.

.

27 Mei 2015

RCC YATOA MAPENDEKEZO YA UGAWAJI MAJIMBO MBEYA

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri cha Mkoa wa Mbeya,(RCC)kimetupilia mbali mgawanyo wa majimbo manne ya uchaguzi ambayo yalipendekezwa kugawanywa kwa ajili ya uchaguzi  mkuu kwa mwaka 2015 baada ya kukosa sifa na vigezo vilivyopendekezwa na Tume ya uchaguzi kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkapa Mei 27 mwaka huu.(Picha na Fahari News)




KIKAO cha kamati ya ushauri cha Mkoa wa Mbeya,(RCC)kimetupilia mbali mgawanyo wa majimbo manne ya uchaguzi ambayo yalipendekezwa kugawanywa kwa ajili ya uchaguzi  mkuu kwa mwaka 2015 baada ya kukosa sifa na vigezo vilivyopendekezwa na Tume ya uchaguzi.

Kikao hicho pia, kimependekeza majimbo matatu yaliyomo katika Wilaya ya Momba, Mbeya na Mbozi kugawanywa kutokana na kukidhi vigezo hususani idadi ya watu.

Zoezi hilo limefanyika leo jijini Mbeya  kupitia kikao cha dharula cha kamati hiyo, kilichoketi Mkoani hapa na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali vikiwemo vyama vya siasa na wabunge.

Awali, akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro, aliwataka wajumbe kuzingatia  vigezo vya ugawaji wa majimbo wakati wa mapendekezo hayo, huku akisisitiza kigezo kikuu ni wastani wa watu, upatikanaji wa mawasiliano na ukubwa wa eneo la jimbo.

Wajumbe, hao walikubaliana na mgawanyo wa jimbo la Mbeya vijijini ambalo linaongozwa na Mchungaji Lacksoni Mwanjale kupitia tiketi ya CCM, jimbo hilo linagawanywa na kuwa majimbo mawili ya uchaguzi kwa mwaka 2015 ambayo ni Jimbo la Mbeya na jimbo la Isangati.

Jimbo la Mbeya, litaundwa na Kata 11 za Tembela, Inyala,Itewe, Njombe,Maendeleo, Igoma, Ilungu, Ihango, Lwanjilo, Ulenje na Swaya na kwamba ukubwa wa eneo hilo ni kilomita 1,225,425 idadi ya watu ikiwa ni 107,349.

Jimbo la Isangati litakuwa na Kata 15 za Masoko,Ilembo, Izyira,Iwiji, Isuto,Bonde la Songwe, Iwindi,Igale, Santiliya, Iyunga Mapinduzi, Itawa, Utengule Usongwe na Nsalala  ukubwa wa eneo ni kilomita 1,206.575 na idadi ya watu ni 221,480.

Jimbo la Mbozi Mashariki,linagawanywa na kuwa majimbo mawili ya uchaguzi ya Vwawa na Mbozi na kwamba kigezo kikuu kilichotumika ni idadi ya watu, hali ya kijiografia haijakaa vizuri pamoja na ugumu wa mawasiliano uliopo.

Lingine ni jimbo la Momba,ambalo awali lilikuwa likitambulika jimbo la Mbozi Magharibi, linagawanywa na kuwa majimbo mawili ya Momba na Tunduma na kwamba kigezo kikubwa kilichotumika ni baada ya serikali kuupandisha hadhi mji wa Tunduma na kuwa halmashauri ya mji mdogo.

Majimbo mengine yaliyotupiliwa mbali kugawanywa ni jimbo la Mbarali, Rungwe, Kyela na Mbeya mjini ambayo yameonekana kukosa sifa zilizoainishwa na tume ya uchaguzi hivyo kuendelea kubakia kama yalivyo.

Aidha, kikao hicho kimebadilisha majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo jimbo la Rungwe Mashariki limekuwa Jimbo la Busokelo huku jimbo la Mbozi Magharibi kuwa jimbo la Momba.


Hata hivyo, alisema kuwa mgawanyo huo utawasaidia wabunge watakao chaguliwa katika kutoa huduma kwa wananchi wa majimbo husika.

Mwisho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni