.

.

22 Julai 2015

ZOEZI LA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA KWA MFUMO WA BVR LIMEANZA JIJINI DAR ES SALAAM









Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR limeanza jijini Dar es Salaam huku likikabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ukosefu wa mashine kwa baadhi ya vituo hali iliyosababisha wananchi kujaza fomu peke yake bila kupigwa picha.

Maeneo yaliyokumbwa na matatizo zaidi ni Kibamba, Kimara, Buguruni, Mikocheni A, baadhi ya vituo vya Temeke pamoja na Pugu ambapo baadhi ya waandikishaji katika vituo hivyo wamezungumzia changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo mashine hizo kukwama kwama hali iliyochangia kushindwa kuandikisha idadi kubwa ya watu kama walivyotegemea.

Wakurugenzi wa manispaa ya Ilala na Kinondoni wamezungumzia malalamiko hayo ambapo mbali na kukiri kuwepo kwa mapungufu katika zoezi zima kwa upande wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilala mbali na changamoto zilizotokana na mashine amesema tatizo kubwa lililojitokeza ni wafanyabiashara kutaka kujiandikishia maeneo yao ya bishara wakati wanatakiwea kujiandikia wanakoishi huku akielezea hatua wanazochukuwa kukabiliana nazo.

Kwa upande wa mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni Bw Musa Nati amesema tatizo lililojitokeza la mashine kutokufika kwa wakati kwenye baadhi ya vituo limetokana na uchache wa mashine ambapo walitarajia kupata mashine 1412 lakini wakapata 1312 kukawepo na upungufu wa mashine 100 na kwamba kuanzia sasa watu watakuwa wanapewa namba kulingana na idadi ya uandikishaji kwa siku.

Awali mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi aliwahakikishia wana Dar es Salaam kuwa mapungufu yaliyojitokeza katika zoezi hili huko mikoani hayawezi kujitokeza jijini hapa kwani mashine zote zitatumika kuandikisha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni