Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote nchini kuhakikisha
wamesajiliwa na kuwa na vibali vya Baraza kwani kufanya vinginevyo ni
kuvunja sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 iliyolianzisha BASATA
ambayo inamtaka mtu yeyote anayejihusisha na shughuli za Sanaa kuwa
amesajiliwa na kupewa kibali na BASATA.
Aidha,
BASATA linawaagiza Wakuzaji Sanaa wote (Mapromota) wanaoendesha matukio
ya Sanaa kama vile matamasha, mashindano, maonyesho na utoaji tuzo
nchini kuhakikisha wanafanya kazi na Wasanii waliosajiliwa na wenye
vibali vya BASATA na si vinginevyo.
Sambamba
na hili, BASATA linawaagiza wamiliki wote wa studio (Production Houses)
zinazozalisha kazi za Sanaa kuzisajili mara moja na kuhakikisha
zinakuwa na vibali halali vya Baraza la Sanaa la Taifa.
Ieleweke
kwamba kwa mujibu wa sheria hii ya BASATA, Baraza limepewa mamlaka ya
kutoa vibali na kuratibu matukio yote ya Sanaa nchini hivyo kuanzia sasa
Baraza litaanza udhibiti wa matukio haya ya Sanaa hasa katika kuongeza
sharti la kuwataka waandaaji wote wa matukio ya Sanaa kuwataka wasanii
watakaoshiriki matukio yao kuwa wamesajiliwa na kupewa vibali na BASATA.
BASATA
halitavumilia kwa namna yoyote kuona Mkuzaji Sanaa (Promota) akitumia
wasanii wasiosajiliwa na kuwa na vibali kutoka BASATA kwani kufanya
hivyo ni kuvunja sheria za nchi hasa sheria hiyo namba 23 ya mwaka 1984
inayoelekeza usajili na utoaji vibali kwa wadau wote wa Sanaa.
Itakumbukwa
kwamba mnamo Mwaka 2013 Serikali kupitia Sheria ya Ushuru wa Forodha
ilitangaza rasmi kuzirasmisha sekta za muziki na filamu. Sheria hii pia
inawataka wasanii wote nchini kusajiliwa na kupewa vibali na BASATA na
kinyume chake ni uvunjaji wa sheria.
Hata
hivyo, toka kuanza kwa mchakato huu wa urasmishaji sekta ya Sanaa ni
wasanii wa muziki wa injili pekee ndiyo wamekuwa wakisajiliwa kwa wingi
huku wale wa muziki wa kizazi kipya na filamu wakisuasua bila kuwepo kwa
sababu za msingi.
BASATA
limekuwa likichukua hatua kadhaa kurahisisha mfumo wa usajili wa
wasanii ambapo kwa sasa msanii anaweza kupata fomu ya usajili kupitia
mtandaoni www.basata.go.tz au kwa maafisa Utamaduni wa Wilaya na baadaye
kujaza fomu na kutakiwa kuziwasilisha BASATA zikiwa zimeambatanishwa na
wasifu binafsi (CV) wa Msanii husika.
Aidha,
gharama za usajili ni kiasi cha Tsh. 75,000/- pekee ambapo fomu
hupatikana kwa Tsh. 5, 000/-, Usajili 30,000/- na kibali cha kila mwaka
40,000/-
Kwa
upande wa studio na wakuzaji Sanaa (Mapromota) gharama ni sawa na za
msanii isipokuwa tofauti huwa kwenye kibali abapo wao hulipa kiasi cha
Tsh. 200.000/- kwa mwaka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni