Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imewatangazia kiama wahalifu, ambapo imeamua kuwasaka kwa kutumia helkopta, baada ya kupata taarifa kwamba wamekimbilia mpakani mwa mkoa huo na wa Pwani.
“Tunaendelea
na operesheni kali dhidi ya wahalifu, kwani tumepata taarifa kwamba
kuna wahalifu wamekimbilia mpakani mwa Mkoa wa Dar es Salaam na
Pwani,” alisema Kamishna wa Kanda hiyo, Suleiman Kova.
Kamishna
Kova aliyasema hayo mjini Dar es Salaam, alipozungumza na mwandishi
wetu kuhusiana na hali ilivyokuwa wakati wa Sikukuu ya Pasaka.
Alisema
Sikukuu ya Pasaka imeisha salama kutokana na kujiimarisha katika doria
mbalimbali, zikiwemo za magari, pikipiki, Vikosi vya Wanamaji, Mbwa na
Farasi.
Pia alisema waliweka vituo vya muda katika fukwe za bahari na doria ya ya helkopta ya polisi.
Aidha,
Kamishna Kova alisema wameamua kutumia mashine za ukaguzi kufanya
ukaguzi wa kawaida kwa wananchi wanaotumia kivuko cha Kigamboni.
Alisema lengo la ukaguzi huo ni kupambana na makosa mbalimbali, yakiwemo ya ujambazi na ugaidi.
Akizungumzia
operesheni ya wahalifu kwa kutumia helkopta, Kamishna Kova alisema
polisi imejipanga kupambana na wahalifu hao ambao kwa sasa wana hali
mbaya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni