.

.

10 Februari 2016

VYAMA 9 VYASUSIA UCHAGUZI ZANZIBAR


Vyama tisa vya siasa kati ya 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar mwaka jana, vimeungana na Chama cha Wananchi (CUF) kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika hapo Machi 20, hadi utakapopatikana mwafaka wa kumaliza mgogoro wa kisiasa.
Kassim Bakari Ali, mratibu wa umoja wa vyama hivyo, alinukuliwa jana akisema kuwa, vyama hivyo vilikutana Unguja na kupitisha maazimio mawili ya pamoja ya kutoshiriki uchaguzi huo. Kwa mujibu wa Bakari Ali, vyama hivyo ni pamoja na UMD, Jahazi Asilia, Chaumma, UPDP, DP, CCK na ACT-Wazalendo. Ushiriki wa vyama vya ADC na CCK bado una utata kutokana na wagombea wake kutangaza kushiriki licha ya vyama vyao kuwa na msimamo tofauti, hali iliyosababisha wagombea hao kusimamishwa. Vyama ambavyo hadi sasa vimetangaza azma ya kushiriki marudio hayo ni pamoja na CCM, Tadea, TLP, Sau na AFP. Kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, Zanzibar imeendelea kushuhudia mgogoro wa kisiasa kati ya vyama vikubwa vinavyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya chama cha Wananchi CUF kususia marudio ya uchaguzi kufuatia ule wa awali kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. Akitaja maazimio ya vyama hivyo, Kassim alisema wamekubaliana kutoshiriki marudio ya uchaguzi huo hadi mgogoro wa CCM na CUF utakapomalizika na kwamba tayari wameunda kamati ya wajumbe 18 ya wenyeviti na makatibu wa kila chama ili kuanzisha meza ya kutafuta suluhu ya mvutano uliopo kati ya vyama hivyo viwili vyenye ushawishi. Kwa mujibu wa Bwana Ali ambaye pia ni mwenyekiti wa Jahazi Asilia, mgogoro wa Zanzibar utamalizwa na Wazanzibari wenyewe, na kwamba ni vyema viongozi hao wa kisiasa wajenge uvumilivu katika kutafuta mwafaka wa kisiasa baina yao.
Amesema tatizo la vyama hivyo siyo kushiriki marudio ya uchaguzi huo tu bali ni kuangalia chanzo na hatima ya mgogoro huo kwa masilahi ya Wazanzibari wote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni