\
Kansela
wa Ujerumani Angela Merkel alimkaribisha rasmi Rais wa Kenya Uhuru
Kenyatta mjini Berlin ambapo Merkel alisisitiza haja ya kuimarsiha
uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwa kuitaja Kenya kuwa ni mahala
thabiti.
Rais
Kenyatta amesema kuwa vita dhidi ya ugaidi ni suala linalolikumba bara
la Afrika kwa jumla akigusia makundi ya waasi wenye itikadi kali katika
nchi kama Nigeria na Mali na hata nchi yake Kenya ambako kumeshuhudiwa
mashambulizi ya kigaidi.
Kenyatta
amesema Umoja wa Afrika sharti ujiimarishe katika ukusanyaji wa taarifa
za kijasusi na kuhimiza ushirikiano zaidi miongoni mwa nchi za Afrika
ili kukabiliana na kitisho cha itikadi kali na ugaidi.
Hata
hivyo Kenyatta amesema kitisho cha ugaidi sio tatizo barani Afrika pekee
bali ni kitisho kwa ulimwengu mzima na hivyo jitihada za dunia nzima
zinahitajika kupambana dhidi ya ugaidi.
Merkel aitaja Kenya mahali Thabiti
Kwa
upande wake, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesifu juhudi za Kenya
za kulinda amani katika nchi jirani ya Somalia ambako wanajeshi wa Kenya
wanapambana dhidi ya waasi wa Al Shabab, kundi lenye mafungamano na
mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.
Ziara ya
Kenyatta nchini Ujerumani inakuja huku nchi za Ulaya zikijaribu kufufua
uhusiano na nchi za Afrika. Merkel amesisitiza haja ya kuwepo kwa
uhusiano imara zaidi akisema kwa miaka kadhaa bara la Ulaya liliisahau
Afrika.
Merkel
amesema China ndiyo ilijaza pengo hilo lakini sasa wananuia kubadilisha
hali ilivyo na kurejesha uhusiano kati ya Ulaya na Afrika.
Kansela
huyo wa Ujerumani amesema Kenya na Ujerumani zinaweza kushirikiana
kuhusu masuala mengi yakiwemo utalii, kupambana dhidi ya ugaidi,
usalama, kupambana dhidi ya umaskini , kuwashajaisha vijana na kuhimiza
utawala bora.
Ujerumani
na Kenya zimekuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi. Ujerumani
ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Kenya kama taifa huru mnamo mwaka
1968 na Kenya ni mshirika mkubwa wa Ujerumani kibiashara barani Afrika.
Idadi
kubwa ya watalii wanaoizuru Kenya kila mwaka hutokea Ujerumani na taifa
hilo pia linapokea kiwango kikubwa cha misaada ya maendeleo kutoka
Ujerumani.
Lakini
ziara ya kiongozi huyo wa Kenya nchini Ujerumani na barani Ulaya kwa
jumla ilichukua muda tangu kuingia madarakani miaka mitatu iliyopita
kutokana na kesi iliyokuwa ikimkabili katika mahakama ya uhalifu ya ICC.
Ulaya yanuia kuimarisha uhusiano na Kenya
Nchi
nyingi za magharibi ziliupa utawala wa Kenyatta kisogo kutokana na yeye
kukabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Hata hivyo mwaka
jana mahakama hiyo ya ICC ilifutilia mbali kesi dhidi yake.
Rais
Kenyatta alifanya mkutano pia na mabalozi wa nchi za Afrika
wanaoziwakilisha nchi zao Ujerumani ambako alizushukuru nchi za Afrika
kwa kusimama na Kenya kuhusu suala la ICC.
Hii leo
jioni, kiongozi huyo wa Kenya anatarajiwa kukutana na wakenya wanaoishi
Ujerumani kabla ya kukamilisha ziara yake nchini humu hapo kesho.(P.T)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni