.

.

24 Februari 2016

LIPUMBA: RAIS MAGUFULI ATANGAZE MSHAHARA WAKE TZ




Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais John Pombe Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake, kwa kile alichokisema kuwa ni rais huyo kujivisha joho la kuwa rais wa wanyonge.
Profesa Lipumba amesema Rais Magufuli aliyejiarifisha kama kiongozi anayeguswa sana na matatizo ya wanyonge, asiyependa makuu, anayehimiza ukusanyaji wa mapato ya serikali na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za umma, anatakiwa kuweka wazi mshahara wake ili Watanzania waamini anayoyasema. Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi, amekumbushia mjadala kuhusu mshahara wa rais, ikiwemo ule uliowahi kuibuliwa mwaka 2013 na Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma mjini, wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kuwa rais alikuwa analipwa Shilingi milioni 32 kwa mwezi wakati huo. Lipumba amemtaka Rais Magufuli atangaze mshahara wake na kwamba, ikiwa mapato yake ni kiasi hicho cha milioni 32 kwa mwezi, basi atoe lau nusu ya kiasi hicho na kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Ameongeza kuwa, hatua hiyo itaimarisha taswira inayojengeka barani Afrika kuwa yeye ni rais wa wanyonge. Itakumbukwa kuwa katika mazungumzo yake na wazee wa jiji la Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais John Pombe Magufuli aliwataka mawaziri, manaibu waziri na makatibu wakuu kuchangia Shilingi milioni moja katika mishahara yao kwa ajili ya elimu. Aidha aliongeza kuwa, yeye mwenyewe, makamu wake na waziri mkuu watachangia kila mmoja Shilingi milioni sita, ili zifikie milioni 100, kwa ajili ya kusaidia changamoto za elimu bure mkoani Dar es Salaam. Profesa Lipumba amesisitiza kuwa, mishahara na marupurupu ya viongozi wa Tanzania hayako wazi na kwamba Watanzania hawajui kila mwezi rais, makamu wa rais, viongozi wakuu wa serikali na wabunge wanalipwa kiasi gani, jambo ambalo limekuwa likiibua shaka miongoni mwa Watanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni