Taarifa kutoka Pretoria Afrika Kusini zinaeleza kuwa, bunge la
Afrika Kusini limepinga ombi la wabunge wa upinzani waliotaka Rais Zuma
apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye. Ombi hilo lilijadiliwa baada ya
Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini kumtuhumu Rais wa Afrika Kusini kuwa
amekiuka katiba.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Lechesa Tsenoli Naibu Spika wa bunge la
Afrika Kusini alitangaza Jumanne wikii hii kuwa mpango wa kumpigia Rais
Zuma kura ya kutokuwa na imani umeshindwa kuidhinishwa kwa kura nyingi
za wabunge baada ya wabunge wa Afrika Kusini kupiga kura 233 za hapana
na kura 143 za ndio.
Hii ni katika hali ambayo Congresi ya Taifa ya Afrika Kusini yaani
chama tawala ambacho kinamuunga mkono rasmi Rais Jacob Zuma kimestafidi
na wingi wa viti ilivyonavyo bungeni kutokana na theluthi mbili ya kura
za hapana zilizopigwa na hivyo kuzuia kura hiyo ya kutokuwa na imani
dhidi ya Rais Zuma.
Chama cha Democratic Alliance kiliwasilisha mpango wa kumpigia kura
ya kutokuwa na imani Rais Jacob Zuma kufuatia uamuzi wa Mahakama ya
Katiba wiki iliyopita.
Hata kama Zuma tangu huko nyuma anatuhumiwa kwa ufisadi wa fedha za
umma huku Afrika Kusini pia ikiwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa
ufisadi wa fedha, lakini makelele ya hivi sasa yalianza mara baada ya
mahakama ya katiba ya Afrika Kusini kueleza kuwa, Jacob Zuma amekiuka
katiba ya nchi hiyo kwa kukataa kurejesha dola milioni 16 fedha za
serikali alizotumia kukarabati nyumba yake binafsi.
Mahakama kuu ya Afrika Kusini Alhamisi iliyopita ilitangaza kuwa Rais
Zuma ameshindwa kutekeleza na kulinda katiba ya nchi hiyo. Rais Zuma
amesema atarejesha serikalini fedha hizo alizotumia kwa matumizi
binafsi. Zuma ametamka wazi kuwa hakukiuka katiba kwa makusudi.
Rais wa Afrika Kusini vile vile amewaomba radhi wananchi na serikali
na kuvitaka pia vyama vyote vya kisiasa nchini kuheshimu katiba.
Mwaka 2014 Jacob Zuma alitumia karibu Rand za Afrika kusini milioni
216 sawa na dola milioni 24 kutoka hazina ya serikali kwa ajili ya
kukarabati makazi yake binafsi.
Kufuatia hukumu hiyo ya mahakama, chama kikuu cha upinzani nchini
Afrika Kusini kilitangaza bungeni kuwa, kitafanya kila linalowezekana
ili kumuuzulu Rais Zuma iwapo bunge litashindwa kuchukua hatua katika
uwanja huo.
Wawakilishi wa chama cha upinzani cha muungano wa upinzani wa
Democratic Alliance katika bunge la Afrika Kusini awali walitangaza
kuwa wameuweka katika ajenda ya kazi mpango wa kupiga kura ya kutokuwa
na imani na utendaji wa kisiasa wa Rais Zuma.
Mbali na mpango huo, mpango mwingine pia unatarajiwa kuwasilishwa
bungeni hivi karibuni kuhusu tuhuma mpya za ufisadi zinazomkabili Rais
Zuma.
Kufuatia hukumu ya mahakama ya Afrika Kusini, Ahmed Kathrada
mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi na mmoja wa shakhsia waliokuwa
karibu wa marehemu Nelson Mandela, rais wa zamani wa Afrika Kusini pia
amemuandikia barua Rais Jacob Zuma akimtaka ajiuzulu. Kathrada ameongeza
kuwa, kujiuzulu Zuma kutaisaidia serikali kuondokana na mgogoro wa
kukabiliwa na upinzani.
Kabla ya hapo, Rais wa Afrika Kusini aliahidi kupambana na ufisadi
slakini hadi sasa hajachukua hatua yoyote katika uga huo, huku mgogoro
wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo ukizidi kupanuka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni