WATEJA wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mikoa ya
Iringa na Njombe wanatarajia kuongezeka kutoka 63,300 wa sasa hadi
zaidi ya 93,000 ifikapo mwaka 2017.
Ongezeko hilo linakwenda sambamba na kuviunganisha vijiji vipya 93
baada ya vingine 84 katika mikoa hiyo kuunganishwa na umeme wa gridi
ya Taifa kupitia awamu ya pili ya mradi wa usambazaji umeme vijijini
unaotekelezwa kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Meneja wa Tanesco mkoani Iringa, Sarah Assey akizungumza ofisini
kwake jana alisema ongezeko hilo la wateja 30,000 wapya kwa mpango
wa kuwaunganisha 15,000 kila mwaka, litakwenda sambamba na
matumizi ya mita za Luku kwa wateja wake wote.
“Mpango wa shirika ni kuona wateja wetu wote wanafungiwa mita za
Luku ifikapo mwaka 2017; mpango utakaohitimisha matumizi ya mita za
zamani,” alisema na kuongeza kwamba mpaka sasa zaidi ya wateja
38,000 katika mikoa hiyo wamekwishafungiwa mita za Luku.
Alisema mpango wa kuwaunganisha na mita za Luku wateja wao wote utapunguza ajira ya wasoma mita na hivyo kupunguza
matumizi ya shirika.
Alisema Tanesco inataka kuondokana na matumizi ya mita za zamani kwa wateja wake kwa sababu ufanisi wake unazidi kushuka
hivyo kulisababishia hasara.
Meneja huyo alisema kuachana na matumizi ya mita hizo za zamani kutamaliza pia kile kinachoonekana kama kero wanayopata
wateja wao wakati wa kulipia Ankara zao katika ofisi za shirika hilo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni