.

.

14 Septemba 2015

ALICHOKISEMA BEN MKAPA KWA MWANDISHI DAVID MARTIN 1995


Ndugu zangu,
Historia ni Mwalimu mzuri. Wakati nikiangalia uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi CCM, Zanzibar jioni hii, nimeguswa na kumbukumbu aliyoitoa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amaan Abeid Karume kuhusu mahojiano ya mwandishi David Martin na Hayati Abeid Karume mwaka 1965. Ilihusu mtazamo wa Mzee Abeid Karume kwenye demokrasia.
Dr Amaan Karume amesimulia vema kabisa, na hakika, amenikumbusha mahojiano yaliyofanywa na Mwandishi David Martin na Ben Mkapa mwaka 1995 hata kabla Mkapa hajaingia madarakani. Mwandishi huyu, Marehemu David Martin, ni mmoja wa wanahabari mahiri kabisa kupata kutokea na kufanya kazi kufuatilia siasa za Afrika.
Nina bahati ya kusoma mahojiano kadhaa aliyoyafanya David Martin kwa viongozi wakuu wa Afrika. Huenda si wengi mliosoma mahojiano hayo aliyofanya David Martin kwa Ben Mkapa.
Nitapenda hapa kurejea sehemu ya mahojiano hayo ambapo David Martin alimuuliza Ben Mkapa juu ya visheni yake kwa Tanzania endapo angechaguliwa kuwa Rais mwaka 1995.
Mwandishi mahiri marehemu David Martin aliuliza;
" Bwana Benjamin Mkapa, mwisho, ukiangalia mbele miaka mitano au labda kumi, ungependa historia ikukumbuke kwa namna gani?"
Mkapa anajibu;
"Ningependa nikumbukwe kama mtu niliyeongoza Utawala ambao kwa vitendo umepiga vita rushwa na umeimarisha aina ya uongozi, utumishi wa umma, thamani na wajibu uliokuza Utawala Bora. Kwamba katika utawala wangu nimeongoza juhudi za kuimarisha nidhamu katika mchakato wa utawala, nidhamu kwa maana ya sheria, kanuni na taratibu, lakini ndani yake zikiwa na misingi ya uhuru.
Hivyo basi, kukuza misingi ya huru na maendeleo ya haraka, lakini katika mtazamo wa sheria na taratibu, hivyo basi nidhamu.
Kwamba nimehamasisha ajenda ya vyama vyingi, mfumo wa vyama vingi, bila kuharibu. Lakini zaidi kwa dhamira ya wazi ya kujenga utaifa katika Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania. Nitatumaini itasemwa, kuwa nimejaribu kwa bidii zangu zote kufikia matokeo hayo bila kujidai ambako mara nyingi kiujumla uhusishwa na ofisi kuu ya nchi, lakini zaidi, kinyume chake, kuyafanya hayo kwa heshima na unyenyekevu mkubwa."- Benjamin Mkapa, mahojiano na David Martin, 1995.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni