Baraza Kuu la
Chama Cha Wananchi (CUF), leo linatarajia kutangaza uamuzi mzito
kutokana na kikao cha Kamati ya Utendaji, kilichofanyika jana jijini Dar
es Salaam chini ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kikao hicho cha
Kamati ya Utendaji kilifanyika kwa saa tatu kujadili suala la tarehe
iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya kurudia uchaguzi wa
Zanzibar, uliofutwa Oktoba 28, mwaka jana.
Kamati hiyo
ambayo ilikuwa na ajenda moja pekee, ilijadili na kutoa uamuzi mzito
ambayo yatawasilishwa kwenye Baraza Kuu leo na kutolewa kwa umma.
Mmoja
wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambaye hakutaka kutajwa jina ,
alisema kuwa maazimio yaliyotolewa na kikao hicho kilichoanza saa nne
asubuhi, yataishangaza dunia.
Alisema uchaguzi
uliotangazwa na ZEC kuwa utafanyika Machi 20, mwaka huu, ni batili kwa
kuwa tayari mshindi wa uchaguzi huo anafahamika ni Maalim Seif.
“Jukumu kubwa la
kikao cha Kamati Tendaji kwa mujibu wa Katiba (ya CUF) ni kuandaa
ajenda kwa ajili ya kikao cha Baraza Kuu litakaloanza kesho (leo) na
baada ya hapo tutatangaza msimamo wetu juu ya uchaguzi huo,” kilieleza
chanzo hicho.
Kwa mujibu wa
Ofisa Habari wa CUF, Silas Bwire, Kamati ya Utendaji ilikuwa na wajumbe
18 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambao ni viongozi waandamizi wa
chama.
Baraza kuu ambalo linatarajia kufanya kikao chake leo, litakalopokea ajenda zilizojadiliwa jana, lina wajumbe 60.
Kikao cha Baraza
ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Tasilima, kitajadili
kwa kina ajenda zitakazowasilishwa pamoja na kuzitolea uamuzi.
Wakati hatima ya
CUF kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio inatarajia kufahamika
leo, mgawanyiko mkubwa umeibuka miongoni mwa wajumbe wake wa Baraza Kuu
la Uongozi Taifa.
Katika mgawanyiko huo, wamo wanaopinga kushiriki huku wengine wakitaka chama kuangalia upya msimamo wa kususia uchaguzi huo.
Akizungumzia
mgawanyiko huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu,
alisema kutokana na ukubwa na uzito wa mgogoro wa uchaguzi, mgawanyiko
ni jambo ambalo halikwepeki kwa chama kikubwa kama hicho.
Alisema uongozi
wa chama uko makini katika kujadili ajenda ya mgogoro wa uchaguzi na
kuwataka viongozi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa na
moyo wa subira wakati Baraza Kuu la Uongozi la Chama linajiandaa kutoa
kauli ya mwisho juu ya hatima ya uchaguzi huo.
Jussa alisema
uamuzi utakaotolewa na Baraza Kuu ndio utakuwa mwongozo kwa wagombea
wote wa chama pamoja na wanachama na watu wanaokiunga mkono chama.
Alisema mchezo
aliyoufanya Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi kwa manufaa ya CCM,
haukubaliki katika misingi ya demokrasia na utawala bora.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni