.

.

14 Februari 2016

DURU YA PILI YA UCHAGUZI JAMHURI YA AFRIK YA KATI KUFANYIKA LEO


Wapiga kura katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wanarejea katika vituo vya kupigia kura Jumapili (14.02.2015) kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi unoatarajiwa kurejesha amani na uthabiti baada ya kukumbwa na vita.
Iwapo chaguzi hizo za Urais zitakuwa shwari, huenda ikawa mwanzo mpya kwa Jamhuri ya Afrika kati ambayo imezongwa na mapinduzii ya serikali, ghasia na msukosuko tangu ilipojinyakulia uhuru kutoka kwa Ufaransa zaidi ya miongo mitano iliyopita.
Wagombea wawili wanaogombea urais wote walikuwa mawaziri wakuu wa nchi hiyo na wameahidi kurejsha usalama na kuimarisha uchumi katika taifa hilo lenye utajiri wa madini lakini linakumbwa na umaskini mkubwa.
Duru ya kwanza ya uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo mwezi Desemba mwaka jana, ilishindwa na Waziri mkuu wa zamani Anicet Georges Dologuele, kwa kupata asilimia 23.78 ya kura. Dologuele almaarufu Bwana Msafi mwenye umri wa miaka 58 anasifika kwa kujaribu kuifanyia mageuzi sekta ya fedha nchini humo wakati alipokuwa Waziri mkuu.
Dologuele na Touadera kumenyana
Faustin Archange Touadera ambaye pia ana umri wa miaka 58, Professa wa somo la Hesabu na Waziri mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliibuka wa pili katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi kwa kupata asilimia 19.4 ya kura zilizopigwa.
Touadera amejipatia umaarufu kwa kuwalipa wafanyakazi wa umma mishahara yao moja kwa moja kupitia akaunti za benki bila ya kucheleweshwa wakati alipokuwa Waziri Mkuu.
Mbali na kumchagua Rais, wapiga kura watashiriki katika uchaguzi wa marudio wa bunge ambao pia ulifanyika tarehe 30 mwezi Desemba mwaka jana lakini ulifutiliwa mbali kutokana na madai mengi ya kuwepo udanganyifu katika uchaguzi huo. Wagombea 1,800 wanawania viti 105 vya bunge.
Uchaguzi wa leo wa Urais unatarajiwa kuwa kinyang'anyiro kikali kati ya wagombea hao wawili. Dologuele amepata uungwaji mkno kutoka kwa mgombea aliyeibuka nafsi ya tatu kati duru ya kwanza ya uchaguzi huku Touadera akiungwa mkono na wagombea 22 walioshiriki katika uchaguzi wa Desemba.
Mkaazi wa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Gaston ameliambia shirika la habari la AFP mkesha wa uchaguzi huo kuwa, uchaguzi wa leo ni wa kufanya maamuzi muhimu, kwani Rais ajaye madarakani atalijenga tena taifa hilo na wana matarajio mengi kutoka kwake. Raia mwingine Emilienne Namsona ambaye anaishi katika kambi ya wakimbizi ya M'poko amesema anatarajia Rais mpya kuwapokonya waasi silaha ili waweze kurejea makwao na kusema atashiriki katika duru ya pili ya uchaguzi kwani wanataraka ama
Kiongozi mpya anatarajiwa kukomesha vita
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa katika vita vya wenyewe tangu mwezi Machi mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais wa muda mrefu Francois Bozize kupitia mapinduzi ya serikali yaliyofanywa na waasi wa kundi la kiislamu la Seleka.
Mapinduzi hayo yalichochea mashambulizi ya kulipiza kisasi na kuibuka kwa kundi la waasi la Kikiristo la Anti Balaka. Maelfu ya watu nchini humo wameuawa tangu kuzuka kwa ghasia hizo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuyahama makaazi yao.
Wagombea wote wawili wa Urais ni Wakristo. Licha yakuwa chaguzi za Desemba kwa kiasi kikubwa ziliendeshwa kwa amani, usalama unatarajiwa kuimarishwa maradufu huku wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na wa Ufaransa wakisaidia katika kushika doria katika maeneo ambayo bado sio salama hasa katika mji mkuu, Bangui.
Licha ya matatizo ya kiufundi, idadi kubwa ya wapiga kura walijitokeza katika duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi Desemba. Zaidi ya kura milioni 1.3 zilipigwa katika duru hiyo. Atakayeshinda urais atakuwa na kibarua kigumu cha kurejesha utawala thabiti nchini humo, kukijenga tena kikosi cha jeshi, kuufufua uchumi na kuimarisha usalama kote nchini humo.
Chanzo:DW

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni