 2 Mchanganuo wa madeni ya Serikali katika kila mfuko wa hifadhi ya
jamii yaliyofanyiwa uhakiki na kikosi kazi hadi kufikia tarehe 30
Septemba, 2014.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG, deni hili la trilioni 1.875 ambalo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii, halijumuishi deni la shilingi trilioni 7.066 ambalo PSPF inaidai Serikali kutokana na kuwahamishia wananchama waliokuwa chini ya mifuko ya pensheni kwenda PSPF ambao makato yao hayakuwa kwenye mfuko wa PSPF lakini Serikali ikaamuru walipwe penshini jambo ambalo ni kinyume na sheria ya mifuko ya hifadhi za jamii.
Mheshimiwa
Spika, ikiwa deni hili la shilingi trilioni 7 litajumlishwa na lile la
awali, Serikali sasa itakuwa inadaiwa na mifuko ya jamii Jumla ya
shilingi 8,942,426,246,224.49 (trilioni 8.942), na hii ni mbali na
madeni mengine ambayo Serikali inadaiwa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Seirkali kutoa maelezo mbele ya
bunge hili, ni kwa nini hailipi madeni (tena yaliyoiva tayari kulipwa)
kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.
15 KODI KATIKA MISHAHARA YA WAFANYAKAZI- PAYE
Mheshimiwa
Spika, wakati Rais Magufuli akilihutubia Taifa wakati wa sherehe za
siku ya Wafanyakazi Duniani alizungumzia suala la makato ya mishahara ya
wafanyakazi (PAYE). Na kwa mamlaka aliyonayo kama Mkuu wa Nchi aliasema
kuwa amepunguza makato hayo ya PAYE kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9,
na kuagiza kuwa suala hilo lianze kufanyiwa kazi katika mwaka wa fedha
2016/2017 .
Mheshimiwa
Spika, kodi hii ya mshahara imekuwa ni kilio kikuu kwa wafanyakazi na
ni ukweli ulio wazi kuwa kundi hili la wafanyakazi ndilo linalolipa kodi
kubwa kuliko makundi mengine katika jamii yetu. Busara iliyotumiwa na
Mhe. Rais Magufuli kupunguza Kodi hii ya PAYE kwa ngazi ya chini
iliyokuwa inalipa asilimia 11 na kuwa asilimia 9 kwa wale wote ambao
wanapokea mshahara wa kati ya shilingi 170,000 na 360,000/-, na kiwango
kitakachokatwa hiyo asilimia 9 ni shilingi 190,000/- ambayo ni tofauti
kati ya (360,000-170,000). Kwa wale ambao mshahara wao ni shilingi
540,000/-, PAYE itakuwa 17,100 + 20% ya tofauti kati ya silingi 540,000-
na 360,000/- ambayo ni shilingi 36,000/-, hii inafanya mshahara huo
kukatwa shilingi 53,100/-. Na kwa wale wanaopokea Mshahara wa shilingi
720,000/- kwa mwezi kodi ya PAYE ni shilingi 53,100 + 25% ya tofauti
kati ya shilingi 540,000/- na 720,000/- ambayo ni shilingi 45,000/-,
hivyo kufanya PAYE kwa mshahara wa shilingi 720,000/ kuwa shillingi
98,100/-.
Mheshimiwa
Spika, na kwa wale wote wanaopokea zaidi ya shilingi 720,000/- kwa
mwezi kodi ya Mshahara ni sawa na Tsh 98,100 +30% ya tofauti ya shilingi
720,000/- na kiwango cha juu cha mshahara. Mathalani kwa mtu anayepokea
mshahara wa shilingi 2,500,000/- kwa mwezi, PAYE ni sawa na Tshs
98,100+ 30% ya 1,780,000/- (534,000) na hivyo makato ya PAYE kuwa
shilingi 632,100/-
Mheshimiwa
Spika, ni dhahiri lengo la Mheshimiwa Rais lilikuwa zuri la
kuwapunguzia mzigo wa kodi watumishi wa umma, lakini inawezekana kabisa
Mheshimiwa Rais bado hajaelewa utaratibu mzima wa makato, kwani ingekuwa
ni bora kama punguzo la asilimia 2 lingekwenda sambamba kwa kila ngazi
ya mshahara (yaani punguzo la 2% kwa 20%, 25% na 30%) kwa kulingana na
utaratibu wa makato kama ulivyowekwa na TRA.
Ni
rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwamba Serikali itoe punguzo la
2% kwa ngazi zote za mshahara kama ambavyo Rais Magufuli alivyokuwa
amedhamiria, kinyume na hapo punguzo hilo la PAYE kutoka asilimia 11
hadi 9 itakuwa ni kiini macho kwa wafanyakazi.
Na
hii ni kutokana na ukweli kuwa wafanyakazi hawa bado wana mzigo mkubwa
sana wa kodi katika kupata huduma mbalimbali ambazo ni mahitaji muhimu
katika maisha yao ya kila siku kama vile VAT, na kodi nyinginezo , hivyo
kuwapunguzia makato ya kodi katika mishahara yao itawawezesha kuwa na
kipato cha kuwawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku.
16 UPOTEVU MKUBWA WA MAPATO ITOKANAYO NA MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa
Spika, misamaha ya kodi imekuwa ikilikosesha taifa fedha nyingi. Kambi
Rasmi ya Upinzani imekuwa ikishauri kila mara katika mapendekezo ya
hotuba ya bajeti kuwa misamaha ya kodi angalau isizidi asilimia 1ya Pato
la Taifa.
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia (Opening the gate 2012)
Tanzania ilikuwa ikipoteza takribani trillioni 2.9 kwa upotevu holela wa
kodi bandarini peke yake. Mwaka 2013/2014 misamaha ya kodi iliongezeka
kutoka 1.4 trilioni mpaka 1.8 trilioni. Mwaka 2014/2015 serikali ilitoa
misamaha ya takribani shilingi bilioni 1,627 sawa na 2% ya GDP.
Mheshimiwa
Spika, kwa takribani miaka mitano sasa serikali haijaweza kufikia lengo
la kupunguza kudhibiti misamaha ya kodi angalau isiyozidi 1%ya GDP. Hii
ni kutokana na uzembe mkubwa wa serikali katika kukusanya kodi, sera
mbovu za ukusanyaji wa mapato, udhaifu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
katika kukusanya kodi, vitendo vya rushwa kubwa na zile ndogo ndogo
zinazotokana na uswahiba wa karibu na baadhi ya viongozi wasio
waaminifu.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na misamaha ya kodi baadhi ya makampuni ya madini yenye
mikataba maalumu yameruhusiwa kuwekeza nje mauzo yake yote kinyume na
utaratibu wa kampuni nyingine ambazo hutakiwa kurejesha nchini mauzo
yao. Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la April 29, 2016, makampuni hayo
yenye mikataba maalum yameruhusiwa kuwekeza mauzo yake nje ya nchi
(illicit financial flows) ambapo jambo hilo limerasimishwa katika sheria
ya madini ya mwaka 2010.
Mheshimiwa
Spika, Jambo hili linaisababisha hasara kubwa serikali, ikiwa ni pamoja
na mapato yatokanayo na kodi zinazopotea tu kiholela. Ni wazi sasa
serikali iko katika wakati mgumu kifedha na maisha ya wananchi yanazidi
kuwa magumu kutokana na kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali ikiwemo
sukari, mafuta ya magari, vyakula n.k Hivyo ni aibu kwa serikali
kuendelea kulegeza, au kutojali kabisa hasara kubwa inayotokana na
misamaha ya kodi, mianya ya udhibiti wa makusanyo ya kodi, mikataba na
sera mbovu ambazo hazinufaishi taifa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa maelezo juu ya maswali yafuatayo:
i. Je, ni kampuni zipi na ngapi zenye ruhusa ya kuwekeza mapato yake yote nje ya nchi?
ii.
Je, serikali imefanya tathimini kuwa tunapoteza kiasi gani cha fedha za
kigeni yaani (foreign reserves) kutokana na mikataba ya namna hii?
17. MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA-UKUSANYAJI KODI
Mheshimiwa
Spika, Ili kuijengea uwezo TRA kutokana na uwezo mdogo wa kukusanya
mapato kulingana na vyanzo vilivyopo na uwepo wa mianya mingi ya
ukwepaji kodi na kushindwa kusimamia sera za misamaha ya kodi, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Serikali iridhie mpango wa
kufanya mapitio makubwa ya Mfumo Mzima wa Ukusanyaji wa kodi nchini
(Robust and Comprehensive Tax Regime Review) ili kuusuka upya kwa
kuondoa na kuziba kabisa mianya yote ya upotevu mkubwa wa mapato
uliosababishwa na uzembe wa Serikali kuisimamia TRA katika ukusanyaji wa
Mapato.
18. KIZUNGUMKUTI CHA MABILIONI YA JK
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kuwa toka serikali ya awamu ya nne iwepo madarakani
uliimbwa wimbo maarufu wa mabilioni ya Kikwete au JK ambayo yalitolewa
na serikali wakati huo ikiongozwa na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete.
Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia hoja mbalimbali za wabunge na maswali
yao hapa Bungeni walizungumzia na kuhoji utaratibu wa mgawanyo wa
mabilioni hayo na serikali haikuwahi kuweka wazi utaratibu mgawanyo huo
zaidi ya kutoa majibu ya kisiasa kuliko uhalisia wa jambo husika.
Mheshimiwa
Spika, wakati akijibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka (Viti
Maalum) katika Mkutano huu wa Bajeti Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri
Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mheshimiwa
Abdalah Possi alieleza Bunge hili kuwa kiasi cha shilingi bilioni 50.6
kilitolewa kama mikopo kwa ajili ya mabilioni ya Kikwete lakini ni kiasi
cha bilioni 41.53 ndicho kilichorudishwa na wakopaji. Hii inamaanisha
kuwa takribani bilioni 9 hazikuweza kurudishwa na walionufaika na
mabilioni hayo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuhoja masuala
yafuatayo; mosi, ni kwa nini fedha hazikurudishwa zote? Kwa sasa fedha
hizo zilizorudishwa zipo wapi na zinafanya kazi gani? Je serikali
imechukua hatua gani kwa fedha ambazo hazijarudishwa? Na je ni utaratibu
gani uliotumika kugawanywa fedha hizo na kwa vigezo gani?
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali kuwa pamoja na majibu
ya maswali yaliyoulizwa kuhusu mabilioni haya imwagize Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Fedha za serikali kufanya uchunguzi maalum juu ya fedha
hizi na kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Fedha za
Serikali (PAC) na taarifa ya Kamati kujadiliwa katika Bunge hili.
19 MIKATABA MIBOVU SEKTA YA MADINI NA NISHATI INALIKOSESHA TAIFA MAPATO
Mheshimiwa
Spika, kutokana na serikali kuendelea kuingia mikataba mibovu na ambayo
haina maslahi kwa taifa na kuifanya mikataba kuwa ni siri hata kwa
Bunge letu tumeendelea kupata hasara kama taifa kutokana na ukweli kuwa
mikataba imekuwa mibovu na ambayo inawanufaisha zaidi wawekezaji kuliko
taifa .
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa kitabu cha mapato volume I kinaonyesha kuwa Gesi
italiingizia taifa katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 kiasi cha
shilingi Bilioni 115.127 (kwa mujibu wa kifungu 140274 - sale of Gas).
Aidha
sekta ya Madini inategemewa kuliingizia Taifa kiasi cha shilingi
Bilioni 180.803 ambazo ni fedha zitakazotokana na mrabaha wa madini
(kifungu cha 140353 --Mineral Royalities) na kiasi cha shilingi Bilioni
29.494 ni kodi mbalimbali kutoka sekta ya Madini (kifungu 140101
–mineral Rent)
Mheshimiwa
Spika, serikali mara zote imekuwa ikijitapa hapa Bungeni na huko nje
kwa wananchi kuwa sasa uchumi wa gesi unaenda kutuondoa katika umasikini
kumbe ni hadaa na hali hii haikubaliki kila mwaka kuendesha serikali
kwa fedha za pombe na sigara ambazo ni nyingi kuliko fedha za sekta ya
nishati na madini –kwa mfano mapato ya VAT kutokana na sigara na bia ni
shilingi bilioni 263.940 mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye
bia, sigara na vinywaji vikali ni kiasi cha shilingi Bilioni 544.112
(kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato volume 1)
Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni , tunaitaka serikali kuiwasilisha mikataba
yote ya sekta ya Nishati na Madini hapa Bungeni ili Bunge liweze
kuipitia na kuchukua hatua za kuisimamia serikali kwa mujibu wa katiba,
na hii ndio itakuwa njia sahihi ya kuliokoa taifa na upotevu huu wa
mapato.Aidha tunamtaka waziri aeleze huu uchumi wa gesi ambao unasemwa
kila mara uko wapi ?
20. UUZWAJI WA HISA ZA TBL
Mheshimiwa
Spika, Msajili mkuu hazina Lawrance Mafulu alinukuliwa wakati serikali
ikipitisha bajeti ya mwaka 2015-2016 kuwa moja ya vyanzo vya mapato ni
kodi na mapato yasiyo ya kodi ambayo yanapatikana na shughuli za
kibiashara ambazo hufanywa na mashirika ya umma ambayo huleta faida
katika mfuko wa serikali kwa njia ya gawio.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ilikuwa inamiliki hisa milioni 11.7 katika Kampuni ya
bia ya Tanzania, lakini kwa utaratibu ambao haukueleweka Serikali
mwishoni mwa mwaka jana iliuza hisa hizo kwa thamani ya shilingi
15,200/- kwa kila hisa na hivyo kufanya jumla ya mauzo kuwa shilingi
bilioni 177.84
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inalazimika kukubali na kutaka maelezo
ya mauzo hayo, kutokana na ukweli kuwa katika bajeti ya mwaka 2015/16
Serikali kutokana na hisa hizo ilipata gawio la jumla ya shilingi
5,700,000,000/- na kwa mwaka huu wa bajeti 2016/17 kitabu cha mapato
VOLUME I Kampuni ya Bia inatoa gawio la shilingi 1,000/- tu. Hoja ni
kuwa inawezekanaje gawio liporomoke kutoka shilingi Bilioni 5.7 mwaka
jana hadi shilingi 1,000 mwaka huu?
Mheshimiwa
Spika, taarifa ya kamati ya Bajeti kuhusu utekelezaji wa bajeti ya
wizara ya Fedha na Mipango uk.21 inaonesha kuwa mauzo ya hisa asilimia 4
za Kampuni ya Bia na asilimia 2.5 za Kampuni ya sigara zingeuzwa kwa
shilingi bilioni 200. Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa makusanyo hadi
februari, 2016 zilikuwa ni shilingi 344,470,000,000/- Kambi Rasmi ya
Upinzani inapenda kupata maelezo ni kwa nini fedha hizi hazikuwa
zimeoneshwa kwenye makisio ya makusanyo kwenye kitabu cha JUZUU ya I uk.
10 hadi 13?
21. KUFUTWA KWA MISAMAHA YA KODI KWA MAJESHI YETU
Mheshimiwa
Spika , wakati waziri wa Fedha akiwasilisha hotuba ya Bajeti alisema
kuwa moja ya hatua ambazo serikali inachukua ili kudhibiti upotevu wa
mapato ya Serikali ni pamoja na kufutwa kwa misamaha ya kodi kwa Majeshi
ya Ulinzi na Usalama na badala yake alipendekeza kuwepo kwa Posho
maalum kwa ajili ya kuwawezesha wanajeshi wetu kununua mahitaji yao
muhimu.
Mheshimiwa
Spika, waziri wa Fedha katika hotuba yake uk.88 alisema kuwa tarehe ya
kuanza kutumika kwa utaratibu huu ni kuanzia Julai 1,2016 .
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupatiwa majibu juu ya masuala yafuatayo;
i.
Fedha za kulipa Majeshi yetu ‘posho maalum’ zipo katika fungu lipi la
fedha za bajeti na hasa ikizingatiwa kuwa mafungu yote katika wizara
husika yalishapitishwa na Bunge hili na posho hiyo haikuwepo?
ii.
Je zile bidhaa na vifaa vilivyopo kwenye bohari za majeshi yetu
zitapelekwa wapi na zipo kiasi gani kwani utekelezaji wa jambo hili
umekuwa wa ghafla sana? yaani chini ya wiki tatu kabla ya utekelezaji
wake kuanza
iii.
Kwanini serikali isingewachukulia hatua wajanja wachache waliokuwa
wanajinufaisha na msamaha huo na badala yake imeamua kuyaadhibu majeshi
yetu yote?
22. BAJETI MBADALA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KWA MWAKA WA 2016/2017
Mheshimiwa
Spika, bajeti mbadala ya KRUB, ni tulivu na yenye kuleta matumaini
yenye heri kwa Watanzania. Katika kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa
katika mwaka 2015, cha mwezi Juni 2016 kilichotolewa na wizara ya fedha
Sura ya I ukurasa wa 1 aya ya 2 kinaonesha takwimu za awali za Pato la
Taifa kwa mwaka husika ni shilingi 90,863,681,000,000.
Angalia jedwali la I;
Mheshimiwa
Spika, ni ukweli ulio wazi kwamba; tukiweka mazingira mazuri na rafiki
kwa mlipa kodi, tukipanua wigo wa kodi, tukiwa na sera na viwango vya
kodi vinavyotabirika na endelevu, ufanisi ukiongezeka TRA kwa asilimia
50, kudhibiti ukwepaji wa kodi, kupunguza misamaha isiyokuwa na tija
hadi kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa, kuongeza ufanisi bandari ya
Dar-es Salaam, kuweka mazingira mazuri na endelevu sekta ya Utali,
kukusanya kwa ufanisi mapato kwenye sekta za madini, uvuvi, maliasili,
nyumba,ardhi n.k. Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi
hadi kufikia aslimia 20.
Mheshimwa
Spika, inawezekana kutekeleza kwa mambo hayo hapo juu. Hivyo, KRUB
inapendekeza kukusanya shilingi 18,990,509,329,000/- ambapo mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi shilingi 18,172,736,200,000/- sawa na asilimia 20
ya Pato la Taifa. Aidha, mapato ya Halmashauri ni asilimia 0.9 ya pato
la Taifa sawa na shilingi 817,773,129,000/-
SURA YA MBADALA YA BAJETI 2016/17
Mheshimiwa
Spika, Bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani inategemea misaada
toka kwa nchi wa hisani na kwa mashirika ya kimataifa (utegemezi) kwa
16% tu na tunaamini kwa mazingira mazuri yakiendelea kuwekwa bila ya
kuwa kero kwa wadau wa sekta mbalimbali, na pia kuondoa mchwa wanaokula
fedha za miradi katika halmashauri, ni dhahiri kwa miaka miwili ijayo
tungeweza kujitegemea.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa inatilia mkazo juu ya
ukuzaji uchumi vijijini (Rural Growth) na hivyo kuwa ni kipaumbele cha
kwanza katika Bajeti zake Mbadala. Vivyo hivyo kwa mwaka huu imetenga
35%. Tunaamini kabisa kuwa ili Tanzania tuwe na uchumi wa viwanda ni
lazima miundombinu ya barabara kutoka pembezoni mwa wilaya zetu, maji na
nishati viwe ni vya uhakika, kwa njia hiyo hata uhamiaji wa vijana
kutoka vijijini kuja mijini utapungua kabisa kwani wawekezaji watafungua
viwanda vya uzalishaji na hata kilimo cha uhakika kitafanyika kwani
masoko yatakuwa na uhakika vile vile.
Mheshimiwa
Spika, Kipaumbele cha pili ni kwenye huduma za jamii ambazo kwa
muktadha wetu ni elimu, afya na maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani,
ambapo Bajeti Mbadala imetenga 28% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Kipaumbele cha tatu ni Miundombinu kwa maana ya Barabara za
kuunganisha wilaya na wilaya, usafiri wa reli, usafiri wa ziwani n.k na
imetengewa 17% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Kipaumbele cha nne ni kwenye usimamizi wa ardhi, kwani
tumeshindwa kutumia fursa ya ardhi yetu kukuza uchumi, na kwakuwa
tulipendekeza uwepo wa chombo cha kusimamia na kuratibu sekta nzima ya
majengo (Real estate regularatory authority-Rera) na pia kuhakikisha
kuwa kodi za ardhi zinalipwa kwa utaratibu unaoeleweka, hivyo basi,
imetengwa 12% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, kipaumbele cha tano na cha mwisho ni kuwekeza katika sekta ya
utalii, kwani sekta hii ndiyo itakayoleta fedha za kigeni na kwa muda
mfupi kama tutapunguza vikwazo vinavyopunguza idadi ya watalii
wanaoingia na kukaa nchini kwa muda mfupi. Hivyo basi,bajeti mbadala
imetenga 8% ya fedha za maendeleo.
Mheshimiwa
Spika, Bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani haikopi mikopo ya
kibiashara kwani mikopo ya kibiashara hasa kwa mabenki ya ndani ndio
chanzo kikuu cha kuua sekta binafsi hapa nchini. Hivyo basi kwa kuliona
hilo bajeti mbadala ni bajeti ya kuweka mazingira wezeshi kwa
wajasiliamali wa ndani na nje kuwekeza maeneo ya vijijini kwa sekta zote
za uchumi.
24. HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kusema kwamba, Serikali hii
ya awamu ya tano imeanza vibaya muhula wake wa uongozi kwa kulidanganya
bunge kwa kuleta bajeti yenye takwimu zinazokinzana. Serikali imeeleza
katika bajeti yake kwamba inakusudia kukusanya na kutumia shilingi
trilioni 29.539 lakini cha ajabu ni kwamba vitabu vya mapato vinaonyesha
kwamba Serikali itakusanya shilingi trilioni 22.063 na cha ajabu zaidi
vitabu vya matumizi vinaonyesha kwamba Serikali itatumia shilingi
trilioni 23.847 ikiwa ni ongezeko la matumizi ya shilingi trilioni 1.784
nje ya makusanyo.
Mheshimiwa
Spika, Ukichukua jumla ya bajeti yote iliyotajwa na Serikali ya
shilingi trilioni 29.539 ukatoa jumla ya makusanyo halisi ya shilingi
trilioni 22.063 utapata tofauti ya shilingi trilioni 5.476 ambazo haziko
kwenye makusanyo wala haziko kwenye matumizi. Ukichukua tofauti hiyo ya
shilingi trilioni 5.476 ukajumlisha na shilingi trilioi 1.784 ambazo
ziliingizwa kwenye matumizi nje ya makusanyo utapata jumla ya shilingi
trilioni 7.26 ambazo hazimo katika makusanyo halisi ya Mapato.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imetafakari kina jambo hili na kufikia
uamuzi kwamba; Serikali imelihadaa bunge na wananchi kwa kuliaminisha
Bunge na wananchi kwamba ina bajeti ya shilingi trilioni 29.539 wakati
ki-uhalisia Serikali hii ya awamu ya tano ina bajeti ya shilingi
trilioni 22.063 tu ikiwa ni pungufu ya shilingi bilioni 432
ukilinganisha na shilingi trillioni 22.495 za bajeti ya Serikali kwa
mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
David Ernest Silinde (Mb)
NAIBU WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YAUPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA
YA FEDHA NA MIPANGO
10 Juni, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni