.
MFANYABIASHARA
maarufu wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Mathias Manga amepigwa risasi
nyumbani kwake juzi usiku na watu wasiojulikana. Polisi imethibitisha tukio na
kwamba majeruhi anaendelea vizuri na matibabu.
Akizungumza
na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas alikiri
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Manga amepigwa risasi ubavuni saa 4.45
usiku nyumbani kwake Ngarenaro alipokuwa anarejea katika shughuli zake.
Sabas
alisema kwa mujibu wa maelezo ya Manga aliyeongea nao kwa njia ya simu alisema
kuwa wakati anarudi nyumbani kwake Ngarenaro kulikuwa na gari aina ya Toyota
Landcruiser Vx ambayo haikuitambua namba ilikuwa ikimfuatilia nyuma kwa muda
mrefu.
Alisema
mara baada ya kufunguliwa mlango wa geti wa nyumbani kwake watuhumiwa hao
waliingia kupitia geti dogo lililokuwa wazi mpaka ndani na kuanza kumshambulia
kwa risasi.
Kamanda
Sabas alisema katika kujiokoa Manga alitoa bastola yake na kuanza kupambana nao
kisha majambazi hao kukimbia wakimwacha akiwa amejeruhiwa kwenye mbavu.
Alisema
Manga alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu
na aliruhusiwa usiku huo huo na kurudi nyumbani kwake kwa kuwa hali yake
haikuwa mbaya sana.
‘’Manga
amepigwa risasi ya kuparazwa ya ubavuni lakini hali yake inaendelea vema sana
na yuko nyumbani kwake amepumzika”, alisema. Sabas alisema polisi inafanya
uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote waliohusika ili
hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Tukio
hilo limeonesha kusikitisha baadhi ya wafanyabiashara wa madini Jijini Arusha
na kusema kuwa polisi inapaswa kulifanyia kazi tukio hilo ili wahusika waweze
kuchukuliwa hatua kali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni