.

.

24 Machi 2016

JESHI LA POLISI TANZANIA KATIKA PASAKA HII


Tunapoelekea kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka ambayo inaanza kesho Ijumaa Kuu, Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi, kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali zao. Katika kipindi cha sikukuu baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu. Hata hivyo, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika mikoa yote kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Aidha, Jeshi la Polisi halitasita kumuwajibisha mzazi ama mlezi yeyote atakayeshindwa kutunza mtoto wake na kusababisha mtoto huyo kupotea au kupata madhara. Pia tunawataka wananchi wote kuwa wepesi katika kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama maeneo ya biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa ni 111 au 112.
Vilevile, Jeshi la polisi linawataka wananchi kuwa makini na watu wanaojipatia kipato kwa njia za utapeli kwa kutumia simu na mitandao. Mtu yeyote asikubali kutaja taarifa zake binafsi kwa mtu asiyemjua, mfano kutaja namba ya siri ya akaunti anayotumia kuhifadhia pesa katika simu, ama kutuma pesa kwa mtu ambaye huna uhakika naye.
Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Tunawatakia watanzania wote Pasaka njema.
Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni