.

.

06 Februari 2016

TAKUKURU WAMTUMBUA AFISA WA UHAMIAJI DAR ES SALAAM


Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Ilala imemkamata afisa wa ofisi ya uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kwa tuhuma ya kuomba shilingi milioni 1 na kupokea Shilingi laki 5 kutoka kwa mfanyabiashara mwenye asili ya Kisomali mnamo tarehe 4 Februari, 2016.
Bw.Kiangwike Ngumba mwenye cheo cha afisa mkaguzi wa uhamiaji alikamatwa baada TAKUKURU kupokea taarifa kutoka kwa Bw.Bille Mohamed kuwa mtuhumiwa na maafisa wengine walifika katika eneo lake la biashara na kuchukua hati ya kusafiria ya ndugu yake kwa madai kuwa wanakwenda kuifanyia ukaguzi. Hata hivyo, baadaye afisa huyo alimtaka mtoa taarifa kutoa kiasi cha shilingi milioni moja kama sharti la kurejesha hati hiyo.
Uchunguzi wa tuhuma hii unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia na kuwachunguza maafisa wengine waliohusika ili wafikishwe mahakamani. Afisa huyo na wenzake wanakabiliwa na tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007.
Tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kuripoti vitendo au viashiria vyovyote vya rushwa dhidi ya watumishi wasio waadilifu katika ofisi za TAKUKURU ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni