Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametoa dola za Marekani milioni 100
(US$ 100m, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 220) kutoka katika Mfuko
Mkuu wa Kushughulikia Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) kwa shughuli
za misaada katika maeneo tisa yenye dharura duniani na yasiyo na fedha
za kutosha.
Tanzania—ambayo
kihistoria imepokea mamilioni ya wakimbizi kutoka nchi jirani kwa miaka
mingi—imetengewa dola za Marekani milioni 11 (Sawa na shilingi za
Tanzania bilioni 24) kutoka katika kiasi hicho kwa lengo la
kushughulikia mahitaji ya wakimbizi kutoka Burundi.
Zaidi ya raia
126,000 wa Burundi wamekimbilia nchini Tanzania tangu mwezi Aprili,
2015, kufuatia machafuko ya kisiasa nchini humo. Huku tayari wakimbizi
64,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wakiwa tayari
nchini. Tanzania hivi sasa ina zaidi ya wakimbizi 193,000.
Kutokana na
ukweli kwamba takribani wakimbizi 1,500 wanawasili nchini kila wiki,
inabashiriwa kwamba huenda idadi jumla ya wakimbizi ikafikia 230,000
hadi mwisho wa mwaka 2016. Hali hii inasababisha changamoto nyingi hasa
katika kutoa msaada na kinga ya kutosha kwa wakimbizi.
Mchango huu
mkubwa kutoka CERF utakuwa muhimu sana katika kutoa misaada ya kiutu kwa
wakimbizi wa Burundi wanaoishi katika kambi za Nyarugusu, Nduta na
Mtendeli katika mkoa wa Kigoma, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, na
vilevile kwa jamii za wenyeji ambazo zinahitaji kwa haraka huduma bora
za maji safi, usafi wa kutosha, matunzo ya afya, chakula na makazi.
Sehemu ya fedha
hizo pia itatumika kushughulikia mlipuko uliopo wa ugonjwa wa
kipindupindu ambao umeathiri mikoa 19 nchini. Fedha za CERF kwa hiyo
zitasaidia kuhakikisha kwamba maeneo muhimu zaidi katika dharura
yanafanyiwa kazi na kwamba wakimbizi wanapewa kinga na huduma za msingi.
“Shirika la
Kushughulikia Wakimbizi (UNHCR) linakaribisha mchango huu wenye ukarimu
mkubwa kutoka CERF ambao unakuja katika kipindi mwafaka kabisa. Utoaji
msaada kwa wakimbizi ulikuwa ukikabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha
katika mwaka 2015, hali iliyoathiri sana uwezo wetu wa juhudi za pamoja
katika mwaka 2015. Tuna imani kwamba hii ni ishara ya kwanza kwa
upatikanaji wa fedha nyingi zaidi kwa utoaji msaada katika mwaka 2016.
Kwa hakika,
mchango huu utasaidia kuziba upungufu mkubwa uliojitokeza katika wito
wetu wa sasa na hivyo kushughulikia mahitaji makubwa zaidi ya wakimbizi
na jamii za wenyeji,” alisema Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Bi.
Joyce Mends-Cole.
Kadiri mahitaji
ya kiutu yanavyoongezeka, mchango kutoka katika Mfuko Mkuu wa
Kushughulikia Dharura wa Umoja wa Mataifa (CERF) umetoa matumaini ya
kuendelea kushughulikia dharura ya wakimbizi kutoka Burundi.
Tangu mwaka
2006, Nchi 125 Wanachama wa Umoja wa Mataifa na waangalizi, wahisani
kutoka sekta binafsi na serikali katika kanda zinazohusika wameendelea
kuusaidia Mfuko huo hadi sasa.
CERF hadi sasa
imetoa jumla ya dola za Marekani bilioni 4.2 (US$ 4.2bn, sawa na
shilingi za Tanzania trilioni 9) kwa miradi ya kiutu katika nchi 94.
CERF hupokea michango ya hiyari katika mzunguko wa mwaka ili kutoa
msaada wa kifedha kwa hatua za kiutu za kuokoa uhai. CERF inapata fedha
zake kutoka kwa washirika wengi huku michango mingi zaidi ikitoka:
Uingereza, Swideni, Norwei, Uholanzi na Kanada.
Chanzo: Michuzi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni