Rais wa TFF Jamal Malinzi akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji wa tuzo jana usiku
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia kwa Rais wake Jamal Malinzi,
jana usiku lilitoa ofa kwa wazazi (baba na mama) wa Simon Msuva
kuhudhuria mechi mbili za timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ itakapokuwa
ikicheza dhidi ya Uganda kwenye michezo ya awali kuwania kufuzu
kushiriki michuano ya Afrika inayoshirikisha wachezaji wa ligi za ndani
(CHAN).
Malinzi
ametoa ofa hiyo kwa wazazi wa Msuva ambaye jana alitangazwa kuwa
mchezaji bora wa ligi kuu ya soka Tanzania bara iliyomalizika Mei 9
mwaka huu ikiwa kama zawadi na shukrani kwa wazazi hao mara baada ya
wazazi wa Msuva kueleza njia ndefu aliyopita mtoto wao kufikia mafanikio
anayoyapata hivisasa na wao kusimama nyuma yake kwa kila jambo gumu na
rahisi alilopitia kijana wao.
Baba yake
Simon Msuva (mzee Msuva) akiwa ameinua juu tuzo ya mfungaji bora wa
ligi iliyokwenda kwa Simon Msuva, (kulia kwake) ni Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Juma Nkamia na (kushoto kwake)
ni mama yake Simon Msuva.
Malinzi
amesema kuwa, amevutiwa na jinsi wazazi hao walivyosimamia na kukilea
kipaji cha mtoto wao hivyo, TTF imeamua kuwapongeza kwa hatua hiyo na
itagharamia kila kitu ili wazazi wa Msuva wapate kumuona kijana wao
akicheza uwanjani kuiwakilisha Tanzania kwenye mechi dhidi ya Uganda
itakayochezwa Zanzibar Juni 20 na ile ya marudiano itakayopigwa jijini
Kampala huku TFF ikigharamia kila kitu kuanzia usafiri, gharama za
viingilio, chakula na malazi ya wawili hao.
“Nimeguswa
sana na maneno ya baba yake Msuva, ameongea maneno mazito sana ambayo
yanaonesha ni jinsi gani amehangaika kutafuta mafanikio ya leo ambayo
kijana wao (Simon Msuva) anayapata. Ni safari ndefu sana wamepitia na
wanahitaji pongezi za dhati na ni mfano wa kuigwa na wazazi wengine”,
alisema Malinzi huku akionekana kuvutiwa na wazazi wa Msuva.
“Kwasababu
hiyo, kama TFF tunawaomba mhudhurie kumshuhudia mtoto wenu atakapokuwa
akicheza kwenye timu ya Taifa wakati ikicheza dhidi ya Uganda mchezo
utakaofanyika Zanzibar Juni 20, pia vilevile kwenye mchezo wa marudiano
utakaochezwa jijini Kampala. TFF itagharamia kila kitu kuanzia usafiri,
viingilio, malazi na chakula , karibuni sana kwenye mechi hizo”, alisema
Malinzi.
Awali
baba yake Msuva alisema, amepata changamoto nyingi sana wakati
anahangaika huku na kule kuhakikisha mwanae anafanikiwa katika mchezo wa
soka ambao alionesha kuuhusudu tangu akiwa kijana mdogo. Mzee Msuva
alisema, ilifika wakati aligombana na mama yake Msuva kwasababu ya
kumtafutia Msuva timu ya kucheza wakati mama yake alikua anahitaji Msuva
aelekeze nguvu zake zote kwenye elimu akiamini ndiyo itamletea
mafanikio maishani.
“Nimehangaika
sana na Msuva kabla hajapata mafanikio aliyonayo leo, ilifikia wakati
nagombana na mama yake kwasababu ya mpira. Mama yake Msuva alikuwa
akitaka mtoto aelekeze nguvu zote shule lakini mimi nilikuwa nyuma ya
Msuva kuendeleza kipaji chake cha kucheza mpira alichokionesha tangu
akiwa mdogo. Sikumzuia kwenda shule, ila nilikuwa nahakikisha anapata
pia nafasi ya kucheza mpira”, alisema mzee Msuva.
Wazazi wa
Simon Msuva wakiwa wameshika tuzo ya mtoto wao mara baada ya
kukabidhiwa tuzo hiyo na Mh. Juma Nkamia aliyekuwa mgeni rasmi kwenye
hafla hiyo
“Nimezunguka
naye kwenye timu nyingi sana nikimpeleka akapate nafasi ya kucheza
kabla hajatua Yanga ambapo wengi wametambua uwezo wake akiwa hapo.
Kwakweli namshukuru sana Mungu kwa mafanikio haya aliyopata kijana wetu
lakini naishukuru pia Yanga na watu wengine wote waliochangia mafanikio
haya ya Msuva”, aliongeza mzee Msuva.
Msuva
yupo na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo imepiga kambi nchini Ethiopia
kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri utakaopigwa nchini Misri Jumapili
Juni 14 mwaka huu kuwania kufuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika
(AFCON). Jana aliwakilishwa na wazazi wake kwenye hafla ya ugawaji tuzo
kwa wachezaji, timu, makocha na waamuzi waliofanya vizuri kwenye ligi ya
msimu wa 2014-2015 iliyomalizika hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni