Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
na mwenyeji wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni jijini Kampala
mara baada ya kumalizika kwa sherehe za uapisho wa Rais Museveni.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru
mwenyeji wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni jijini Kampala mara
baada ya kumaliza mazungumzo yao nchini Uganda. PICHA NA IKULU.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
12 Mei, 2016 amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe.
Yoweri Kaguta Museveni muda mfupi baada ya kuhudhuria sherehe ya
kuapishwa kwa Rais huyo iliyofanyika katika uwanja wa Kololo Jijini
Kampala.
Katika
Mazungumzo hayo Rais Magufuli amempongeza Rais Museveni kwa kuapishwa
kuwa Rais wa Uganda kwa kipindi kingine cha miaka 5 na kumhakikishia
kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi Uhusiano, ushirikiano na udugu
wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo.
Viongozi
hao pia wamezungumzia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la
kutoka Hoima (Ziwa Albert) nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini
Tanzania ambapo pamoja na kuishukuru Uganda kwa uamuzi wake wa kuamua
bomba hilo lipitie Tanzania, Rais Magufuli amemshauri Rais Museveni
kufupisha muda wa ujenzi wa mradi huo, kwa kutumia mbinu inayojumuisha
usanifu na ujenzi (Design and Construct method) na kutumia wakandarasi
wengi watakaogawanywa katika vipande tofauti badala ya kutumia
mkandalasi mmoja.
"Nashauri
tutumie mbinu ya usanifu na ujenzi pamoja, hii ni njia ya haraka zaidi,
na pia tugawe vipande vya ujenzi kwa njia yote ya bomba la mafuta yenye
urefu wa kilometa 1,410 tunaweza kuwa na Wakandarasi watano mpaka sita
ambao watatumia njia hiyo mpya ya usanifu na ujenzi.
"Kwa
kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza muda utakaotumika kwa ajili ya
ujenzi wa bomba la mafuta, inaweza hata kuchukua mwaka mmoja tu" Amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo faida za mradi huo wa
mafuta zitaanza kupatikana mapema badala ya kusubiri miaka miwili au
mitatu ijayo, na kwamba hiyo itakuwa inaendana na kauli mbiu yake ya "Hapa Kazi Tu"Pia
Rais Magufuli amemshukuru Rais Museveni kwa uamuzi wa nchi hiyo wa
kuipa Tanzania umiliki wa asilimia 8 katika mradi huo wa bomba la
mafuta.
Kwa
upande wake Rais Museveni amesema amefurahishwa na hatua iliyofikiwa
katika utekelezaji wa mradi huo, na pia amempongeza Rais Magufuli kwa
juhudi zake kubwa ambazo amezifanya katika mapambano dhidi ya rushwa
nchini Tanzania.
"Napenda
kasi yako ya uongozi, napenda jinsi unavyopambana na rushwa, kwa sababu
rushwa ilikuwa inazaa matatizo mengine kama vile ucheleweshaji wa
mizigo bandarini na vikwazo vya mpakani, hivyo nakupongeza sana kwa
hilo" Amesema Rais Museveni.
Katika
sherehe ya kuapishwa kwa Rais Museveni iliyofanyika kabla ya mazungumzo
hayo, pamoja na Rais Magufuli viongozi wengine kutoka Tanzania
waliohudhuria ni Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi,
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa na
Mkewe Mama Salma Kikwete na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU
Kampala
12 Mei, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni