KULINGANA na Hazina ya Umoja wa
Mataifa ya Idadi ya Watu, zaidi ya wanawake nusu milioni hufa kila mwaka
kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba. Isitoshe, Shirika la Umoja
wa Mataifa la Hazina ya Watoto linasema kwamba kila mwaka zaidi ya
wanawake milioni 60 huugua vibaya wakiwa wajawazito hivi kwamba karibu
thuluthi moja kati yao hupata majeraha au maambukizo yanayodumu maisha
yote. Katika nchi zinazoendelea, wanawake wengi hupata mimba moja baada
ya nyingine, hujifungua, na kujiachilia, jambo ambalo huwafanya wawe
wachovu na wagonjwa. Naam, mimba inaweza kuleta madhara—hata kuhatarisha
uhai. Je, mwanamke anaweza kufanya nini ili mimba yake iwe salama
zaidi?
Utunzaji wa Kiafya Kabla ya Kuwa Mjamzito
Kupanga. Huenda
waume na wake wakahitaji kuzungumza kuhusu idadi ya watoto ambao
watapata. Katika nchi zinazoendelea, ni kawaida kuwaona wanawake wenye
watoto wanaonyonya wakiwa wajawazito. Kwa kupanga vizuri na kutumia
ufikirio unaweza kuruhusu wakati upite kabla ya mtoto mwingine kuzaliwa,
hivyo kumpa mama nafasi ya kurudia hali yake ya kawaida. Jambo hilo pia
litamruhusu apate nafuu baada ya kujifungua.
Ulaji. Kulingana
na Muungano wa Matokeo Bora ya Uzazi, mwanamke anahitaji angalau miezi
minne kabla ya kuwa na mimba baada ya kufanya kazi karibu na bidhaa
zinazodhuru, ili pia apate kuwa na afya bora. Kwa mfano, hatari ya
kupinda uti wa mgongo inayoletwa na kutoziba kwa mrija wa neva wa kitoto
kilicho tumboni, inaweza kuzuiwa iwapo mama mjamzito ana kiasi cha
kutosha cha aina fulani ya vitamini ya C. Kwa kuwa mrija huo
huziba siku ya 24 hadi ya 28 baada ya mimba kutungwa—muda mrefu kabla ya
wanawake wengi kugundua wana mimba—baadhi ya wanawake wanaopanga kupata
mimba hula vyakula vyenye vitamini hiyo.
Chuma ni madini muhimu pia. Kwa
hakika, mwanamke huhitaji madini mengi zaidi ya chuma anapokuwa
mjamzito. Asipokuwa na kiasi cha kutosha—hali ambayo huwapata wanawake
wengi katika nchi zinazoendelea—damu yake inaweza kuwa na upungufu wa
madini hayo. Hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi mwanamke apatapo mimba
moja baada ya nyingine, kwa kuwa hana nafasi ya kurudisha kiasi
kinachohitajika cha madini ya chuma.*
Umri. Wasichana
wenye umri wa chini ya miaka 16 ambao ni wajawazito wanakabili hatari
ya kufa ya asilimia 60 zaidi kuliko wale walio na umri wa miaka 20 na
kitu. Kwa upande mwingine, wanawake wenye umri unaozidi miaka 35 wana
uwezekano mkubwa zaidi wa kuzaa watoto wenye kasoro, kama vile ugonjwa
wa Down. Akina mama wachanga sana au wenye umri mkubwa wanaweza kuugua ugonjwa wa preeclampsia. Ugonjwa
huo, ambao dalili zake zinatia ndani shinikizo la juu la damu baada ya
juma la 20 la mimba pamoja na kuwa na umajimaji usio wa kawaida kwenye
viungo na ongezeko la protini kwenye mkojo, huongeza hatari ya mtoto na
mama kufa.
Maambukizo. Maambukizo
ya mfumo wa mkojo, mlango wa kizazi na sehemu ya siri, na mfumo wa
chakula yanaweza kuzidi wakati wa mimba na kuongeza uwezekano wa kuugua
ugonjwa wa preeclampsia na mtoto kuzaliwa kabla ya wakati. Inafaa maambukizo yoyote yatibiwe kabla ya mwanamke kuwa mjamzito.
Utunzaji wa Kiafya Akiwa Mjamzito
Utunzaji kabla ya kujifungua. Mwanamke
anaweza kupunguza hatari ya kufa akiendelea kumwona daktari mara kwa
mara anapokuwa mjamzito. Hata katika nchi ambako haiwezekani kutembelea
kliniki na hospitali kwa ukawaida, wakunga waliozoezwa vizuri wanaweza
kupatikana.
Utunzaji wa kabla ya kujifungua
unaweza kuwasaidia wataalamu kuona hali ambazo huenda zikahitaji
utunzaji wa pekee. Hali hizo zinatia ndani kuwepo kwa watoto zaidi ya
mmoja tumboni, shinikizo la juu la damu, matatizo ya moyo na figo, na
ugonjwa wa sukari. Katika nchi fulani, mwanamke mjamzito anaweza kupewa
chanjo ya pepo-punda ili kumkinga na ugonjwa huo wakati wa kujifungua.
Anaweza pia kupimwa kama ana bakteria za kundi la B streptococcus kwenye juma la 26 hadi la 28 la mimba. Bakteria hizo zinaweza kuambukiza mtoto wakati wa kuzaliwa, zikiwa kwenye utumbo mkubwa.
Mwanamke anapaswa kuwapatia
wataalamu wa afya habari nyingi iwezekanavyo, kutia ndani rekodi yake ya
tiba. Pia, anapaswa kuuliza maswali kwa uhuru. Anapaswa kuomba msaada
wa kitiba mara moja ikiwa damu inatoka kupitia sehemu ya siri, uso wake
unafura ghafula, ana maumivu makali yenye kuendelea kichwani au uchungu
kwenye vidole, apoteza uwezo wake wa kuona ghafula au haoni vizuri,
anaumwa na tumbo sana, anatapika sana, anaugua homa, mtoto aliye tumboni
anaruka isivyo kawaida, umajimaji unatoka kupitia sehemu ya siri,
anasikia maumivu anapokojoa, au hapati mkojo kama kawaida.
Pombe na dawa za kulevya. Mama
anayekunywa pombe na kutumia dawa za kulevya (kutia ndani tumbaku)
huzidisha hatari ya kumzaa mtoto aliye na akili punguani, mlemavu, na
hata aliye na tabia yenye kasoro. Inajulikana kuwa watoto waliozaliwa na
wazazi ambao wamezoea kutumia dawa za kulevya huwa na matatizo kama ya
watu ambao walitumia dawa za kulevya zamani. Ingawa wengine hudai eti
kunywa pombe kidogo hakuwezi kudhuru, mara nyingi wataalamu hupendekeza
akina mama wajawazito wasiinywe hata kidogo. Wanapaswa pia kuepuka moshi
wa sigara.
Dawa. Hakuna
dawa zinazopaswa kutumiwa ila tu zile zilizopendekezwa na daktari
anayejua kuhusu mimba hiyo na ambaye amechunguza athari zake. Vitamini
fulani pia zinaweza kudhuru. Kwa mfano, kiasi kikubwa sana cha vitamini
ya A chaweza kumlemaza mtoto aliye tumboni.
Kuongeza uzito. Mwanamke mjamzito anapaswa kuepuka kupita kiasi katika ulaji. Kulingana na kichapo Krause’s Food, Nutrition and Diet Therapy, mtoto
anayezaliwa akiwa na uzito wa chini sana anakabili hatari ya kufa
mara 40 zaidi kuliko yule aliyezaliwa akiwa na uzito wa kawaida. Kwa
upande mwingine, kula chakula cha watu wawili hunenepesha tu. Ongezeko
linalofaa la uzito—ambalo huanza kuonekana katika mwezi wa nne wa mimba
na kuendelea—huonyesha kwamba mama anakula chakula cha kutosheleza
mahitaji yake yanayoongezeka.*
Usafi na mambo mengine. Kuoga
kwenye karai na kutumia maji ya bomba kunaweza kufanywa kama kawaida,
lakini haifai kuingiza maji kwa nguvu kupitia sehemu ya siri. Mwanamke
mjamzito anapaswa kuepuka kumkaribia yeyote mwenye ugonjwa wa virusi, kama surua ya rubella. Zaidi
ya hayo, ili kuzuia ugonjwa unaoambukiza ubongo na uti wa mgongo hasa
katika mtoto mchanga, ni lazima awe mwangalifu asile nyama ambayo
haijaiva vizuri wala kugusa kinyesi cha paka. Ni muhimu kudumisha usafi
wa kawaida kama kunawa mikono na kuosha vyakula kabla havijapikwa. Mara
nyingi kufanya ngono hakuleti tatizo lolote, ila tu katika majuma ya
mwisho-mwisho ya mimba au kukiwa na mtiririko wa damu, maumivu tumboni,
au ikiwa mimba ya awali ilitoka.
Kujifungua kwa Mafanikio
Yaelekea mwanamke mjamzito
anayejitunza hatapata matatizo wakati wa kujifungua. Kwa kawaida, yeye
atapanga kama atapenda kujifungulia nyumbani au hospitalini. Atafahamu
vizuri zaidi mambo yatakayotukia na jinsi ya kushirikiana na mkunga au
daktari. Huyo naye atafahamu mapendezi ya mwanamke huyo yanayotegemea
ujuzi aliopata—mahali ambapo anaweza kuchagua—jinsi atakavyokaa
anapojifungua, kupasua ili kumtoa mtoto, na utumizi wa vifaa vya kumvuta
mtoto, dawa za kupunguza maumivu, na kuchunguza mtoto kwa kutumia mbinu
za elektroni. Pia ni lazima wakubaliane kuhusu mambo mengine: je, ni
hospitali au kliniki gani atakayopelekwa iwapo hataweza kujifungulia
nyumbani? Ni hatua gani itakayochukuliwa iwapo atapoteza damu nyingi?
Kwa kuwa wanawake wengi hufa wanapojifungua kwa sababu ya kupoteza damu
nyingi, ni lazima kuwe na vitu ambavyo huongeza kiasi cha damu kwa wale
ambao hawakubali kutiwa damu mishipani. Pia, ni lazima wafikirie kimbele
kuhusu upasuaji wa kutoa mtoto iwapo utahitajika.
Aina hiyo ya
vitamini ya C na madini ya chuma yaweza kupatikana katika maini,
maharagwe, mboga zenye majani mabichi, njugu, na nafaka zilizoongezwa
vitamini na madini mbalimbali. Kuchanganya chakula chenye vitamini ya C,
kama matunda yaliyotoka shambani karibuni, pamoja na chakula chenye
madini ya chuma huongeza madini hayo mwilini.
Ongezeko linalopendekezwa kwa mwanamke mwenye uzito unaofaa anapokuwa
na mimba ni kilogramu 9 hadi 12 kufikia wakati wa kujifungua. Hata
hivyo, wasichana au wanawake ambao hawakuwa wakila chakula cha kutosha
wanapaswa kuongeza kati ya kilogramu 12 hadi 15, na wale wanene
wanapaswa kuongeza kilogramu 7 hadi 9 tu.
MADOKEZO YA KUWASAIDIA WANAWAKE WAJAWAZITO
● Kila siku mwanamke mjamzito
anahitaji kula matunda, mboga (hasa zilizo na majani ya rangi nzito ya
kijani, na zenye rangi ya machungwa, au nyekundu), maharagwe mbalimbali
(kutia ndani soya, dengu, na njegere), nafaka (kutia ndani ngano,
mahindi na shayiri—hasa zile ambazo hazijatolewa maganda au zilizotiwa
vitu vingine), chakula kinachotokana na wanyama (samaki, nyama ya kuku,
nyama ya ng’ombe, mayai, jibini, na maziwa, hasa yale ambayo yametolewa
mafuta). Mafuta, sukari na chumvi vinapaswa kutumiwa kwa kiasi. Kunywa
maji mengi. Epuka vinywaji vyenye kafeini, na vyakula vilivyotiwa dawa
za kuhifadhi na kemikali nyinginezo (kama za kutia rangi na ladha).
Wanga, udongo wa mfinyanzi, na vitu vingine visivyoliwa vyaweza
kusababisha utapiamlo na kumtia sumu.
● Jihadhari na hatari ya mambo
yanayochafua mazingira, kama minururisho ya eksirei na kemikali hatari.
Punguza utumizi wa dawa za kupulizia na dawa nyingine za nyumbani.
Usijipashe joto kupita kiasi kwa kukaa mahali penye joto sana au kwa
kufanya mazoezi sana. Epuka kusimama kwa muda mrefu na kujikaza kupita
kiasi. Funga mkanda wa usalama vizuri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni