Vyama tisa vya
siasa kati ya 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar
mwaka jana, vimeungana na Chama cha Wananchi (CUF) kutoshiriki uchaguzi
wa marudio uliopangwa kufanyika hapo Machi 20, hadi utakapopatikana
mwafaka wa kumaliza mgogoro wa kisiasa.
Kassim Bakari
Ali, mratibu wa umoja wa vyama hivyo, alinukuliwa jana akisema kuwa,
vyama hivyo vilikutana Unguja na kupitisha maazimio mawili ya pamoja ya
kutoshiriki uchaguzi huo. Kwa mujibu wa Bakari Ali, vyama hivyo ni
pamoja na UMD, Jahazi Asilia, Chaumma, UPDP, DP, CCK na ACT-Wazalendo.
Ushiriki wa vyama vya ADC na CCK bado una utata kutokana na wagombea
wake kutangaza kushiriki licha ya vyama vyao kuwa na msimamo tofauti,
hali iliyosababisha wagombea hao kusimamishwa. Vyama ambavyo hadi sasa
vimetangaza azma ya kushiriki marudio hayo ni pamoja na CCM, Tadea, TLP,
Sau na AFP. Kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, Zanzibar imeendelea
kushuhudia mgogoro wa kisiasa kati ya vyama vikubwa vinavyounda
Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya chama cha Wananchi CUF kususia
marudio ya uchaguzi kufuatia ule wa awali kufutwa na Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. Akitaja maazimio ya vyama
hivyo, Kassim alisema wamekubaliana kutoshiriki marudio ya uchaguzi huo
hadi mgogoro wa CCM na CUF utakapomalizika na kwamba tayari wameunda
kamati ya wajumbe 18 ya wenyeviti na makatibu wa kila chama ili
kuanzisha meza ya kutafuta suluhu ya mvutano uliopo kati ya vyama hivyo
viwili vyenye ushawishi. Kwa mujibu wa Bwana Ali ambaye pia ni
mwenyekiti wa Jahazi Asilia, mgogoro wa Zanzibar utamalizwa na
Wazanzibari wenyewe, na kwamba ni vyema viongozi hao wa kisiasa wajenge
uvumilivu katika kutafuta mwafaka wa kisiasa baina yao.
Amesema tatizo
la vyama hivyo siyo kushiriki marudio ya uchaguzi huo tu bali ni
kuangalia chanzo na hatima ya mgogoro huo kwa masilahi ya Wazanzibari
wote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni