Klabu ya Azam imezifuata Simba na Yanga katika hatua ya 16
bora ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania baada ya kuibamiza bila huruma
timu ya daraja la kwanza African Lyon kwa mabao 4-0 katika mchezo ulichezwa Uwanja
wa Karume jijini Dar es Salaam leo.
Azam walianza kwa kasi hivyo
kuwachanganya kabisa Lyon walionekana kuwa wageni na uwanja wa nyasi bandia
pale dakika ya pili ya mchezo Mudathir Yahya akimalizia mpira uliotoka upande
wa kulia uliokung’utwa na Shomari Kapombe na kumkuta Farid aliyempenyezea
mfungaji.
Dakika ya nne ya mchezo Farid
Mussa akipokea mpira uliotumbukizwa ndani ya kisanduku cha goli na Abubakar
Salum ‘Sure Boy’ alifumua shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Lyon Hamad
Juma.
Baada ya mabao hayo ilionekana
wazi mpira kuanza kutulia kwa upande Lyon ambao katika dakika ya saba ya mchezo
walifika katika lango la Azam kwa mara ya kwanza kupitia mpira uliotumbukizwa
katika kisanduku cha goli na Mandela
Mgundi kuishia mikononi mwa kipa Aishi
Manula.
Hata hivyo uelewano wa
wachezaji wa Lyon Hamad Manzi, John Simbeya na Omar Salum uliifanya timu hiyo
icheze mchezo wa kuvutia.
Dakika ya 19 ya mchezo mpira wa
mlinzi wa kulia wa Lyon Omar Salum ulitaka kuzaa matunda lakini ukaondoshwa kwa
umahiri na Jean Baptist Mugiraneza.
Aidha dakika ya 37 ya mchezo
huo Mugiraneza alikokota mpira vizuri na kumpa pasi mpenyezo Farid Mussa ambaye
alilitazama vilivyo lango la Lyon umbali wa mita 25 na kusalimia nyavu kwa mara
ya pili.
Mshambuliaji raia wa Burundi Didier
Kavumbagu, ambaye hakucheza katika mchezo huo akifuatilia mechi jambo katika dimba la Karume Januari 25, 2016.
|
Mabadiliko yalifanyika kwa timu
zote zote mbili walipoanza kipindi cha pili Lyon wakimtoa Omary Salum na
kumwingiza Kassim Simbaulanga huku Azam wakimtoa Shomari Kapombe na kumwingiza
Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabadiliko hayo yaliipa faida
Azam ambao dakika ya 54 Ame Ally aliichambua vyema safu ya kiungo ya Lyon baada
ya Farid Mussa kumpa pasi ambayo aliitendea haki na kuipa bao la nne lililodumu
hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa na mwamuzi Kennedy Mapunda.
Baada ya mchezo huo Farid Mussa
ameisifu Lyon kwa kucheza mpira huku akiitaka kuongeza umakini na kujituma ili
kuweza kufika mbali.
Nyota huyo katika mtanange wa
leo amepiga mabao mawili na kutoa pasi za mwisho mbili hali ambayo imeongeza
kuaminiwa zaidi na kocha wake Stewart Hall.
Ikumbukwe kwamba Lyon imeshinda
mchezo mmoja tu katika michezo mitano iliyokutana na ‘Wanalambalamba’ hao.
Vikosi:
African
Lyon; Hamad Juma, Mandela Mgunda, Omary Salum/Kassim Simbaulanga,
Wiliam Otong, Hamad Manzi, Baraka Jafari, Hamis Issa, Awadh Salum, Tito Okello,
Tito Okello, Raizam Hafidh/Hood Mayanja, John Simbeya/Abdallah Mguhi.
Azam
FC;
Aishi Manula, Shomari Kapombe/Khamis Mcha, Farid Mussa, Abdallah Kheri, Erasto
Nyoni, Jean Baptist Mugiraneza/Said Morad, Michael Bolou, Abubakar Salum, John
Bocco/Allan Wanga, Ame Ally, Mudathir Yahya.
African Lyon imepata nafasi
hiyo baada ya Ashanti United kuondolewa katika michuano hiyo kwa kudanganya
jina la mchezaji Enock Balagashi ambaye katika mechi dhidi ya Lyon alitumia
Awesu Abdu katika mchezo namba 3, uliochezwa tarehe 15 Desemba, 2015.
Katika mchezo huo Ashanti
iliibuka na ushindi kwa mikwaju ya penati.
Je
wajua?
Azam FC imeanza kwa kishindo
michuano hii kwa mara ya kwanza tangu ipande ligi kuu mwaka 2008.
Azam FC imerudi kwa kishindo
baada ya kufanya makubwa jijini Tanga ilikopambana na ‘Wapiga Kwata’ wa Mgambo
JKT kwa kuwazabua kwa mabao 2-1.
Januari 25, 2012 katika mechi
namba 97 ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2011/12 African Lyon
ilikutana na Azam FC kwenye mchezo ulichezwa katika dimba la Chamazi jijini Dar
es Salaam na kumalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Aidha Januari 8, 2010 Azam FC
ilikutana na African Lyon kwenye mzunguko wa tano VPL msimu wa 2010/11
uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Azam kuibuka na ushindi wa
mabao 2-1.
African Lyon iliizabua Azam FC
kwa bao 1-0 katika mzunguko wa pili wa VPL msimu wa 2011/12 katika mchezo
uliochezwa Uwanja wa Taifa Januari 8, 2011.
Aprili 11, 2013 Azam FC
iliizabua African Lyon mabao 3-1 katika VPL katika mchezo uliochezwa Uwanja wa
Taifa.
Kagera
Sugar, Panone FC zavuka
Matokeo mengine ya
michezo mechi za leo, Kagera Sugar imesonga mbele kwa mikwaju 4-2 ya penalti
dhidi ya Rhino Rangers baada ya kumaliza wakiwa sare ya 1-1 katika dimba la Ali
Hassan Mwinyi.
Panone FC imeifutilia
mbali Madini kwa mabao 3-1 Madini katika mchezo uliocheza katika dimba la
Ushirika mjini Moshi.
Mechi za Januari 26, 2016
Januari 26 mwaka huu
kutashuhudiwa Mtibwa Sugar dhidi ya Abajalo FC (Jamhuri, Morogoro) Lipuli ikiwakaribisha
JKT Ruvu (Wambi, Mafinga)
African Sports dhidi ya jirani
zao Coastal Union (Mkwakwani, Tanga) na Geita Gold itawakaribisha Mgambo JKT (Nyankumbu, Geita).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni