MABOSI wa
mashirika mawili ya Serikali nchini, wanaodaiwa kulipwa mshahara wa Sh
milioni 36, wamekanusha madai hayo, huku wakielezea kushangazwa na
taarifa hizo wakati hata nusu ya fedha hizo, hawapati.
Akizungumza
mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC),
mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, halipwi mshahara huo.
Akijibu hoja za
wajumbe wa kamati hiyo kuhusu taarifa ya utekelezaji na utendaji wa
shirika hilo kwa mwaka 2014/15, Mchechu alisema shirika hilo pamoja na
kutekeleza majukumu yake, bado lina changamoto za uhaba wa fedha.
“Katika ujenzi
wa nyumba zetu, Serikali haigharamii masuala ya miundombinu kama vile
maji, umeme, barabara hilo ni jukumu letu na linatugharimu fedha nyingi.
“Sasa nashangaa wako watu wanasema mimi nalipwa mshahara mkubwa,
sielewi wametoa wapi huo mshahara kwa sababu silipwi mshahara huo, mimi
nalipwa chini ya huo walioutaja,” alisema Mchechu.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(Ewura),Felix Ngamlagosi aliiambia kamati hiyo kwamba mamlaka hiyo ina
changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa watumishi na maslahi duni. Alisema
wakati maslahi ya wafanyakazi ni duni, ameshangaa kusikia vyombo vya
habari vikisema yeye ni miongoni mwa wakurugenzi wanaolipwa Sh milioni
36 kwa mwezi.
“Jamani hapa
tunazungumzia maslahi duni ya watumishi wetu, nashangaa kusikia naambiwa
nalipwa milioni 36, mshahara wangu haufiki hata nusu ya hizo fedha,”
alisema Ngamlagosi. Nyumba nafuu Awali wajumbe wa kamati hiyo baada ya
kupitia taarifa hiyo ya NHC, waliiomba Serikali kuharakisha kuwepo kwa
sera ya nyumba ili kurahisishia mashirika yanayohusika na masuala ya
ujenzi wa nyumba kujenga nyumba za bei nafuu kwa wananchi.
“Yapo malalamiko
kutoka kwa wananchi kwamba NHC mnauza nyumba kwa bei kubwa, huku mkitoa
matangazo kuwa nyumba hizo ni bei nafuu,” alihoji mjumbe wa Kamati
hiyo, Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa. Akijibu hoja hiyo, Mchechu
alisema nyumba zinazojengwa na NHC zinauzwa kuanzia Sh milioni 30 hadi
250 kwa fedha taslimu na kwamba mnunuzi atatakiwa kulipa kodi.
Aliongeza kuwa
kama mnunuzi hatakuwa na fedha taslimu, benki washirika wanatoa mikopo
kwa ajili ya ununuzi wa nyumba hizo, ila wanunuzi watatakiwa kulipa riba
za benki husika. Baada ya majibu hayo, wajumbe hao walitaka Serikali
iangalie jinsi ya kupunguza mzigo kwa shirika hili na ikiwezekana
waondolewe kodi ya uingizaji vifaa vya ujenzi ili kusaidia nyumba hizo
kuuzwa kwa bei nafuu, kwa lengo la kuwanufaisha wananchi hasa wale wa
kima cha chini.
Akizungumzia
hoja hizo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Angelina Mabula alisema shirika hilo, linapaswa kuwasiliana na watendaji
katika maeneo husika ya ujenzi wa nyumba hizo, ili wawasaidie kubeba
gharama ndogondogo.
“Serikali na
wizara zinafanya kazi kwa ushirikiano na NHC, na hili la gharama za
miundombinu, kila halmashauri nchini ambayo ujenzi wa nyumba hizo
unafanywa, inaweza kuangalia jinsi ya kusaidia gharama za miundombinu,
ili nyumba hizo ziuzwe kwa bei nafuu zaidi kwa wananchi,” alisema
Mabula.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni