.

.

10 Februari 2016

WANIGERIA WAANDAMANA KUPINGA BEI MPYA YA UMEME


Maelfu ya raia wa Nigeria wamefanya maandamano kulalamikia hatua ya serikali kupandisha bei za bidhaa muhimu nchini humo. Maandamano hayo yaliyofanyika mjini Abuja, yaliitishwa kulalamikia ongezeko la gharama za umeme na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuangalia kipato cha raia wake badala ya kupandisha gharama za nishati hiyo muhimu.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 45, hatua ambayo imetajwa na wapinzani kuwa iliyo dhidi ya watu masikini na kushindwa viongozi kukabiliana na ufisadi uliokithiri ndani ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Katika maandamano hayo wananchi hao sanjari na kubeba maberamu na mabango yenye jumbe mbalimbali dhidi ya serikali, wamemtaka Rais Buhari kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi uliomuingiza madarakani. Aidha waandamanaji wametaka pia rais huyo kukabiliana na ufisadi, kupunguza hali mbaya ya uchumi na pia kulitokomeza kundi la kigaidi la Boko Haram. Hii ni mara ya kwanza kwa wananchi wa matabaka mbalimbali kumiminika mabarabarani kupinga uongozi wa Rais Buhari, tangu rais huyo alipoingia madarakani kwa ahadi nyingi alizozitoa. Kabla ya hapo Waislamu walifanya maandamano makubwa katika miji kadhaa ya nchi hiyo kulaani kitendo cha askari wa serikali kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa mji wa Zaria, ambapo watu 1000 wanatajwa kuuawa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni