Dodoma. Harakati za wagombea urais wa Jamhuri
ya Muungano kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana zilihamia katika ukumbi wa
Bunge ambapo kila mmoja wao alikuwa akitafuta mbinu za kusalimiana na wabunge.
Hata hivyo baadhi ya wagombea hao walikuwa
wanatumia nafasi hiyo kuzunguka na kuwafuata wabunge kwenye viti vyao, kiasi
cha kufanya kuwepo na kile Spika alichokita kama ni vurugu ndani ya Bunge.
Spika Anne Makinda alilalamika mara kadhaa
kuwa wabunge walikuwa wakifanya vurugu ndani ya ukumbi na kuwataka watulie,
kwani wengi walikuwa wanapishana kwenye viti vya wagombea akiwamo Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ambaye kiti chake kilipata wageni
wengi pia.
“Waheshimiwa wabunge naombeni utulivu basi,
mbona mnaleta vurugu kwa kutembea tembea humu ndani wakati kanuni hazisemi
hivyo, nitawataja kwa majina sasa,” alisema Makinda.
Karibu wagombea wote ambao ni wabunge, naibu
mawaziri na mawaziri jana walikuwa bungeni isipokuwa wagombea watatu wa CCM ambao
ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala
na Mbunge wa Kisesa, Luhwaga Mpina ndiyo hawakuonekana.
Mapema mgombea urais, Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuvunja mwiko baada ya kuhama katika
kiti chake anachotumia kila siku na kumfuata mgombea mwenzake Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na wawili hao walitumia muda mrefu
wakizungumza pamoja.
Kutoka hapo, Mwigulu alianza kuzunguka kwa
staili yake kwa kwenda kwa wabunge huku akiwa makini kwa kukwepa viti
walivyokaa wagombea wenzake, ambao wakati wote nao walikuwa na wabunge karibu
yao wakizungumza.
Wagombea wengine waliokaa pamoja kwa muda
mrefu ndani ya ukumbi ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda baada ya Magufuli kumfuata Pinda katika kiti chake.
Mgombea mwingine ambaye jana alionekana
kutotulia katika kiti chake alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Kazi
Maalumu, Profesa Mark Mwandosya.(VICTOR)
Profesa Mwandosya huwa hana tabia ya kuhama
kiti chake na kuwafuata wabunge au mawaziri na badala yake hufuatwa alipo,
lakini jana hali ilikuwa tofauti.
Profesa Mwandosya alisalimiana na watu wengi
ndani na nje ya ukumbi wa Bunge, ambako alikutana na wabunge kadhaa wa Mkoa wa
Mbeya akiwemo mgombea mwenzake ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe na waliteta kwa muda.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa zamani Edward
Lowassa wabunge wengi kufika kumsalimia anapokaa na haikuwa jambo geni jana,
kwani ni kawaida yake awapo ukumbini mara nyingi hukosa nafasi ya kupumua
kutokana na msururu wa wabunge.Hata hivyo, katika kiti ambacho wabunge
hukitumia kuzungumza naye, jana kilitumika zaidi na Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM), Juma Sadifa ambaye alikaa kwa muda mrefu zaidi wakiteta
na alionekana kama ameziba nafasi ya wengine.
Nje ya ukumbi wa Bunge, Dk Magufuli na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe waliongoza kupata
watu wengi waliokuwa wakiweka msururu kuwasalimia.
Idadi kama hiyo pia ilikuwa kwa Pinda, ambaye
licha ya kuwa na ulinzi, lakini nje ya ukumbi jana alisalimiana na watu wengi
tofauti na siku zote.
Hata hivyo Pinda tofauti na siku zote jana
alikuwa na staili tofauti kwani kila aliyemhisi kuwa alitaka kumpa walau mkono,
alimfuata yeye na kusalimiana jambo lililowapa wakati mgumu walinzi wake
kumzuia.
Mgombea pekee ambaye alikuwa na staili ya
kwake katika salamu alikuwa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba ambaye toka ndani hadi nje alisalimia na watu
wachache kwa kushikana mikono huku akionekana kuwapungia mikono zaidi.
CHANZO:MWANANCHI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni