Maelfu ya raia
wa Nigeria wamefanya maandamano kulalamikia hatua ya serikali kupandisha
bei za bidhaa muhimu nchini humo. Maandamano hayo yaliyofanyika mjini
Abuja, yaliitishwa kulalamikia ongezeko la gharama za umeme na kuitaka
serikali ya nchi hiyo kuangalia kipato cha raia wake badala ya
kupandisha gharama za nishati hiyo muhimu.
Hatua hiyo
imekuja baada ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari kupandisha gharama za
umeme kwa asilimia 45, hatua ambayo imetajwa na wapinzani kuwa iliyo
dhidi ya watu masikini na kushindwa viongozi kukabiliana na ufisadi
uliokithiri ndani ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Katika
maandamano hayo wananchi hao sanjari na kubeba maberamu na mabango yenye
jumbe mbalimbali dhidi ya serikali, wamemtaka Rais Buhari kutekeleza
ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi uliomuingiza
madarakani. Aidha waandamanaji wametaka pia rais huyo kukabiliana na
ufisadi, kupunguza hali mbaya ya uchumi na pia kulitokomeza kundi la
kigaidi la Boko Haram. Hii ni mara ya kwanza kwa wananchi wa matabaka
mbalimbali kumiminika mabarabarani kupinga uongozi wa Rais Buhari, tangu
rais huyo alipoingia madarakani kwa ahadi nyingi alizozitoa. Kabla ya
hapo Waislamu walifanya maandamano makubwa katika miji kadhaa ya nchi
hiyo kulaani kitendo cha askari wa serikali kufanya mauaji ya umati
dhidi ya Waislamu wa mji wa Zaria, ambapo watu 1000 wanatajwa kuuawa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni