.

.

20 Septemba 2015

FAHAMU MAZINGIRA RAFIKI YA KUJISOMEA


Kila kitu kina mazingira yake ya kuweza kukifanya kwa ufanisi ili kutoa matokeo yaliyokusudiwa kwa asilimia kubwa; vivyo hivyo zoezi la kujisomea kwa wanafunzi pia hupaswa kuandaliwa mazingira rafiki ili kufanya ubongo upokee mambo mengi kwa wakati mmoja na hatimaye kuweza kufaulu vizuri katika masomo yao.
Wanafunzi wengi hujisomea bila kujali mazingira ya kufanya hivyo jambo ambalo huwafanya washindwe kufaulu mitihani yao vizuri kwa kuwa ili mwanafunzi aweze kujisomea kwa tija hupaswa kusaidiwa na mazingira rafiki waliyojitengenezea yatakayomfanya awe makini kwenye masomo yake bila umakini wake kutekwa na mambo mengine.
Ukweli ni kwamba wanafunzi wengi siku hizi hujisomea kwa mtindo wa kupitisha macho tu kwa kuwa husoma huku akili zao zikiwa sehemu nyingine kutokana na mambo wanayoyafanya kama vile kutazama televisheni, kusikiliza redio au muziki kupitia simu na kuchati ambapo huwafanya wapoteze umakini wao na hatimaye kufeli masomo yao.
Ifahamike wazi kuwa, kitendo cha kujisomea kwa umakini hakizidi hata dakika 40 kwa kuwa uwezo wa ubongo kupokea mambo ya mrengo mmoja bila kupumzika hudumu kwa wastani huo kwa mwanadamu wa kawaida, ndiyo maana basi hata walimu hushauriwa kufundisha vipindi vya wastani wa dakika 40.

Hivyo ili mwanafunzi anayejisomea aweze kuelewa vizuri na kujenga kumbukumbu thabiti hupaswa kutumia dakika 40 kwa ujumla wake akiwa katika mazingira ya kujisomea la sivyo anaweza asiingize kitu kwa asilimia alizokusudia.
Chagua eneo lisilo na makelele, eneo hili huweza kumfanya mwanafunzi atulize akili yake kwa kiasi kikubwa ambapo huweza kusikia sauti yake ya ndani anayosomea kwa ukubwa bila kuchanganywa na sauti nyingine za nje kama vile redio, simu au televisheni na pengine mawazo binafsi ambazo zote humfanya mwanafunzi asitulize akili yake kwenye jambo moja.

Pili, mazingira ya kujisomea hutakiwa kuwa tulivu yaani yasiyokuwa na pilikapilika zozote za kushtusha kiasi cha kumfanya mwanafunzi anayejisomea kuwa na shauku ya kutazama kitu kinachojitokeza na kupoteza umakini wake.
Ni jambo lililo wazi kuwa katika mazingira yetu ni ngumu kutengeneza mazingira hayo kwa kuwa ndugu na marafiki huweza kuchangia usumbufu na kumpotezea umakini mwanafunzi, hivyo basi ningewashauri wanafunzi kupanga ratiba zao vizuri na kuzingatia muda mzuri ambao usumbufu unakuwa mdogo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni