.

.

30 Machi 2016

MAKAMPUNI YANAYO HUDUMU BANDARINI KUHAKIKIWA


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amemuagiza Kaimu Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Nelson Mlali kufanya uhakiki wa kampuni zinazotoa huduma mbalimbali bandarini ili kuboresha utendaji kazi na kuepuka mgongano wa maslahi binafsi minongoni wa watumishi wa bandari.
Profesa Mbarawa alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza jana jioni(29/03/2016) kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) eneo la kupakulia mafuta yanayoingia nchini (KOJ) Kurasini.
“Mtafanyaje kazi na mtu ambaye ni mfanyakazi na huku kampuni yake inatoa huduma bandarini, hamuoni kutakuwa na mgongano wa kimaslahi binafsi,” alihoji Profesa Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka Kaimu Meneja Msaidizi Mlali azingatie umiliki wa makampuni kulingana na taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Kampuni nchini (BRELA) katika zoezi la kuhakiki kampuni hizo.
Akiwa eneo la (KOJ) Kurasini, Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa TPA wabadilike na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa badala ya kufanya kazi kwa mazoea ili kuboresha kuongeza ufanisi na kuliongezea taifa mapato kwa manufaa ya wananchi.
Prof. Mbarawa amewaagiza pia Mamlaka ya Bandari wanaponunua vipuri na vifaa mbalimbali vinavyohitajika bandarini hapo wazingatie vipimo sahihi kulingana na vifaa vinavyohitajika kuendeshea mitambo mbalimbali ili kulipunguzia taifa gharama zisizohitajika.
Mamlaka ya Bandari nchini ina bandari mbalimbali zilizopo katika ukanda wa bahari ya Hindi na maziwa yaliyopo nchini.
Ukanda wa Bahari ya Hindi una bandari ya kuu za Dar es salaam, Tanga na Mtwara pamoja na Bandari ndogo zilizopo Lindi, Kilwa Masoko, Mafia, Bagamoyo, Pangani na Kwale.
Bandari nyingine ziliozo katika maziwa mbalimbali nchini ni pamoja na Ziwa Victoria lenye bandari ya Mwanza, Bukoba, Kemondo, Musoma na Nansio, Ziwa Tanganyika likihusisha bandari ya Kigoma na Kasanga wakati Ziwa Nyasa kuna bandari ya Itungi, Manda, Liuli na Mbaba Bay.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni