KAMPUNI
ya simu ya TTCL imetoa msaada wa saruji na mbao katika Shule ya
Sekondari ya Luswisi iliyopo Kata ya Luswisi Wilaya ya Ileje mkoani
Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za Walimu na chumba kimoja cha
darasa.
Kampuni
hiyo ilitoa msaada wa mifuko 100 ya saruji na mbao vyenye thamani ya
shilingi Milioni tatu ikiwa ni kupunguza changamoto inayowakabili Walimu
wa Shule hiyo ambayo inawalimu 22 huku ikiwa na Nyumba moja
iliyokamilika ambayo anaishi Mkuu wa Shule.
Wakizungumza
baada ya kupokea msaada huo baadhi ya Walimu hao wakiongozwa na Makamu
Mkuu wa Shule, Mseven Ndangala, alisema Walimu wanaishi katika wakati
mgumu kwani asilimia kubwa wamepangishwa na wanakijiji sehemu ambayo ni
mbali na eneo la shule.
Alisema
Walimu wengi wamepanga umbali wa kilomita 7 kutoka shuleni hivyo
hulazimika kukodi pikipiki kuwapeleka na kuwarudisha shule kwa gharama
ya shilingi 6000 kwa siku hali inayowarudisha kwenye umaskini na
kupunguza ari ya kufundisha kutokana na kutumia gharama kubwa kwenye
usafiri.
Aliongeza
kuwa hivi sasa kuna walimu wapya watano ambao kwa mazingira yalivyo
hawataweza kupanga kutokana na ukosefu wa fedha na kuwalazimu kuishi
walimu wote watano kwenye chumba kimoja hali inayoonesha kuwakatisha
tama kuendelea kufundisha shuleni hapo.
Awali
akikabidhi msaada huo, Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, James Mlaguzi,
alisema Kampuni ilipata maombi kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Ileje,
Aliko Kibona kwa ajili ya kusaidia kupunguza adha hiyo jambo ambalo
lilikubaliwa na hatimaye kuwafikishia.
Alisema
kampuni imejipanga kuhakikisha mwishoni mwa mwaka huu inapeleka huduma
za mawasiliano vijijini ili kuwawezesha wakulima kutafuta masoko ya
mazao yao kwa njia za mtandao.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Ileje aliyemaliza muda wake, Aliko
Kibona aliwashukuru kampuni ya TTCL Hususani Afisa mtendaji Mkuu Dk.
Kazaula Kamugisha kwa kumkubalia ombi lake ili kuhakikisha walimu
wanakuwa na mazingira mazuri ya kufundishia kwa kuwajengea nyumba nzuri.
Aidha
alitoa wito kwa Watendaji wa vijijini na Kata kuhakikisha wanasimamia
vizuri msaada huo kwa kuhakikisha unafanya kazi zilizokusudiwa ili
kuwaridhisha waliotoa misaada na hivyo kuwafanya wawe na moyo wa
kujitolea katika kipindi kingine.
Aliongeza
kuwa ni wajibu wa Wabunge, wadau na wananchi kuhakikisha wanatumia kila
njia wanatengeneza mazingira mazuri ya Walimu kuwa na ari kubwa ya
kufundisha kuliko kuitegemea Serikali kwa kila kitu.
Meneja
wa TTCL Mkoa wa Mbeya, James Mlaguzi akisoma taarifa ya msaada
uliotolewa na kampuni hiyo katika shule ya Sekondari Luswisi.
Mbunge
wa Ileje aliyemaliza muda wake,Aliko Kibona akitoa shukrani kwa niaba
ya wananchi wa Kata ya Luswisi kwa kampuni ya TTCL kutokana na msaada
waliopokea.
Mbunge Aliko Kibona pamoja na Meneja wa TTCL wakikabidhiana mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.
Mbunge na Meneja wakipongezana baada ya kukabidhiana Saruji na Mbao.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Luswisi wakifurahia msaada uliotolewa na TTCL.
Wanafunzi wakisaidia kushusha mifuko ya saruji iliyotolewa na kampuni ya TTCL.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni