.

.

02 Mei 2015



MAAFANDE wa Tanzania Prisons ‘Wajelajela’ wameibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya mahasimu wao wa jiji la Mbeya, Mbeya City fc katika mechi ya ligi kuu soka Tanzania bara iliyomalizika jioni hii uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya.
Goli la Prisons limefungwa dakika ya 90’ na Lugano Mwangama kwa mkwaju wa penalti.
Kabla ya mchezo huu kulikuwa na stori nyingi kuwa Mbeya City watawabeba Prisons ili wasishuke daraja, lakini uongozi wa Mbeya City ulikanusha hilo mara kadhaa.
Leo baada ya Prisons kupata penalti katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mashabiki wa Mbeya City walikuwa wanashangilia kuashiria kufurahishwa na tukio, na hata lilipoingia goli walishangilia huku wengine wakipiga ngoma na kutoka nje ya uwanja.
Lakini baada ya dakika 90’ kumalizika, baadhi ya mashabiki wa ukweli wa Mbeya City walikuwa na hasira kutokana na matokeo hayo na walitaka kumvamia kocha mkuu, Juma Mwambusi, lakini aliondoka haraka uwanjani hapo.
Mashabiki hao wanadai kocha huyo amekula njama ya kuwabeba Prisons kama ilivyokuwa ikielezwa siku chache kabla ya mechi.
Hata hivyo timu zote zilicheza kwa nguvu na kutengeneza nafasi, lakini Prisons walijikosa nafasi nyingi za wazi.
Kwa matokeo hayo, Prisons wamefikisha pointi 28 na kupanda kutoka nafasi ya 12 mpaka nafasi ya 8 katika msimamo.
Mbeya City wanaendelea kushika nafasi ya nne wakiwa na pointi 31 ambazo zimewaweka mikono salama ya kubaki ligi kuu na mechi ya mwisho mei 9 mwaka huu wataikaribisha Polisi Morogoro uwanja wa Sokoine.

Prisons watasafiri mpaka CCM Kirumba Mwanza kuchuana na Kagera Sugar na hii inatokana na Stand United kuwa na mchezo mei 9 CCM Kambarage, uwanja ambao Kagera wanautumia kama wa nyumbani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni