Serikali
imezipiga marufuku shule zote binafsi za msingi na sekondari kuongeza
kiwango cha ada katika mwaka huu wa masomo na kuzitaka shule zote
zilizopandisha ada kinyume cha tamko la serikali kusitisha mara moja
ongezeko hilo.
Kaimu Mkurugenzi
wa Idara ya Ithibati ya Shule, Hadija Mcheka amesema kuwa kufuatia
tangazo la serikali la kuzitaka shule binafsi zinazotaka kupandisha ada
kuwasilisha maombi yao kwa Kamishna wa Elimu, shule 45 pekee ndizo
zilizowasilisha maombi hayo lakini sababu ilizotoa hazikuwa na mashiko.
Alisema kuwa shule nyingine 900 ziliwasilisha maombi ya kuendelea na kiwango cha ada ilichokuwa ikitoza mwaka jana.
Mcheka alieleza
kuwa kati ya sababu zilizotolewa na wamiliki wa shule hizo ni pamoja na
kuongeza majengo na kuajiri walimu kutoka nje, sababu ambazo Kamishna wa
Elimu aliona hazina mashiko kwa kuwa hazimhusu mzazi.
“Mwingine
anasema anataka kupandisha ada kwa vile anataka kuajiri walimu kutoka
nje ya nchi, hili nalo halimhusu mzazi ndio maana tumewanyima kibali cha
kupandisha ada. Sababu zote hizi hazikumridhisha kamishna ndio maana
tumewataka watii agizo la Serikali hadi hapo baadaye,” alisema Mcheka.
Akieleza kuhusu
mpango wa kuweka ada elekezi, Mcheka alisema kuwa serikali imemuajiri
mtaalam mwelekezi atakayefanya kazi ya kubaini gharama za kumsomesha
kila mtoto ili kuisaidia serikali kupanga ada elekezi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni