Jaji
Mstaafu Thomas Mihayo alipokuwa akitoa Mada katika Semina ya Siku mbili
kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu nchini ili kulijengea uwezo Jeshi la Polisi katika
kulinda haki za binadamu kipindi cha uchaguzi. Semina hiyo imefanyika
huko Ukumbi wa Hotel ya Grand mjini Zanzibar.
…………………………………………………..
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Jeshi la Polisi nchini limeshauriwa kuzisoma kwa kina na kuzielewa vyema Sheria na kanuni za Uchaguzi kabla ya kuzitekeleza.
Kufanya hivyo kutalipelekea Jeshi
hilo kuepuka lawama na kufanya wajibu wao kikamilifu ili kuufanya
Uchaguzi unaokuja uwe katika hali ya uhuru, haki na amani.
Wito huo umetolewa na Jaji Mstaafu
Thomas Mihayo alipokuwa akitoa Mada katika Warsha ya Siku mbili kwa
Maafisa wa Jeshi la Polisi iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki
za Binadamu nchini huko Ukumbi wa Hotel ya Grand mjini Zanzibar.
Amesema Jeshi hilo linawajibu wa
kuhakikisha Sheria za nchi zinafuatwa lakini jambo la msingi ni
kuzielewa Sheria hizo kabla ya kuzitekeleza.
Jaji Mihayo amesema inashangaza
kuona kuwa Tanzania inaelekea katika kipindi cha uchaguzi Mkuu wakati
Maafisa na Makamanda hawazielewi vyema Sheria na kanuni za Uchaguzi
unaokuja.
Hivyo amewaomba Maafisa
Wawaelimishe Makamanda wenzao juu ya Sheria na kanuni za uchaguzi ili
wakati utakapofika watende haki na Wajibu wao bila ya upendeleo.
“Polisi kazi yenu nikuhakikisha
Sheria zinafuatwa lakini zitafutwa vipi wakati wenyewe hamzijui..Jambo
la msingu ni kuzisoma na kuzielewa kwanza ndio mufanye juhudi za
kutekelezwa” alisema Mihayo.
Amefahamisha kuwa Jeshi hilo
linapaswa kufuata Sheria za nchi bila kufuata matakwa ya Watawala na
kwamba Watawala hao watabadilika kulingana na uchaguzi lakini Wananchi
wataendelea kuwepo.
“Jeshi la Pilisi linawajibika kwa
Wananchi na si Viongozi wa Serikali hivyo nakuombeni mzijue Sheria na
muwe wakwanza kuzitekeleza” Alishauri Jaji Mihayo.
Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi
la Polisi Zanzibar Hamdan Makame ameshukuru Mtandao wa Watetezi wa haki
za Binadamu kwa kuendesha Semina hiyo katika kipindi muafaka cha
harakati za uchaguzi mkuu.
Amesema kila mtu ni mlinzi wa haki
za binadamu katika kila sehemu anayofanyia kazi nakwamba jambo muhimu
ni kuhakikisha Haki zinalindwa hasa ikizingatiwa kuwa suala la haki za
binadamu ni lakimataifa.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti
wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Harusi Mpatani
ameliomba Jeshi hilo kuhakikisha linawalinda Wananchi wote ikiwemo
Watetezi wa haki za binadamu.
Semina hiyo ya siku mbili
iliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini ni
mwendelezo wa kulijengea uwezo Jeshi la Polisi katika kulinda haki za
binadamu ili kuufanya uchaguzi unaokuja uwe huru,haki na Salama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni